Na Ripota Wetu, Arusha

MAISHA ya wanawake 250 waliopo Kata ya Lemooti na Mswakini Monduli mkoani Arusha yanataraji kubadilika baada ya Asasi ya Watu na wanyama(TPW) kuwapatia Sh.milioni 40 za mradi wa uhifadhi mazingira na ufugaji nyuki.

Kupitia mradi huo wanawake hao kutoka kwenye vijiji sita vya Mswakini Juu, Mswakini chini, Lengolwa, Lemooti, Oldonyo na Naitolia watapatiwa mizinga 475 itakayofungwa kwenye maeneo ya vikundi 25 vya watu 10. Akizungumza wakati wa kukabidhi mradi huo leo, Msimamizi wa miradi Asasi ya TPW Revocatus Magayane amesema mradi huo wanautekeleza kwa ushirikiano na Baraza la Wanawake wa Kifugaji Monduli (BAWAKIMO).

Magayane amewataka wanawake hao kutoa taarifa za maendeleo ya mradi kila wakati hatua itakayowawezesha kuwa na mwanzo mzuri wa utekelezaji. Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Monduli Iddi Kimanta aliwataka wanawake hao kutoingiza siasa kwenye shughuli zinazohusiana na maendeleo kwani kufanya hivyo kutawafanya wakwame kufikia ndoto zao.

“Uchumi hauna itikadi ya kisiasa, mkiingiza siasa kwenye masuala haya mtahawanyika na kushindwa kufikia mnachokihitaji kama kuwa na maisha mazuri kusomesha watoto na kujenga nyumba bora na kisasa,” alisema Kimanta. Naye Katibu wa BAWAKIMO Nai Zakayo ameishukuru TPW kwa kuwawezesha kupata na kuanzisha mradi huo wa nyuki kwenye kata mbili za wilaya hiyo.

Aidha ameiomba TPW kuwafikia wanawake wengi zaidi kwani bado wanayo maeneo mengi katika Kata nyingine ambazo zinaweza kufanya miradi ya uhifadhi wa mazingira na ufugaji wa nyuki.
Mkuu wa wilaya ya Monduli Iddi Kimanta akipokea mfano wa Hundi ya zaidi ya Sh milioni 40 kutoka kwa Msimamizi wa Miradi wa Asasi ya Watu na Wanyama (TPW),Revocatus Magayane kwa ajili ya mtaji wa mradi wa ufugaji nyuki kwa wanawake 250.
Mkuu wa wilaya ya Monduli Iddi Kimanta akibadilishana mawazo na Msimamizi wa Miradi wa TPW Revocatus Magayane mara baada ya kukabidhi mradi wa ufugaji nyuki kwa wanawake 250 wa Kata ya Lemooti na Mswakini.
Mratibu wa Miradi kutoka BAWAKIMO Angela Kagashe akizungumza na baadhi ya wanawake wanachama wa baraza hilo juu ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo mpya wa uhifadhi mazingira na ufugaji wa nyuki wilayani Monduli. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...