Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni kumi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za
askari polisi kote nchini, ikiwa ni kukabiliana na changamoto ya makaazi ya askari
na uchakavu wa vituo vya polisi ili kuwawezesha askari hao kutekeleza majukumu
yao kwa ufanisi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi
Hamad Masauni alipotembelea kijiji cha Makongoro wilaya ya Bunda mkoani
Mara kuona changamoto wanazokutana nazo askari polisi katika kutekeleza
majukumu yao ya ulinzi na usalama.
Alisema wizara iko katika mpango maalumu wa kuboresha makazi ya askari polisi
nchini huku akitoa wito na nafasi kwa wadau wa maendeleo pia kujitokeza na
kuunga mkono juhudi za Rais Dk.John Magufuli kuboresha makazi ya askari
polisi
“Katika kukabiliana na changamoto ya askari nchi nzima tayari tushaanza kujenga
makazi ya askari wetu tukianza na nyumba za polisi Kusini Pemba na tutaendelea
na ujenzi huo wa nyumba 400 katika mikoa mingine nchini na kutokana na hali
niliyoiona hapa Bunda basi tutatoa kipaumbele hapa”Alisema Naibu Waziri
Masauni
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili,
ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanashirikiana na serikali katika ujenzi wa
makazi ya askari polisi wilayani humo huku Mwenyekiti wa Kijiji hicho Mussa
Masilu aliongeza kuwa nyumba hizo ni chakavu na zinashusha hadhi ya Askari
Polisi
Hadi sasa serikali imeshaanza taratibu za awali ikiwemo tathmini ya ujenzi wa
nyumba hizo mia nne za askari polisi nchini ambapo mikoa mbalimbali itanufaika
na ujenzi huo utakaotekelezwa kwa awamu tofauti ukienda sambamba na ujenzi
na ukarabati wa vituo vya polisi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akikagua moja
ya makazi ya askari polisi katika kijiji cha Makongoro B, kilichopo wilayani Bunda
wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua na kushughulikia changamoto za makazi ya askari
polisi ambapo jumla ya nyumba mia nne za askari polisi zinatarajiwa kujengwa nchi
nzima.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akisoma
maelezo ya mmoja ya mtuhumiwa aliyemkuta katika chumba cha mahabusu katika Kituo
cha Polisi Bunda wakati wa ziara ya kikazi ya kupitia shughuli za utekelezaji wa
mashtaka ya mahabusu walioko katika vituo vya polisi nchini.Wapili kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili na wengine ni viongozi waandamizi wa kamati ya
Ulinzi na Usalama wilayani Bunda.
Afisa Mnadhimu wa Polisi mkoa wa Mara, Mrakibu Mwandamizi ,Jeremiah Shila akitoa
maelezo ya mwenendo wa mashtaka ya watuhumiwa walioko katika Kituo cha Polisi
Bunda kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni(wapili kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili(watatu kulia),
wakati wa ziara ya naibu waziri kupitia shughuli za utekelezaji wa mashtaka ya
mahabusu walioko katika vituo vya polisi nchini.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (watatu
kushoto), akifuatilia wakati mpelelezi akifunua jalada la mmoja wa mahabusu
aliyemkuta katika chumba cha mahabusu katika Kituo cha Polisi Bunda wakati wa ziara
ya kikazi ya kupitia shughuli za utekelezaji wa mashtaka ya mahabusu walioko katika
vituo vya polisi nchini.Wapili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili na
wengine ni viongozi waandamizi wa kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Bunda.Picha
na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...