Bandari ya Tanga kwa mara nyingine tena imepokea meli ya Mv Dubai Energy iliyobeba shehena ya “petroleum coke” (pet coke) takribani tani 27,500. Shehena hii ya “pet coke” imekuwa ikihudumiwa mara kwa mara kwa ufanisi zaidi katika bandari ya Tanga.
Hii inadhihirisha kuwa Bandari ya Tanga inayo uwezo wa kuhudumia shehena ya “pet coke” na nyinginezo zenye uzito wowote ule kama bandari nyingine yeyote duniani.
Akizungumza mara baada ya kuipokea meli hiyo Mkuu wa Bandari ya Tanga Bw. Percival Salama amesema kuwa meli hiyo inategemea kushusha shehena hiyo ya “pet coke” katika bandari ya Tanga na wamejipanga kupakua mzigo huo kwa ufanisi wa hali ya juu ili kuipunguzia meli hiyo kukaa bandarini kwa muda mrefu hivyo kuipunguzia gharama zake za uendeshaji.
''Meli hii itapakua tani 27,500 katika bandari yetu na ni mara ya kwanza kushusha shehena hii kwa mwaka huu 2018, tumejipanga kuihudumia ndani ya siku tatu ambayo ni juu ya viwango vya tija tulivyopangiwa” alisema Bw. Salama.
Aliendelea “tukifanikiwa kuihudumia meli ndani ya siku tatu tukamaliza, tutakuwa tumepunguza masaa ya meli hii kukaa bandarini kwetu kwa muda mrefu hivyo kuwapunguzia gharama za uendeshaji wamiliki wa meli, kama mnavyojua kupunguza masaa ya meli kukaa bandarini ni kivutio kikubwa kwenye biashara ya bandari kwani kinapunguza gharama za uendeshaji wa biashara za meli duniani.'' Aliongeza Bw. Salama.
“Pet coke” ni malighafi inayotumika kuunguza au kuchoma (kama makaa ya mawe) mawe au chokaa inayotumika kama malighafi kwenye Viwanda vya Saruji, Mkoa wa Tanga ni maarufu nchini Tanzania kwa kuwa na wingi wa malighafi hii ya chokaa, hivyo kuwa kivutio na fursa ya kuanzisha Viwanda vingi vya Saruji.
Shehena ya “pet coke” iliyohudumiwa katika bandari ya Tanga mwaka wa fedha 2016/2017 ni takribani tani 145,535. Shehena ya “pet coke” iliyohudumiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/2017 (Julai hadi Desemba 2016) ni tani 93,324 zikilinganishwa na tani 36,281 zilizohudumiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2015/2016. Hii ni sawa na ongezeko la tani 57,043 sawa na asilimia 38.8.
Itakumbukwa kuwa pia Bandari ya Tanga imechaguliwa kuwa lango la kupitishia mafuta ghafi kutoka Hoima, Kabaale nchini Uganda kwakuwa na sifa za kina kirefu cha kufunga meli kubwa za mafuta hadi kufikia mita 25, kuwa na kingo za asili (natural shelter) zinazozuia upepo mkali na mawimbi makubwa ya bahari na hivyo kuifanya kufanya kazi siku zote za mwaka, eneo kubwa la kugeuzia meli (turning area) pamoja na kuwa na sifa ya kuwa ni bandari pekee yenye ghuba tano nazo ni ghuba ya Tanga, Mwambani, Manza, Moa na Kwale . Mradi huu wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi unatarajiwa kukamilika mwaka 2019 na kuanza kazi katikati ya mwaka 2020.
Imetolewa na:
MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BANDARI TANZANIA (TPA)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...