Na Mathias Canal, WK, Kahama-Shinyanga
Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba amefungua masoko ya tumbaku Kitaifa huku akitoa onyo kali kwa wakulima waliolima zao hilo nje ya mfumo wa ushirika kwa mujibu wa sheria ya zao hilo kwa kuwataka kuacha mara moja kwani serikali itashughulika na wote wanaokiuka taratibu za kilimo hicho.
Dkt Tizeba ameyasema hayo leo 12 Juni 2018 katika viwanja vya kata ya Mwendakulima Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga wakati akihutubia mamia ya wakulima wa tumbaku kwenye sherehe za ufunguzi wa masoko ya tumbaku Kitaifa.
Dkt Tizeba amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Zainabu Telack kufanya kikao na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Wilaya zote za Mkoa huo kuhakikisha wanazuia wananchi kulima nje ya mfumo wa ushirika kwa mujibu ya sheria ya zao la tumbaku.Alisema kuwa wigo wa soko la tumbaku unazidi kuwa finyu kutokana na viongozi mbalimbali kuwakumbatia baadhi ya wakulima wa tumbaku wanaolima nje ya mfumo wa zao hilo.
Katika sherehe hiyo Mhe Dkt. Tizeba amekabidhi vyeti vya pongezi kwa wakulima waliofanya vizuri katika msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 ambao ni mkulima Emmanuel Cherehani kutoka Wilaya ya Ushetu aliyeshika nafasi ya kwanza, nafasi ya pili ni Jimson Mwanjwenga kutoka Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya na Jonas Blakali kutoka Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita.
Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akimkabidhi cheti cha pongezi Mkulima Jonas Blakali kutoka Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita ambaye ameshika nafasi ya tatu katika msimu wa kilimo cha tumbaku wa mwaka 2017/2018 wakati wa sherehe za ufunguzi wa masoko ya tumbaku Kitaifa iliyofanyika katika viwanja vya kata ya Mwendakulima Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, leo 12 Juni 2018.
Mgeni rasmi-Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akikata utepew kuashiria ufunguzi wa masoko ya tumbaku Kitaifa katika sherehe iliyofanyika kwenye viwanja vya kata ya Mwendakulima Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, leo 12 Juni 2018.
Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akishuhudia ununuzi wa tumbaku wakati wa sherehe za ufunguzi wa masoko ya tumbaku Kitaifa iliyofanyika katika viwanja vya kata ya Mwendakulima Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, leo 12 Juni 2018.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...