WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua ofisi ya Umoja wa Mataifa na kusema uamuzi huo ni hatua muhimu ya kuendeleza mchakato wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamsi, Desemba 7, 2017) wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa taasisi za Umoja wa Mataifa waliohudhuria hafla ya ufunguzi rasmi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Dodoma, katika eneo la Mlimwa, Manispaa ya Dodoma.
         
“Wote mtakubaliana nami kwamba uzinduzi wa ofisi hii ya Umoja wa Mataifa ni hatua muhimu sana ya kuendeleza mchakato wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Pia, inafungua mlango mpya utakaowezesha ofisi zote za kibalozi na mashirika ya kimataifa kujenga ofisi zao hapa Dodoma na kuhamia mapema,” alisema.

Alisema anatambua kwamba kwamba wapo viongozi na watendaji wenye hofu ya kuhamia na kuanza maisha mapya Dodoma. “Baadhi ya watendaji wanaogopa changamoto za kuhamisha watoto wao na wenza wao ili kuanza maisha mapya. Napenda kuwatoa hofu kwamba Dodoma ni mahali pazuri pa kuishi na kuna fursa nyingi,” alisema.  Alisema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu iliyopo ya huduma za jamii na miundombinu ya barabara, maji, umeme na mawasiliano ili iwe bora zaidi. Alitumia fursa hiyo kuwasihi waombe maeneo ya ujenzi kwa ajili ya ofisi na makazi.

Aliushukuru Umoja wa Mataifa kwa kuiteua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza mfumo mpya wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kuungana na kutekeleza shughuli zake kwa pamoja kama familia moja ya Umoja wa Mataifa yaani “UN Delivering as One”.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga alisema Umoja wa Mataifa unayo mashirika 50 na kwamba mashirika 23 kati ya hayo, yanafanya kazi zake hapa nchini. Alisema wizara yake kwa kushirikiana na Manispaa ya Dodoma, watahakikisha kuwa mashirika hayo yanapatiwa viwanja vya kutosha ili kujenga ofisi zao mapema iwezekanavyo.

Mapema, Mwakilishi Mkazi wa UNDP na Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania; Bw. Alvaro Rodriguez alisema wamefurahi kupata fursa ya kuwa taasisi ya kwanza ya  kimataifa kuwa na Ofisi yake kwenye makao makuu ya nchi hapa Dodoma


“Tumefurahi kujumuika kwa pamoja hapa Dodoma, lakini tunaahidi kuwa na sisi tutahamia kwa awamu kama ambavyo Serikali imekuwa ikifanya. Hili litategemea upatikanaji wa viwanja na majengo kwa ajili ya ofisi, kwa hiyo wafanyakazi wetu nao watahamia taratibu,” alisema.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP. nchini, eneo la Mlimwa mjini Dodoma Desemba 7, 2017. Wapili kulia ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa UNDP Bw. Alvaro Rodriguez na wanne kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dr. Augustine Mahiga.
Waziri Mkuu,. Kassim Majaliwa akifungua Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini eneo la Mlimwa mjini Dodoma Desemba 7, 2017. Kulia ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, na Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Bw. Alvaro Rodriguez.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mahariki, Dr. Augustine Mahiga akizungumza katika ufunguzi wa Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi w UNDP Nchini uliofanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, eneo la Mlimwa mjini Dodoma Desemba 7, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza kabla ya kufungua Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini eneo la Mlimwa mjini Dodoma, Desemba 7, 2017.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Bw. Alvaro Rodriguez akizungumza katika ufunguzi wa Ofisi yake uliofanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, eneo la Mlimwa mjini Dodoma Desemba 7, 2017.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...