Jamii kwa sasa imeanza kutambua na kuthamini haki za mwanamke kwenye masuala ya umiliki wa ardhi na hivyo kumpa nafasi zaidi kisheria kupata, kumiliki, kutumia na kugawa ardhi kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa wanaume.
Kuwepo kwa mabadiliko haya chanya kwa baadhi ya jamii imetokana na kusambaa kwa elimu ambayo imekuwa ikitolewa na Shirika la PELUM Tanzania kupitia mradi wa Ushiriki wa wananchi katika kusimamia sekta ya kilimo unaofadhiliwa na watu wa marekani.
Angolile Rayson ambaye ni Afisa Mradi amesema vijiji vyote 30 vya mradi ambavyo 27 kati yake toka wilaya sita za Morogoro, Mvomero, Kilolo, Mufundi, Bahi na Kongwa vimefanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi, wananachi wake walikuwa wakiendeleza mila na tamaduni potofu za kuona kuwa mwanamke si sehemu ya familia hivyo hapaswi kumiliki ardhi kwani ataolewa na kwenda kuendeleza ukoo mwingine.
Lakini baada ya kufanya mafunzo kwenye vijiji hivyo juu ya haki za mwanamke kumiliki ardhi, jamii imebadilika na sasa mwanamke si tu amekuwa akimilikishwa ardhi peke yake bali pia ana maamuzi nayo kisheria kuitumia kwa shughuli zozote za kiuchumi, kukodisha na hata akiamua kuiuza.
“Tunashukuru baada ya kutoa elimu juu ya haki za mwanamke kumiliki ardhi wakati wa kutekeleza mpango wa matumizi ya ardhi, wanaume wengi wamewapa wenza wao maeneo wamiliki kwa majina yao wenyewe na wengine wamemiliki umiliki wa pamoja yaani mke na mume na zaidi ya yote hata watoto wa kike kwenye baadhi ya familia wamepewa maeneo na wazazi wao wamiliki. Shirika kupitia Hamlashauri za wilaya husika tumewapimia maeneo yao na kwa sasa wanasubiri hatimiliki za kimila ili wawe na umiliki halali jambo ambalo sisi kama Shirika tumeona ni sehemu kubwa ya mafanikio.” Alifafanua Angolile
Wananchi wa Kijiji cha Mawala, Wilaya ya Kilolo Iringa, wakisaidia kutekeleza baadhi ya shughuli za mpango wa matumzi ya ardhi ya kijiji chao.
Bahati Mwinyimvua mwananchi toka kijiji cha Melela Wilaya ya Mvomero Morogoro. Akichangia hoja kuhusiana na umiliki wa ardhi kwa wanawake
Ng’eng’enu Mambega katibu wa kamati ya maamuzi kijiji cha Mela, wilaya ya Mvomero Morogoro akibainisha jinsi elimu ya umiliki wa ardhi kwa wanawake ulivyosaidia kuwabadili kifikra na kuwapa wenza wao maeneo wayamiliki.
Angolile Rayson Afisa mradi toka Shirika la PELUM Tanzania akichangia mada kuhusiana na mpango wa matumzi ya ardhi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...