Watanzania waishio nchini Botswana wamesifu juhudi zinazochukuliwa na Rais Magufuli za kupambana na mafisadi, wizi wa mali za umma, wafanyakazi hewa, mikataba mibovu na uporaji wa mali za nchi hasa madini. Hayo yalisemwa kwenye mkutano mkuu wa 24 wa chama cha watanzania waishio nchini Botswana uliofanyika mjini Gaborone kwenye kumbi za mikutano za Maharaja jumamosi iliyopita.
Mgeni rasmi kwenye mkutano huo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ambaye pia anaiwakilisha Botswana, Balozi Silvester Ambokile. Wageni wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na wawaikilishi kutoka NSSF, CRDB, NHC (T) LTD na Solomon Stocker Brokers.
Akimkaribisha Mh. Balozi Ambokile ili afungue rasmi mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama Cha Watanzania Botswana, Bw. Nieman Kissasi, alisema kuwa Watanzania waishio nje kwa ujumla wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano za kuinua uchumi wan chi na kuleta nidhamu mahali pa kazi.
Aidha Bw. Kissasi aliendelea kusema kuwa maendeleo yaliyoko kwenye nchi za kusini mwa Afrika yanaletwa na tabia ya viongozi na wananchi wa nchi hizo kuwa na nidhamu ya kutumia kwa uaminifu kile kidogo wanachokipata. Bw. Kissasi alisisitiza umuhimu wa Watanzania kutoa ushirikiano kwa serikali ili maendeleo ya kweli yaweze kupatikana kwa haraka.
Kwa upande wake Mh. Balozi aliwahakikishia watanzania wa Botswana kuwa serikali ya awamu ya tano itatumia uwezo wake wote ili kuwaletea watanzania maendeleo. Aidha aliwasihi watanzania waishio nje kufuata sheria na taratibu za nchi wanazoishi. Pia aliwasihi kuwekeza nyumbani na kudumisha utamaduni wa kitanzania hasa kueneza lugha ya Kiswahili.
Mh. Balozi pia alikuwa na mkutano na watanzania wote siku iliyofuata. Mkutano huu ulifanyika kwenye hoteli ya Crystal Palace na ulifuatiwa na maonyesho ya huduma zitolewazo na mashirika ya NSSF, NHC, CRDB na Solomon Stock Brockers.
Mh. Balozi alifunga mikutano hii kwa kuwapongeza watanzania waishio Botswana kwa kuwa na umoja miongoni nao na kuwasihi wale ambao hawajajiunga na umoja huo kufanya hivyo kwani ni umoja imara na uthabiti unaostahili kuigwa na watanzania waishio nchi zingine.
PICHANI: Mh. Balozi akiongea na watanzania kwenye Hoteli ya
Crystal Palace. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Watanzania Botswana, Bw. Nieman Kissasi.
Meneja wa huduma za Diaspora wa CRDB, Bi Lucy Naivasha,
akielezea huduma zitolewazo kwa
watanzania waishio nje nchi.
Meneja
wa NHC (T) LTD, Bi Sophia Mwema, akielezea huduma zitolewazo na NHC baada ya
mkutano mkuu kwenye kumbi za mikutano za Maharaja mjini Gaborone
Mh. Balozi Ambokile, wa nne kulia akiwa na baadhi ya wageni
na wanachama baada ya mkutano. Pamoja naye ni mwenyekiti wa Watanzania, Bw.
Kissasi, wa tatu kushoto, Meneja wa CRDB, Lucy Naivasha, wa kwanza kushoto,
Meneja wa NSSF, Bi. Halima Mjala, wa pili kushoto na mwakilishi wa Solomon
Stock Brockers, wa tatu kulia.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...