WAZIRI wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba ameshauri utaratibu unaofanyika katika kusaidia maendeleo ya Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini uendelee katika maeneo mengine ya nchi kwa sababu umeonyesha mafanikio makubwa. Akizindua Kongani ya Mbarali inayojumuisha mikoa miwili ya Mbeya na Songwe mkoani hapa mwishoni mwa wiki/
 Dkt. Tizeba alisema Kituo cha Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT) kimefanya kazi kubwa katika sekta ya kilimo hali inayokifanya kuwa miongoni mwa vituo vinavyohitajika barani Afrika. 
 “Utaalamu upo na uwezo wa kufanya hivyo tunao, kwa kawaida jirani anapofanya vema lazima wengine waone wivu hivyo mpango huu tuupeleke maeneo mengine ya nchi kwa kuwa hatuna sababu za kuona baadhi ya mikoa inaneemeka na mingine inabaki hivihivi,” alisema Dkt. Tizeba. Alibainisha kuwa kituo hicho kinasimamia mambo mengi katika ukanda huo wa nyanda za juu kusini ikiwemo kusimamia miundombinu hasa ya nishati, barabara na maji. Hivyo kuwepo shughuli za SAGCOT katika maeneo mengine ya nchi ni faida kwa watanzania wote. 
 “Kuchaguliwa kwa ukanda huu kulikuwa na sababu nyingi ikiwemo hali ya hewa, sababu hizohizo zitumike kupeleka shughuli hizi maeneo mengine. Kazi yetu serikali ni kuweka mazingira wezeshi na kazi hiyo tunaifanya vema,” alisema Dkt. Tizeba na kugusia changamoto zilizokuwepo kwa kusema: “Zipo changamoto zinazotukabili katika kilimo ikiwemo uduni wa teknolojia, hali inayosababisha kupanda gharama za uzalishaji kwa wakulima wadogo. 
Vilevile kuna kodi za kero kwa wakulima ambapo mkulima akishavuna anatakiwa kulipa kodi zaidi ya tatu. Haya lazima tuyatafutie ufumbuzi kwa pamoja ikiwa tunataka kusonga mbele kwenye kilimo.” 
 Akizungumza kwa niaba ya wabia wa kituo hicho Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Misaada la Maendeleo la Uingereza (DIFD), Bi. Beth Arthy alisema kinachofanyika katika ukanda huo ni jambo kubwa kwa sababu kilimo ndicho kitu pekee kitakachosaidia kukuza uchumi wa Tanzania. 
 “Mimi ni mgeni katika nafasi hii lakini nilipofika Tanzania nimezunguka maeneo mengi ya nyanda za juu kusini, nimeonana na wakulima wadogo na kujua changamoto zao, nimeona kwa macho yangu umuhimu wa sekta binafsi na sekta ya umma kufanya kazi pamoja. 
 “Bwana Kirenga,Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT na timu yake wamefanya kazi kubwa sana katika ukanda huu kwenye kilimo. Hiki wanachofanya ni wazi wanamsaidia Rais John Magufuli kufikia uchumi wa viwanda kwa sababu malighafi za viwandani zinatoka kwa wakulima,” alisema Bi. Arthy. 
 Akizungumzia safari ya kituo hicho Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Bwana Geoffrey Kirenga alisema majadiliano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma katika kusuhirikiana katika kilimo ndiko kulikosababisha kuzaliwa kwa mpango huo. 
 Alisisitiza kuwa kupewa jukumu la kusimamia kilimo katika kongani hizi ni heshima kubwa kwao na wanaahidi kufanya vizuri na kuongeza kuwa safari ya sagcot ilianza kama majadiliano kwa sekta binafsi na sekta ya umma. “Utaona tunataja eneo la ukanda huu lakini tumeligawa ktika kongani, sababu zake ni kuwa hatuwezi kufika kila sehemu kwa wakati mmoja, tunataka hadi ifikapo mwaka 2030 mbali ya mambo mengine tuwaondoe katika umasikini wakulima zaidi ya milioni mbili si jambo dogo. 
 “Vilevile tuongeze makusanyo yatokanayo na kilimo nchini, tutambue pia kufanya kazi katika kilimo changamoto yake ni rasilimali ya asili, hasa hali ya sasa ya mabadiliko ya tabianchi ukikosea unaweza usiendelee kuzalisha,” alisema Bw. Kirenga. SAGCOT ina kongani sita ambazo ni Ihemi inayojumuisha mikoa miwili ya Iringa na Njombe, Mbarali (Mbeya na Songwe), Kilombero (Morogoro), Ludewa (Ruvuma), Sumbawanga (Rukwa) na Rufiji (Pwani), ambapo katika maeneo hayo inaangaziwa ongezeko la mnyororo wa thamani katika mazao ya nyanya, viazi mviringo, chai, mahindi, mchele, soya na maziwa. 
 Wabia wa kituo hicho ni Serikali ya Tanzania, Ubalozi wa Norway, Benki ya Dunia, UKAID, USAID, UNDP na AGRA.
  Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba akifurahia baada ya kuzindua kongani ya Mbarali inayojumusiha mikoa ya Songwe na Mbeya chini ya Kituo cha Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT),
wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Amos Makala na mwakilishi wa wabia wa kituo hicho ambaye ni Mkuu wa DFID Tanzania, Bi. Beth Arthy. Uzinduzi huo ulifanyika mwishoni mwa wiki mkoani Mbeya
  Sehemu ya wabia wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT), wakiwa katika uzinduzi wa kongani mpya ya Mbarali inayojumuisha mikoa miwili ya Mbeya na Songwe mkoani Mbeya mwishoni
mwa wiki.
Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba akihutubia wadau wa kilimo waliohudhuria katika ufunguzi wa wa Kongani mpya ya Mbarali inayojumuisha mikoa miwili ya Mbeya na Songwe mkoani Mbeya mwishoni mwa wiki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...