Zabuni ya Ujenzi wa Mradi wa kuzalisha Umeme kiasi cha
MW 2100 kwa kutumia maporomoko ya maji katika Mto
Rufiji (Stiegler's Gorge) imefunguliwa leo tarehe 27/11/2017
ambapo Kampuni 81 zilijitokeza kununua nyaraka za Zabuni
hizo na kampuni Nne ndizo zilizorudisha nyaraka za
zabuni husika.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ugavi ya
Wizara ya Nishati, Armon Macachayo wakati wa kikao cha
Zabuni hiyo kilichofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dar es
Salaam.
Macachayo alisema kuwa baada ya ufunguaji wa Zabuni
husika, Zoezi linalofuta ni kufanyika kwa tathmini ili kupata
Kampuni moja itakayokidhi vigezo vya kukabidhiwa mradi.
Zabuni hiyo ilitangazwa tarehe 30 Agosti, 2017 ambapo
Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini, ilialika
Taasisi Binafsi na Kampuni zenye uwezo kutoka ndani na
nje ya nchi kujitokeza kuomba zabuni husika.
Akitoa taarifa za kutangazwa kwa Zabuni husika mwezi
Agosti, 2017, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani
alisema kuwa Mkandarasi atakayepewa kazi ya kujenga
mradi huo ni yule atakayeridhia kujenga mradi husika kwa
gharama nafuu na kwa muda mfupi na kusema kuwa
kukamilika kwa mradi husika kutasaidia kuimarisha
upatikanaji wa huduma ya umeme nchini.
Inatarajiwa kuwa, baada ya zoezi la tathmini na majadiliano
ya mkataba wa ujenzi kukamilika, mwanzoni mwa mwezi
Januari mshindi wa zabuni hiyo atakabidhiwa Mradi ili
kuweza kuanza kazi ya ujenzi wa mradi mara moja.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi
Innocent Luoga alishukuru kampuni zote zilizojitokeza
kununua zabuni husika na kuwakaribisha kuwekeza katika
miradi mingine ya uzalishaji Umeme.
Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga akishuhudia ufunguaji wa Zabuni ya Ujenzi wa mradi wa
Umeme wa Stiegler’s Gorge (MW 2100) uliofanyika katika Ofisi za Wizara
ya Nishati jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya
Manunuzi, Wizara ya Nishati, Armon Macachayo na wengine ni Viongozi
Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati pamoja na watendaji kutoka
Kampuni mbalimbali.
Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati pamoja na watendaji
kutoka kampuni mbalimbali zilizonunua zabuni ya Mradi wa Umeme wa
Stiegler’s Gorge wakiwa katika kikao cha ufunguaji wa Zabuni hizo jijini
Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...