Na Ibrahim Mdachi, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) ameahidi kukisaidia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kuwa anatambua mchango wake katika utoaji mafunzo ya Sheria nchini.
Waziri wa Katiba na Sheria ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za Mahafali ya 18 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Novemba 23 alisema kuwa Serikali inatambua mchango wa Chuo hiki katika kutoa mafunzo ya sheria kwa ngazi ya Stashahada na Astashahada na katika kutoa mafunzo endelevu katika fani mbalimbali za sheria.
“Ninaahidi kutimiza wajibu wangu kwa kutoa msaada pale mtakapohitaji na nitakapoona sina budi nitatoa msaada huo hata kama hamjaleta rasmi hitaji lenu kwangu.” Alisema Prof. Kabudi.Akiendelea kuhutubia hadhara ya Wahitimu, Watumishi wa Chuo na Mahakama Wazazi na Walezi wa wahitimu, Prof. Kabudi aliongeza kuwa wahitimu wa chuo hiki wamekuwa mfano kwa jamii kwa uadilifu na maadili kutokana na malezi wanayopata chini ya usimamizi wa Mahakama ya Tanzania.
Alipongeza Uongozi wa Chuo kwa jitihada unazozifanya katika kukabiliana na changamoto mbalimbali na namna unavyoweza kuzikabili na kuweza kutekeleza jukumu lake la utoaji wa mafunzo sambamba na utekelezaji wa miradi mbalimbali.Sambamba na hayo aliwaasa na kuwasisitizia Wahitimu na juu ya kujiendeleza katika fani ya Sheria ambayo huhitaji kusoma kwani sheria na kanuni hubadilika kila mara na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Mhe. Prof Kabudi aliwataka Wahitimu hao kuendelea kusoma vitabu kwa wingi kwani itawasaidia katika utendaji kazi wao wa kila siku.Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Jaji, Prof. Paul Kihwelo alisema kuwa Chuo kimeendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa Watumishi wa Mahakama ili kuwajengea uwezo zaidi.
“Kwa kutambua umuhimu wake kwa Mahakama ya Tanzania pamoja na kuwajengea uwezo wa utafiti watumishi wake, Chuo kimeendesha mafunzo yaliyowajumuisha Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata mkoani Tabora ili kuwajengea uwezo wa namna wanavyopaswa kusikiliza mashauri katika ngazi zao,” alieleza Mkuu huo wa Chuo. 

Mhe. Waziri, mgeni rasmi (aliyeshika kipaza sauti) akiongoza sherehe za Mahafala ya ‘IJA’ Lushoto.
Waziri wa katiba na Sheria akipewa maelezo ya jinsi mfumo wa Kielektroniki wa Menejimenti ya Mafunzo ‘Training Management Information System (TMIS)’ unavyofanya kazi, Mhe. Waziri alizingua rasmi mfumo huo ambao utakuwa ukitoa taarifa ya Mafunzo mbalimbali na kuwezesha kujua ni Watumishi wangapi wa Mahakama waliopatiwa Mafunzo na ambao hawajapata mafunzo.
Meza Kuu katika picha ya pamoja na sehemu ya Wahitimu wa Astashahada ya Sheria.
Meza kuu ikiongozwa na Mhe. Mgeni rasmi (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wahitimu wa Stashahada ya Sheria.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...