Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Joseph Nyamhanga, ameagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kumuandikia barua mkandarasi wa Kampuni ya Impesa di Construzioni anayejenga kituo cha ukaguzi wa pamoja (one stop inspection station) eneo la Manyoni mkoani Singida na Nyakanazi mkoani Kagera kurejea eneo la kazi na kuendelea na ujenzi.

Akizungumza katika kijiji cha Muhalala mkoani Singida wakati wa ukaguzi wa kituo hicho, Katibu Mkuu huyo amesema Serikali tayari imeshashughulikia madai ya mkandarasi huyo, hivyo hana sababu ya kutoendelea na ujenzi wa mradi huo. “Naagiza Mkandarasi huyu arudi eneo lake la kazi na kuanza kazi ya ujenzi wa mradi huu mara moja”, amesema Mhandisi Nyamhanga.

Aidha, Mhandisi Nyamhanga, ameeleza kuwa jumla ya gharama za mradi wa vituo hivyo ni takribani shilingi bilioni 55, ambayo itahusisha gharama za ujenzi, usimamizi na fidia.Mhandisi Nyamhanga amefafanua kuwa ujenzi wa kituo hicho unaenda sambamba na ujenzi wa kituo kingine eneo la Nyakanazi mkoani Kagera ambapo kituo kingine cha vigwaza mkoani Pwani kimeshakamilika na hivyo kutafanya jumla ya vituo vikuu vitatu vya ukaguzi vyenye umbali wa kilomita 500 kutoka kwa kila kimoja.Amefafanua kuwa lengo la ujenzi wa mizani hizo ni kupunguza vizuizi barabarani na gharama za usafirishaji wa mizigo kupitia barabara ya ukanda wa kati.

Kwa sasa magari ya mizigo husimama takriban katika vituo 31 ambapo kati ya hivyo vituo nane ni vya mizani, vituo 20 ni vya polisi na vituo 3 ni vya ukaguzi wa mapato ambavyo vyote viko kati ya Dar es Salaam hadi mipaka ya Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa umbali wa kilomita 1000.Awali, akitoa taarifa za maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida Mhandisi Masige Matari, amesema ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 60 na kazi zinazoendelea kutekelezwa ni kama vile barabara zinazoingia na kutoka kituoni.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, akikagua moja ya boksi kalvati iliyojengwa katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa KM 85.4 kwa kiwango cha lami, Mkoani Tabora.
Muonekano wa baadhi ya nyumba za watumishi wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Polisi watakaoishi mara baada ya ujenzi wa Kituo cha Ukaguzi wa Pamoja kukamilika katika kijiji cha Muhalala, Wilayani Manyoni, Mkoani Singida.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri Adel alkhateeb, anayesimamia ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa KM 85.4 kwa kiwango cha lami wakati alipoukagua mradi huo, Mkoani Tabora.

Muonekano wa kazi zikiendelea za ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya yenye urefu wa KM 85.4 kwa kiwango cha lami, mkoani Tabora. Ujenzi wa sehemu ya barabara hiyo utafungua mkoa huo na mikoa ya Katavi na kigoma.



Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Singida Mhandisi Masige Matari, akitoa taarifa ya mradi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja (One Stop Inspection Station), katika kijiji cha Muhalala, wilayani Manyoni, mkoani humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...