*Mkurugenzi Mtendaji Kadogosa asema ujenzi umekamilika kwa asilimia 22
*Wajumbe Bodi ya Wakurugenzi washuhudia kasi ya ujenzi kuanzia Dar
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii.
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania(TRC) Masanja Kadogosa amesema kwa sasa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti wizi wa mafuta huku akieleza kuna baadhi ya madereva wamefukuzwa kazi kutokana na tuhuma hizo.
Kadogosa amesema hayo leo katika eneo la Soga mkoani Pwani ambapo kuna kambi ya wafanyakazi wanaojenga Reli ya Kisasa ambapo ameelezea namna ambavyo wamedhibiti wizi wa mafuta kwa kuimarisha ulinzi kwa kushirikiana na mamlaka za ulinzi na usalama.
Sababu za kuelezea hayo ni baada ya baadhi ya waandishi waliokuwa kwenye ziara ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC wakiongozwa na Mwenyekiti wao Profesa John Kondoro kutaka kufahamu hali kutokana na kuwepo kwa taarifa za uwepo wa wizi wa mafuta.
"Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti wizi wa mafuta katika mradi huu.Ni tofauti na hapo awali, tumeimarisha ulinzi na sasa tumefanikiwa kudhibiti wizi huo.
"Kuna watu 30 wamekamatwa kwa tuhuma za wizi wa mafuta na tayari wamefunguliwa kesi.Pia katika kukomesha vitendo vya wizi kuna baadhi ya madereva ambao tumewafukuza,"amesema Kadogosa.
VIPI KUHUSU UJENZI WA RELI?
Akizungumzia ujenzi wa reli hiyo ya kisasa ambayo awamu ya kwanza ni kutokea Dar es Salaam hadi Morogoro, Kadogosa amewaeleza wajumbe wa bodi hiyo kwamba ujenzi umekamilika kwa asilimia 22.
Amesema katika ujenzi wa reli hiyo kuna hatua mbalimbali za ujenzi zinazoendelea na kila eneo kwa asilimia tofauti na eneo jingine lakini kwa ujumla wake ujenzi umefikia asilimia 22 na ujenzi unaendelea kwa kiwango cha kuridhisha.
Ameongeza ujenzi wa madaraja unaendelea na tayari zimeanza kuwekwa , ujenzi wa tuta nao unaendelea na maeneo maeneo mengine wameanza kuweka kokoto kwa ajili ya kuanza kutandika mataluma.
Mradi mradi wa reli ya kisasa ya standard gauge ulipofikia baadhi ya maeneo.
Mataaluma yakiwa tayari kwaajili ya kwenda kuwekwa kwenye maeneo ambayo reli ya kisasa itapita.
Maeneo yanayoendelea kujengwa reli ya kisasa eneo la Mlandizi.
Picha na Avila Kakingo, Globu ya jamii.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...