Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb) leo tarehe 3 Januari, 2018
amekutana na wadau wa mchezo wa ngumi za kulipwa nchini. Kikao hicho ni
mwendelezo wa vikao vya Mhe. Waziri na Wadau hao ili kutatua migogoro
iliyodumu kwa muda mrefu katika mchezo huo wa masumbwi ya kulipwa, vikao
hivyo vilianza mwishoni mwa mwaka 2017.
Katika kikao kilichofanyika
leo, Mhe. Waziri aliwaagiza wadau hao kufanya kazi kwa pamoja katika
kuunda mfumo mpya utakaolinda maslahi ya mabondia na wahusika wengine wa
mchezo wa ngumi za kulipwa na kuliletea Taifa letu heshima kwa kupitia
mchezo huo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Ili kupiga hatua, Waziri Mwakyembe
ameunda kamati ya watu kumi na moja (11) itakayokusanya maoni ya wadau
na kupitia upya katiba ya kuunda Chombo kitakachosimamia mchezo wa ngumi
za kulipwa hapa nchini. Kamati hiyo imeanza kufanya kazi leo tarehe
03 Januari, 2018 na itakamilisha kazi yake tarehe 31 Januari, 2018.
Kamati itasimamiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na itakuwa na
wajumbe wafuatao:-:
- Ndg. Emmanueli Salehe – Mwenyekiti
- Ndg. Joe Enea – Makamu Mwenyekiti
- Ndg. Yahya Pori – Katibu
- Ndg. Habibu A. Nyogoli – Mjumbe
- Ndg. Shomari Kimbau – Mjumbe
- Ndg. Fike Wilson – Mjumbe
- Ndg. Anthony Ruta – Mjumbe
- Dkt. Killaga M.Killaga – Mjumbe
- Ndg. Ally B. Champion – Mjumbe
- Ndg. Rashidi Matumla – Mjumbe
- Ndg. Karama Nyilawila – Mjumbe
Aidha, Waziri Mwakyembe ameeleza
kwamba katika kipindi cha mpito shughuli za kutoa vibali kwa mapambano
ya ndani na kwa mabondia wanaosafiri nje ya nchi zitaendelea kutekelezwa
na BMT. “BMT endeleeni kusimamia vibali vya mapambano ya ndani na
vibali vya safari za nje ya nchi za mabondia kwa kuzingatia uzalendo,
weledi, kanuni na sheria za nchi bila kumwangalia mtu usoni wala
kumuonea aya”, amesisitiza Waziri Mwakyembe.
Imetolewa na
Octavian F. Kimario
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
03/01/2018
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...