SERIKALI HAIJARUHUSU KOZI ZA FOUNDATION CHUO KIKUU HURIA

SERIKALI haijatoa ruhusa kwa Chuo Kikuu Huria (OUT) kiendelee kutoa kozi ya ‘Foundation’ kama ambavyo imedaiwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii.
Baadhi ya mitandao ilitoa taarifa yenye kichwa cha habari kisemacho: “Waziri Mkuu aruhusu kozi za 'Foundation' Chuo Kikuu Huria” kwa madai kuwa alitoa ruhusa hiyo jana Alhamisi, Novemba 30, 2017 wakati akiwa mkoani Singida ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu hicho.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Singida waliohudhuria mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Katoliki mjini Singida, Waziri Mkuu alisema Serikali bado inafanyia maboresho Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014.
“Kwa sasa Serikali inafanya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo kwani sera tuliyonayo haifafanui vizuri jinsi ya kuwasaidia vijana wetu wajiendeleze kwa njia ya mfumo wa elimu huria na masafa,” alisema.
“Programu kama zilizoelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo za Foundation, zinahitaji pia kufafanuliwa kwenye sera yetu, ambayo kwa sasa wataalamu wetu wanaendelea kuiboresha. Pindi itakapokamilika, tutaitolea taarifa kwa Chuo Kikuu Huria na wataalamu wataweza kushirikiana na sekta zote ili kuhakikisha jambo hili linakwenda vizuri,” alisema.
Mapema, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Tozo Bisanda alisema wamepokea barua kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwaarifu juu ya nia ya Serikali kutaka kurejeshwa kwa kozi za Foundation katika chuo hicho.
“Tayari tumekwisha wasilisha mtaala wa Foundation ulioboreshwa ili kukidhi matakwa ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), na tunasubiri mrejesho kutoka Kamisheni baada ya kikao chao, mapema mwezi ujao,” alisema Prof. Bisanda.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
S. L. P. 980,
DODOMA.

IJUMAA, DESEMBA MOSI, 2017    
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda,  baada ya kuwasili kwenye Mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mjini Singida ambapo alikuwa mgeni rasmi, Novemba 30, 2017.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika mjini Singida Novemba 30, 2017. Kushoto ni Mkuu wa Chuo Kikuu hicho na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.

 Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa (mwenye miwani mbele) akiwa na wahitimu wenzake katika Mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika mjini Singida, Novemba 30, 2017.
 Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akimtunuku Shahada ya Uzamili Katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera (Master Of Education in Administration, Planning and Policy Studies), Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa (kushoto) katika Mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika mjini Singida, Novemba 30, 2017. Wapili kulia ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Watatu kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinoloji, Profesa Joyce Ndalichako. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akitelemka kutoka kwenye jukwaa baada ya kutunukiwa Shahada ya Uzamili Katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera (Master of Education in Administration, Planning and Policy Studies) na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Waziri Mkuu MStaafu, Mizengo Pinda (kulia)  huku  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishuhudia. 
 Mke wa  Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa   akipokea ua kutoka kwa mwanae, Saad Majaliwa Kassim baada ya kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika Elimu ya Utawala, Mipango na Sera (Master of Education in Administraion, Planning and Policy Studies) katika Mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika mjini Singida Novemba 30, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...