Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inatoa pole kwa familia zote ambazo
zimepoteza ndugu na jamaa zao na wengine kujeruhiwa katika ajali ya barabarani
iliyohusisha magari matano, iliyotokea katika eneo la Igawilo Mjini Mbeya siku ya
tarehe 7 Septemba, 2018 na kusababisha vifo vya watu 15 na kujeruhi wengine.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Kangi Alphaxard Lugola,
(MB), kwa masikitiko makubwa anatoa pole kwa familia zote zilizopoteza
wapendwa wao na kuwatakia majeruhi wote ahueni ya haraka ili warejee katika
hali zao za kawaida na kuendelea na shughuli zao za kujenga nchi.
“Natoa pole nyingi kwa Watanzania wenzangu waliowapoteza wapendwa wao
katika ajali hii na nawatakia majeruhi wote afya njema na wapate ahueni
haraka ili waweze kurejea katika hali zao za kawaida”.
“Ni wakati muafaka kwa Watanzania wenzangu, Wasimamizi wa Sheria za
Usalama Barabarani na Madereva kutokatishwa tamaa na ajali hii na badala
yake changamoto hii iwafanye waongeze umakini barabarani, kuongeza
umadhubuti katika usimamizi wa Sheria ya Usalama barabarani kwa kuchukua
hatua kali zaidi kwa madereva wazembe na askari wasiotimiza wajibu wako wa
kuhakikisha magari mabovu hayaruhusiwi kutembea barabarani”.
Mwenyezi Mungu azipe roho za ndugu zetu pumziko la amani. Amina
Imetolewa na:
Meja Jenerali Jacob G. Kingu, ndc
KATIBU MKUU
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...