Leo Mbunge wangu Mwalimu Kasuku Bilago, Mbunge wa Buyungu utalala katika nyumba yako ya milele, utalala hutaamka tena, familia yako itakukosa, wananchi wa Buyungu watakukosa, ndugu jamaa na marafiki hatutakuona tena mtu uliyefanya siasa za kistaarabu, uliyetanguliza mbele maslahi ya wananchi wake na uliyetamani chama chako cha CHADEMA kufanya siasa zenye mwelekeo wa maendeleo.

Tangu kauli yako izimike Mei 26, 2018 katika hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam, nimekumbuka mengi tuliyozungumza na uliyoniambia kwa dhati ya moyo wako. Mengi hayajatimia lakini hayo ndio maisha ya mwanadamu.

Nakumbuka sana siku ile Julai 21, 2018 baada ya Rais John Magufuli kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Kibondo - Nyakanazi Mkoani Kigoma, yenye urefu wa Kilometa 50 uliniambia umefurahishwa sana na kuanza kwa ujenzi huo, ulisema barabara hiyo ikikamilika italeta ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Kibondo likiwemo jimbo lako la Buyungu.

Ulinibonyeza kuwa bahati mbaya ndani ya chama chako cha CHADEMA kushabikia miradi ya maendeleo sio jambo linalopendwa sana, ulinidokeza kuwa linapokuja suala la maendeleo upo tayari kutofautiana na viongozi wako wa chama.

Nakumbuka uliniambia kuwa hata uliposalimiana na Rais Magufuli ulimwambia upo tayari kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilimradi wananchi wako wa Buyungu wapate maendeleo. Nilikuamini kwa sababu hata maneno uliyozungumza baada ya kupewa nafasi ya kusalimu wananchi ulijikita kuzungumzia maendeleo na kumshukuru Rais Magufuli na serikali yake.
Ndio maana nasema umeondoka kabla ndoto yako haijatimia, najua kuwa ulikuwa njiani kuhamia CCM, hukupenda kumaliza nguvu zako na muda wako kushabikia mabishano ya kisiasa badala ya kuelekeza nguvu kuwapigania wananchi wa Buyungu. Najua kwa namna Rais Magufuli alivyozungumza nawe kwa bashasha, ungekaribishwa ndani ya CCM na ungepewa nafasi ya kuwatumikia wananchi ili ukate kiu yako.

Kifo hiki kimezima ndoto zako, kimeondoa neema kwa wananchi wa Buyungu. Najua ndani ya CHADEMA ulishaanza kusemwa vibaya kutokana na kuwepo hisia kuwa ulikuwa mbioni kuhama chama. Ulianza kuwekewa maazimio mabaya, ulianza kutishwa.

Nasikia minong’ono ya wana CHADEMA wanaotaka kifo chako kichunguzwe, kuna hofu kuwa umeuawa. Kuna wasiwasi kuwa msimamo wako wa kupingana na viongozi wakuu wa chama chako na nia yako ya kutaka kuhamia CCM vimesababisha kifo chako.

Kuna hofu kuwa umeuawa kama ambavyo viongozi wengine wa chama chako cha CHADEMA akiwemo Mhe. Chacha Wangwe waliuawa, kuna hofu kuwa umeuawa ili usifikie uamuzi wako wa kukihama chama kwa kuwa ungekidhohofisha chama kama walivyokidhohofisha akina Dk. Godwin Mollel na madiwani lukuki wa CHADEMA waliokihama chama hicho na kujiunga na chama Tawala.

Mimi rafiki yako nitafurahi kuona uchunguzi huu unafanywa, japo kuwa nami ulinishawishi kujiunga na CHADEMA lakini natafakari sana uanachama wangu, na kama nilivyokuahidi kuwa ukihama na mimi nitahama. Sasa umeondoka, nakuahidi kuwa nikimaliza msiba na mimi nitahamia kwenye chama kilichotayari kupigania maendeleo ya wananchi na sio porojo na kutishiana usalama.

Mwalimu Bilago kwa heri, unalala leo milele lakini tunakulaza wakati viongozi wako wa CHADEMA wakiwa wametukwaza sana sisi ndugu na marafiki zako wa Buyungu. Kifo chako kimegeuzwa kuwa mtaji wa kisiasa, wameanzisha mabishano na Bunge bila sababu za msingi, Spika Mhe. Job Ndugai alikuja kukuzika lakini ameondoka bila kukuzika.

Unazikwa huku vichwa vya habari vya magazeti vikiwa vimeandikwa bila heshima kwako “Mazishi ya Bilago yaibua utata, Ndugai aondoka” hilo ni gazeti la Mwananchi, “Mazishi ya Mbunge Chadema fugisu tupu, Spika akabidhi mwili na kuondoka, Chadema wabaki kuzika leo” hilo ni gazeti la Tanzania Daima. 
Naomba kutoa pole kwa wote walioguswa na kifo chako Mwalimu Kasuku Bilago, nakuombea radhi kwa Spika wa Bunge Job Ndugai, na nakuombea radhi kwa wote waliokwazika na vitendo vya viongozi wa CHADEMA kugeuza msiba wako kuwa mtaji wa kisiasa, nakuombea Mwenyezi Mungu akupumzishe mahali pema peponi na pia awape uvumilivu, subira na ustahimilivu ndugu wote na hasa Mke wako uliyempenda sana na familia yako.

Saimon Michael
Kigoma.
Mei 31, 2018


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...