Wizara ya Maji na Umwagiliaji imetekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kufika Tunduru na kulipatia ufumbuzi tatizo la maji katika mji huo, alilolitoa siku chache zilizopita wakati alipofanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Ruvuma.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso ameweza kufika Namtumbo kwa lengo la kujua changamoto zinazoikabili wilaya hiyo, ambapo kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji ni asilimia 21 kwa sasa.
Akizungumza katika ziara yake hiyo Aweso alisema kuwa kuna haja ya kuchukua hatua za haraka ili kuunusuru mji huo na hali mbaya iliyonayo, kwa kuipa nguvu miradi inayosuasua na kuahidi kutuma fedha mara moja ili kufanikisha jambo hilo.
‘‘Nitafanya utaratibu Sh. milioni 300 zinazohitajika zipatikane mwezi ujao, ili utekelezaji miradi inayosuasua ikamilike mara moja na wananchi waanze kupata maji kama Waziri Mkuu alivyoagiza kwani fedha ipo na ndio lengo letu kama wizara,’’ alisema Naibu Waziri.
Pia, Aweso ameagiza wakandarasi kuacha visingizio na kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa miradi kwa wakati kulingana na mikataba yao inavyoonyesha na si vinginevyo.
‘‘Umefika wakati wakandarasi kuacha visingizio ambavyo havina msingi wowote, nawaagiza wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya maji nchi nzima wakamilishe miradi hiyo kwa wakati. Kama viwanda vya vifaa mbalimbali vipo nchini, wanunue vifaa katika viwanda hivyo na si kusingizia kuchelewa kwa vifaa kwa sababu vinaagizwa kutoka nje ya nchi, wakati hakuna sababu ya kufanya hivyo,’’ alisema Naibu Waziri.
Aidha, Naibu Waziri alitembelea Wilaya ya Tunduru ambapo hakuridhishwa na hali ya utekelezaji wa miradi ya maji wilayani humo na kuagiza apate ripoti ndani ya siku tatu inayoeleza sababu za kusuasua kwa mmoja wa miradi wakati fedha zote za kutekeleza mradi huo zimeshalipwa na bado haujakamilika.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Jumaa Aweso akitoa maagizo kwa Mhandisi wa Wilaya ya Namtumbo, Bakari Mwanyiro (kushoto) na katikati ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhandisi Edwin Ngonyani katika mradi wa Rwinga wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Jumaa Aweso akikagua tenki la mradi wa Kumbara na Mhandisi Mshauri wa Mradi, Benjamin Kyaruzi wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Jumaa Aweso akiwa kwenye mradi wa Milende na Mhandisi wa Mkoa wa Ruvuma, Jones Kimaro (kushoto) katika Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Jumaa Aweso akikagua moja ya visima viwili vya mradi wa Matemanga unaotekelezwa katika Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...