Na: Veronica Kazimoto-Sirari
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere amewataka Wafanyakazi wa taasisi mbalimbali wakiwemo wa mamlaka hiyo wanaofanya kazi katika Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Sirari kilichopo wilaya ya Tarime mkoani Mara kufanya kazi kwa ushirikiano na kuhakikisha wanaendelea kutoza kodi stahiki.
Akizungumza wakati wa ziara yake kituoni hapo, Kamishna Mkuu Kichere alisema nchi inaendeshwa kwa kodi za ndani hivyo ni muhimu kila taasisi iliyopo eneo hilo kutimiza wajibu wake katika suala zima la ukusanyaji wa kodi.
“Wote mnajua umuhimu wa kodi na pia mnafahamu kuwa, kwa kupitia kodi hizi, Serikali inajenga miundombinu ya barabara, umeme, inasomesha wanafunzi, inajenga shule, inalipa mishahara ya wafanyakazi wake na mambo megine mengi. Hivyo, mfanye kazi kwa bidii na kwa weledi ili mkusanye kodi inayotakiwa kukusanywa kwa mujibu wa sheria bila kumuonea mtu yeyote.” alisema Kichere.
Kichere aliongeza kuwa, wafanyakazi wote kituoni hapo wana wajibu wa kukusanya kodi ili kuisaidia nchi kupiga hatua kimaendeleo kwa kutumia mapato yanayokusanywa nchini kupitia kodi mbalimbali.Aidha, Kamishna Mkuu huyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tarime kwa ushirikiano wanaoutoa kwa TRA.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...