WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya kutowajibika miongoni mwa watumishi kwa kisingizio cha mgawanyo wa madaraka.
Ametoa onyo hilo jana (Jumamosi, Julai 7, 2018) wakati akizungumza na wanaushirika na mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Furahisha, jijini humo.
Amesema kuna maafisa ushirika ambao hawataki kuwajibika kwa sababu wameajiriwa TAMISEMI na wengine wako chini ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika."Afisa Ushirika wa Wilaya yuko mkoani ambako ni chini ya TAMISEMI, Mrajis Msaidizi wa Mkoa yuko Wizarani. Serikali ni moja, kwa hiyo wote bado mnawajibika kwa Mrajis Msaidizi wa Mkoa," alisema.
Aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri (DED) wasiwapangie kazi nyingine zilizo nje na taaluma yao maafisa ushirika wa wilaya na wahakikishe wanatoa taarifa kwenye vikao vya Halmashauri zao.
"Msimpe kazi ya kufundisha Afisa Ushirika kwa sababu hakuna mtu mwingine. Afisa Ushirika aachwe afanye kazi ya ushirika na atoe taarifa kwenye vikao vyenu. Madiwani mnapokutana kwenye Baraza, mpeni nafasi Afisa Ushirika aeleze maendeleo ya ushirika yakoje katika wilaya yenu."
Alisema changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya ushirika ni wizi na ubadhirifu miongoni mwa watendaji wa vyama vya ushirika waliopewa dhamana ya kuvisimamia na kuviendesha vyama hivyo.Alisema changamoto nyingine ni ukosefu wa elimu ya kutosha ya ushirika miongoni mwa wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika; kuporomoka kwa imani ya ushirika miongoni mwa jamii na kwa baadhi ya wanachama kutokana na vyama vya ushirika kushindwa kukidhi mahitaji ya wanachama wake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...