Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi na Kaimu Meneja Uhusiano Mamlaka Hifadhi ya Ngorongoro, Joyce Mgaya wakisaini hati ya makubaliano ya kuboresha mandhari ya mizunguko ya magari kwenye barabara kuu za jiji hilo. Kwenye uboreshaji huo wa mandhari Mamlaka Hifadhi ya Ngorongoro itaweka vivutio mbalimbali kutangaza utalii.
Na Abuu Kimario
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeingia makubaliano na Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kuboresha mandhari ya mizunguko ya magari (roundabout) kwenye barabara
kuu za jiji hilo.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo kwenye hafla ya fupi ya kutiliana saini ambapo jiji
la Dodoma liliwakilishwa na Meya, Profesa Davis Mwamfupe na Mkurugenzi Mtendaji,
Godwin Kunambi na upande wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iliwakilishwa na
Kaimu Meneja Uhusiano, Joyce Mgaya kwa niaba ya Mhifadhi Mkuu wa mamlaka hiyo
Dkt. Fredy Manongi.
Kwenye makubaliano hayo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekubali kuifanyia
ukarabati mizunguko mitatu ya magari ambayo ni mizunguko ya barabara kuu za Dar-
es-Salaam (Shabiby), Singida na Arusha.
Akiwasilisha salamu za Mhifadhi Mkuu, Kaimu Meneja Uhusiano Mgaya amesema,
uongozi wa jiji la Dodoma kuichagua mamlaka hiyo ni heshima kubwa na wanaipokea
kwa mikono miwili na pia mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na halmashauri ya jiji
kwenye kuibua fursa mbalimbali za kitalii.
Aidha, Mgaya ameongeza kuwa makubaliano hayo yaliyofikiwa ni fursa ya Halmashauri
ya jiji la Dodoma na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kubadilishana uzoefu kwenye
maeneo ya uhifadhi wa mazingira na kuboresha mandhari.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Dodoma, Mstahiki Davis Mwamfupe amesema nia ya
uongozi wa jiji la Dodoma ni kulifanya liwe jiji la mfano wa kuigwa na majiji mengine
ya Tanzania, barani Afrika na duniani kwa kuwa na mazingira bora kuishi na mandhari
yenye kuvutia.
Nae Mkurugenzi Mtendaji, Godwin Kunambi ameishukuru Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro kwa kukubali ombi la kutengeneza sanamu kubwa ya tembo kama ishara
ya kuhifadhi historia ya chimbuko la jina la mkoa wa Dodoma. Kwa mujibu ya maelezo
ya wenyeji wa mkoa huo jina Dodoma limetokana na neno la kigogo “idodomya”
baada ya tembo kudidimia ardhini miaka mingi iliyopita.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...