Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe
(kulia) leo akimsikiliza Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, Bi. Doris
Uhagile (katikati), akimpa maelezo mbalimbali wakati alipofanya ziara ya kikazi
kwenye kiwanja hicho. Mwenye tai nyekundu ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela na kushoto ni Mkuu
wa Wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Ruyangu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe
akipita eneo la ukaguzi wa abiria na mizigo la Kiwanja cha Ndege cha Bukoba,
leo alipofanyua ziara ya kikazi. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushari (MAB) ya
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Prof. Ninatubu Lema.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, Bi. Doris Uhagile
(katikati) leo akiwa eneo la ukaguzi wa tiketi za abiria ambapo alitoa maelezo ya
namna mashirika ya ndege yavyohudumia abiria kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela, akifuatiwa na
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya TAA, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema.
SERIKALI inafikiria kufanya upanuzi na urefushaji wa barabara ya kutua na kuruka kwa
ndege ya Kiwanja cha Ndege cha Bukoba licha ya changamoto zilizopo, ili kiruhusu
kutua kwa ndege kubwa zaidi.
Hayo yamesemwa leo (jana) na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi
Isack Kamwelwe katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu ya taasisi
zilizopo chini ya Wizara yake, ambapo kiwanja hicho kipo chini ya Mamlala ya Viwanja
vya Ndege Tanzania (TAA).
Mhe. Kamwelwe amesema bado Kiwanja hicho kinakabiliwa na changamoto endapo
kitaongezwa lazima baadhi ya nyumba za Ibada, hospitali na nyumba za kuishi watu
zitalazimika kuondolewa ili kupisha upanuzi huo.
“Ukiangalia upande mmoja unamakazi ya watu na upande mwingine ni Ziwa Viktoria na
mwingine kuna Mlima, hivyo bado tunafanyia kazi hizi changamoto na endapo
zitatatuliwa basi miundombinu hii itaboreshwa zaidi kwa kuwa tayari lipo jengo zuri na
lenye mfumo mzuri wa maji taka na mifumo mingine mbalimbali,” amesema Mhe.
Kamwelwe.
Hata hivyo, amesema Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) litaongeza safari zake mara
mbili kwa siku wenye Kiwanja cha ndege cha Bukoba, kutokana na kuwa na abiria
wengi kwa sasa.
Mhe. Kamwelwe amesema kwa sasa ndege hiyo aina ya Bombardier Q400 inakuja
mara moja kwa siku kwa kila siku kuanzia Jumatatu hadi Jumapili.
“Kwa sasa abiria wameongezeka zaidi nimeelezwa kuwa kwa mwaka ilikuwa kiwanja
kinaweza kuhudumia abiria 28,000 pekee, lakini sasa ni zaidi ya 45,000 kwa mwaka,
hivyo inaonesha ni kiasi gani wanavyoongezeka na ndio maana ninasema kutakuwa na
uwezekano wa kuongeza safari za ATCL na iwe mara mbili kwa siku balada ya sasa
mara moja,” amesema Mhe. Kamwelwe.
Amesema serikali tayari imenunua ndege mbili aina ya Airbus 220 zenye uwezo wa
kubeba abiria 132 zitakazowasili nchini Desemba 18 na 23, 2018 tayari kwa safari za
maeneo mbalimbali.
Ndege hizi zinaweza kutua kwenye viwanja vya ndege vya daraja la 4C, ambapo kwa
sasa ni Songwe na Mwanza, na baada ya ukarabati kukamilika kwenye kiwanja cha
Mtwara na kuboreshwa kwa Kigoma, pia itaweza kutua; hali kadhalika pia itatua kwenye
viwanja vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA), ambavyo ni
daraja la 4E.
Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kinajengo la kisasa la abiria, ambalo lilizinduliwa
Desemba 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe
Magufuli, ambapo mbali na ATCL ndege nyingine zenye ratiba maalum zinazotua ni
pamoja na Precision, wakati nyingine zinakuwa zimekodiwa bila kuwa na ratiba maalum
kama Auric.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...