Na Hamza Temba-WMU-Moshi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ametoa wito kwa taasisi za Serikali, jamii, sekta binafsi na wadau kwa pamoja kushirikiana kuendeleza utalii katika maeneo yao ili sekta hiyo iweze kunufaisha zaidi taifa kwa kiwango kinachostahiki kuliko ilivyo hivi sasa.

Ametoa wito huo juzi katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi wakati akifungua maonesho ya kimataifa ya utalii ya Karibu/Kili Fair 2018 ambayo yameshirikisha makampuni na wadau wa utalii zaidi ya 350 kutoka nchi zaidi ya 12 duniani huku na kuvutia watu zaidi ya 4,000 kuyatembelea.

Amesema ushirikiano huo utaiwezesha sekta hiyo kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa ambao kwa sasa ni takriban asilimia 17.2 ya pato la Taifa, zaidi ya asilimia 24 ya mapato yote ya fedha za kigeni sambamba na zaidi ya asilimia 10 ya ajira zote nchini.

Amesema mchango huo bado ni mdogo ukilinganisha na aina na idadi ya vivutio vilivyopo hapa nchini.Dkt. Kigwangalla amesema Serikali ya awamu ya tano imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali zitakazosaidia kuboresha sekta hiyo ikiwemo ujenzi unaoendelea wa reli ya kisasa ya Standard Gauge, ujenzi wa Terminal 3 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Saalam na uboreshaji wa Shirika la Ndege la ATCL.

Pamoja na hayo amesema Serikali kupitia wizara yake inaendelea na mpango wa kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini ili kuongeza idadi ya watalii na mapato ambapo Mapori matano ya Akiba mkoani Kagera na Geita yatapandishwa hadhi kuwa Hifadhi za Taifa (Burigi, Biharamulo, Kimisi, Ibanda na Rumanyika).

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Bodi ya Utalii Tanzania, Jaji Mst. Thomas Mihayo (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla kuhusu Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 kabla ya kuzindua maonesho hayo katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye (wa tatu kulia), Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa Kampuni ya Kilifair Promotion, Tom Kunkler (kushoto).
Kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Bodi ya Utalii Tanzania, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo na Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Devotha Mdachi wakiwa katika meza kwenye hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilifair Ltd,Tom Kunkler, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Mkurugenzi wa Karibu Fair, Dominick Shoo na viongozi wengine wa Serikali na sekta binafsi wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kuzindua Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye na viongozi wengine wa Serikali na sekta binafsi wakiwa kwenye eneo la mfano wa kilele cha Uhuru cha mlima Kilimanjaro baada ya kuzindua Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi. 
Waziri Kigwangalla akisalimia baadhi waoneshaji katika banda la utalii wa kiutamaduni kwenye maonesho hayo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...