NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
JESHI la polisi mkoani Pwani ,linaendelea na ukaguzi kwa madereva na magari ambapo leseni za madereva 1,710 zimekaguliwa huku leseni ya mmoja ikionesha akiwa amezaliwa mwaka 1951 huku akionyesha kuwa na umri mdogo.
Aidha madereva watano walikamatwa kwa kosa la kutokuwa na leseni ,madereva saba walikamatwa kwa kutokuwa na sifa daraja la D/L,PSV.
Akielezea kuhusiana na ukaguzi huo, kaimu kamanda wa polisi mkoani Pwani, Blasius Chatanda ,alisema dereva mwingine mmoja leseni yake ilionyesha amezaliwa mwaka 1951 wakati anaonyesha yeye akiwa na miaka 27 huku akiendesha gari la abiria.Alisema ukaguzi huo ni endelevu na atakaebainika kwenda kinyume na sheria za usalama barabarani atatozwa faini ama kufikishwa mahakamani.
Chatanda aliwaasa madereva ,kubadilika kwa kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka kugharimu maisha ya watu na wengine kubakia na ulemavu wa viungo.Pamoja na hayo ,alikemea baadhi ya madereva wanaoendesha kwa mwendo kasi na wale wanaotumia vileo .
Akielezea mikakati wanayoendelea nayo kudhibiti ajali za barabarani ,alisema ifikie wakati madereva wakatumia taaluma zao kwa kuendesha wakiwa makini bila kukiuka sheria jambo linalosababisha ajali ambazo nyingine ni za uzembe wa madereva.
Chatanda alieleza wamejipanga kufanya misako ya usiku na mchana, mara kwa mara kwa magari makubwa na madogo hadi watakapohakikisha ajali zinapungua kabisa."Tuna askari wetu wa usalama barabarani waliotanda kama utitiri kwenye barabara zetu za mkoa ,tuna vipima vileo ,ambapo tunahakikisha dereva atakaekutwa na kosa lolote la kukiuka sheria zinazostahiki atakiona" alisisitiza Chatanda.
Pia kunafanyika operesheni za mara kwa mara ili kuwakamata wale madereva bodaboda watakaokuwa hawataki kutii sheria bila shuruti kwa kuwachukulia hatua kali na kuwafikisha mahakamani ili kupunguza ajali na vifo kwa waendesha pikipiki.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...