Na Dotto Mwaibale, Bukombe Geita
WAKULIMA wilayani Bukombe Mkoani Geita wameiomba Serikali na wasambazaji wa mbegu bora za mahindi ya WEMA 2109 yanayostahimli ukame kufikisha mbegu hizo wilayani humo ili kuweza kutatua changamoto ya mavuno kidogo wanayoyapata kila mwaka kutokana na mabadiriko ya tabia nchi na wadudu.
Ombi hilo limetolewa na wana Kikundi cha Igembensabho kwenye Kijiji cha Kabagole Kata ya Busonzo wilayani Bukombe mkoani Geita wakati wakipokea mbegu bora za mahindi yaliyozalishwa na Mradi wa WEMA kwa ajili ya kupanda kwenye shamba darasa la kikundi hicho ili waweze kuyalinganisha na aina za mahindi wanayolima kila mwaka na mahindi hayo yenye sifa ya kustahimili ukame yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB)
Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi hicho, Adam Kasalamsigwa alisema kuwa kutokana na sifa walizoambiwa na wataalamu kwenye mahindi hayo yatakuwa mkombozi kwa wakulima wengi kutokana na aina zingine za mahindi waliyozoea kupanda kushindwa kutoa matokeo waliyokuwa wakiyatarajia baada ya mvua kukata mapema kabla mahindi hayajazaa.
“Tunashukuru mmetuletea mbegu hizi ili tufanye majaribio na kuona jinsi mahindi haya yanavyostahimili ukame lakini mmetuambia tayari mmeshayafanyia majaribio kwenye maeneo mengine ya Tanzania na kuonyesha mafanikio makubwa hivyo hatuna sababu ya kusubiri hadi msimu ujao tuleteeni mbegu hizo tununue na kupanda” alisisitiza Kasalamsigwa.
Mshauri wa Jukwaa la Matumizi ya Bioteknolojia katika kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange (kulia), akimkabidhi mbegu ya mahindi ya Wema 2109, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya kwa ajili ya kupanda katika shamba darasa katika Kijiji cha Msasa kilichopo Kata ya Runzewe wilayani humo leo. Wengine kutoka kulia ni Mtafiti wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula na Mtafiti, Dk. Beatrice Lyimo kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Maofisa Ugani wakiandaa shamba darasa la mahindi ya Wema katika Kijiji cha Kabagole kilichopo Kata ya Busonzo litakalosimamiwa na Kikundi cha Igembensabho.
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bukombe, Joseph Bachibya, akizungumza na wakulima wa Kikundi cha Igembensabho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...