Na Estom Sanga- TASAF

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- bwana Ladislaus Mwamanga amewaagiza Maafisa Ufuatiliaji na Waratibu wa Mfuko huo ngazi ya halmashauri za Wilaya nchini kote kushirikiana na Vyombo vya Habari kutangaza mafanikio ya utekelezwaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye maeneo yao.

Bwana Mwamanga amesema serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF- imefanikiwa kuzikifia kaya za wananchi waliokuwa wanakabiliwa na hali ya umaskini wa kipato ambao wameanza kukabiliana na kadhia hiyo kwa kuwekeza kwenye shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Akizungumza katika siku ya pili ya kikao kazi cha watumishi, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF ametoa mfano wa Mafanikio yaliyoanza kupatikana tangu kaya za walengwa kujumuishwa kwenye shughuli za Mpango, amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa katika uundwaji wa vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana miongoni mwa walengwa na hivyo kukuza mitaji yao na kuibua shughuli za kiuchumi hususani biashara ndogo ndogo.

Aidha bwana Mwamanga amesema walengwa wa TASAF wameanza kuboresha makazi kwa kuezeka nyumba zao kwa mabati baada ya kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi kutokana kutokana na ruzuku inayotolewa na serikali kupitia TASAF huku kukiwa na mwitikio chanya katika sekta za elimu, afya na lishe kwa kaya za Walengwa.

Kutokana na mafanikio hayo,Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amesema jitihada hizo zilizofanywa na serikali kupitia TASAF zinapaswa kuwekwa bayana na hivyo kuwaagiza Watendaji wote walioko kwenye halmashauri za Wilaya kushirikiana na Vyombo vya habari kutangaza mafanikio hayo ili kuwawezesha wananchi kutambua jitihada za kukabiliana na umaskini .

Aidha Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amesisitiza watumishi wa Mfuko huo kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa ili Mfuko huo uendelee kuaminiwa na Serikali na Wadau wengine wa Maendeleo kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amesema mwelekeo wa siku zijazo za utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo ni kuhakikisha kuwa walengwa wake wanatumia vyema fursa hiyo kwa kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa miradi ya Maendeleo na kujiongezea kipato kama njia mojawapo ya kuboresha maisha yao.
Mmoja wa Walengwa wa TASAF katika halmashauri ya mji wa Tabora, akimwonyesha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Mkuchika nyumba aliyoanza kuijenga baada ya kujiongezea kipato kwa kuanzisha mradi wa biashara ya mboga na matunda kwa kutumia fedha za ruzuku kutoka TASAF. Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF bwana Ladislaus Mwamanga (aliyeshika kipaza sauti) akizungumza wakati wa kikao kazi cha watumishi wa taasisi hiyo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Watumishi wa TASAF wakimsikiliza meneja wa miradi ya kutoa Ajira, Mhandisi Barnabas Jachi aliyeshika kipaza sauti) alipokuwa akielezea manufaa ya miradi ya ajira za muda katika kuongeza kipato cha walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Baadhi ya Watumishi wa TASAF wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi (hayupo pichani )alipozungumza kwenye kikao kazi cha taasisi hiyo kinachojadili pamoja na mambo mengine namna uboreshaji wa huduma zake kwa wananchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...