Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wilayani Mkinga, wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kabla kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo. 
Baadhi ya watumishi wa umma wilayani Mkinga wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao, kabla ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo. 
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiteta jambo na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Bi. Zena Said, kabla ya kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao, kabla ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo. 
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Bi. Zena Said (kushoto) akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kabla kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo. 
Afisa Utumishi Mwandamizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Baraka N. Nangosongo akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa watumishi wa umma wilayani Mkinga wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kabla kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo. 



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amemuagiza Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Bi. Zena Said kuhakikisha watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga wanaoishi nje ya vituo vya kazi kuhamia wilayani Mkinga ndani ya siku saba ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati. 

Agizo hilo amelitoa wilayani Mkinga wakati wa kikao kazi na watumishi wa halmashauri hiyo, alipowatembelea kuhimiza uwajibikaji kabla ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo kwa lengo la kukagua na kujiridhisha kuhusu utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo. 

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga wanaoishi nje ya vituo vya kazi na kutumia rasilimali za serikali, ni dhahiri kuwa wanatumia vibaya rasilimali za umma hivyo wanafanya kosa kwa mujibu wa Kanuni, Sheria na Taratibu za Utumishi wa Umma. 

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesisitiza kuwa, ni marufuku kwa mtumishi wa umma yeyote nchini kuishi nje ya kituo cha kazi, kwani kitendo hicho kinawanyima haki ya msingi wananchi wanaohitaji huduma katika Taasisi za Umma kutokana na watumishi wengi kuchelewa kufika kazini kwasababu ya kuishi nje ya vituo vyao vya kazi. 

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amehoji uwepo wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga na wakuu wake wa Idara kushindwa kushughulikia tatizo hilo la watumishi kuishi nje ya vituo vya kazi, na kumtaka Mkurugenzi huyo kuhakikisha anashirikiana na menejimenti yake kushughulikia suala hilo kwa wakati na kuongeza kuwa, iwapo tatizo hilo litaendelea kuwepo wilayani humo, itakuwa ni ishara tosha kwamba, wamedhihirisha kutokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao. 

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa umma wilayani humo kuzingatia nidhamu ya kazi na kutochezea fursa waliyonayo ya kuutumikia umma na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwa na utumishi wa umma wenye viwango na unaomjali mwananchi pindi anapofuata huduma katika taasisi za umma. 

Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amemuagiza Katibu Tawala Mkoa wa Tanga na Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kushughulikia ubadhirifu wa fedha uliopo katika Kituo cha Afya cha Kiwegu na kutaka apatiwe mrejesho mapema iwezekanavyo. 

Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Bi. Zena Said amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga na Maafisa Utumishi kuhakikisha ifikapo Februari 21 mwaka huu, watumishi wote wanaoishi nje ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga wawe wameshahamia wilayani Mkinga. 

Bi. Said amemshukuru Dkt. Mwanjelwa kwa kuwahimiza watumishi wilayani Mkinga kuvaa mavazi yenye staha na kumtaka kila mtumishi wa umma wilayani humo kuzingatia Waraka wa Mavazi Na. 3 wa Mwaka 2007. 

Kuhusiana na ubadhirifu wa fedha katika Kituo cha Afya cha Kiwegu, Bi. Said amemuahidi Dkt. Mwanjelwa kutekeleza maelekezo aliyoyatoa kwa wakati kwa kufanya ufuatiliaji ili kutatua tatizo hilo. 

Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Tanga yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi kwa umma, ikiwa ni pamoja na kukagua na kujiridhisha na utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na TASAF mkoani humo. Mpaka sasa ameshatembelea Halmashauri ya Mji wa Tanga, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...