Na Zainab Nyamka,Globu ya jamii

MWEKEZAJI katika klabu ya Simba, Mohammed Dewji 'MO' ameanzisha tuzo zitakazotolewa kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wa klabu ya Simba ambazo amezipa jina la Mo Simba Awards.

Kwa mara ya kwanza tuzo hizo zitatolewa Jumatatu ya Juni 11 mwaka huu katika hoteli ya Hyatt Regency – Kilimanjaro iliyopo Jijini Dar es Salaam.

Tuzo hizo zitakuwa na vipengele 16, ambavyo ni Mchezaji Bora wa Mwaka, Goli Bora la Mwaka, Golikipa Bora wa Mwaka, Beki Bora wa Mwaka, Kiungo Bora wa Mwaka, Mshambuliaji Bora wa Mwaka, Shabiki Bora wa Mwaka na Tuzo ya Heshima.

Pia tuzo zingine ni Mchezaji Bora Mwanamke wa Mwaka, Mchezaji Bora Mdogo wa Mwaka, Tuzo ya Benchi la Ufundi, Kiongozi Bora wa Mwaka, Tuzo ya Wasimamizi wa Mchakato wa Mabadiliko, Mhamasishaji Bora wa Mwaka katika Mitandao ya Kijamii, Mhamasishaji Bora wa Mwaka na Tawi Bora la Mwaka.

Washindi wa tuzo hizo watatokana na kura ambazo zitapigwa na mashabiki kupitia mitandao ya kijamii na tovuti ya mosimbaawards.co.tz na kamati maalumu ya tuzo ambayo itahusisha wadau mbalimbali wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.

Akizungumza kuhusu tuzo hizo, Dewji amesema ameanzisha tuzo hizo kwa lengo la kutambua mchango wa wachezaji, viongozi na mashabiki ambao juhudi zao zimeiwezesha Simba SC kupata mafanikio iliyonayo sasa.

Dewji amesema tuzo hizo ni sehemu ya mikakati yake ya kuifanya klabu ya Simba kuwa timu kubwa barani Afrika, ambayo itakuwa na uwezo wa kifedha ambao utaiwezesha kuwa na wachezaji na benchi la ufundi bora ambalo litaiwezesha kushinda mataji makubwa.

"Simba ni timu kubwa inastahili kuwa na tuzo zake ambazo zitakuwa zinatolewa kwa kutambua mchango wa wenzetu ambao umetuwezesha kupata mafanikio haya ikiwepo kushinda taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Ni jambo ambalo litawatia moyo kuendelea kujituma lakini hata kwa ambao watakosa itawatia hamasa na hivyo kuongeza juhudi," amesema Dewji.

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo itakuwa mbashara kupitia Azam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...