Trekta aina ya URSUS likiendelea na kazi yakulima mashamba ya wakulima katika Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro.

Kazi
ya uunganishaji matrekta katika Kiwanda cha Kuunganisha Trekta
kilichopo Kibaha mkoani Pwani ikiendelea ikiwa ni juhudi za Serikali ya
Awamu ya Tano kufufua na kukuza sekta ya Kilimo hapa nchini ambapo
matrekta zaidi ya 200 yameunganishwa na kuuzwa kwa wakulima mbalimbali
nchini.
Moja ya Trekta aina ya URSUS likiwa limekamilika.

Matrekta yaliyounganishwa yakiwa tayari kuuzwa.
Sehemu ya majembe ya matrekta ya URSUS yakiwa tayari yameunganishwa Kiwandani Kibaha mkoani Pwani.

Trekta aina ya URSUS likiendelea na kazi yakulima mashamba ya wakulima katika Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro.

Mkulima
kutoka Wilaya ya Gairo, Haji Salum akifanyia majaribio ya kuendesha
trekta aina ya URSUS mara baada yakukabidhiwa trekta hilo alilonunua
kutoka Kiwanda cha kuunganisha matrekta kilichopo Kibaha mkoani Pwani.
(Picha na MAELEZO)
Na: Lilian Lundo - MAELEZO
Kiwanda
cha Kuunganisha Trekta Aina ya URSUS kilichopo Mkoani Pwani kimekuwa
mkombozi mkubwa kwa wakulima wadogo kutokana na masharti nafuu ya
ukopeshaji wa trekta hizo.
Kutokana
na urahisi wa upatikanaji wa trekta hizo umepelekea kuongezeka kwa
idadi ya wakulima wenye trekta ambazo zimekuwa zikiwalimia wakulima
wadogo wadogo kwa gharama nafuu.
Akizungumia
Trekta hizo, Mkulima wa zao la Mahindi na Alizeti kutoka Gairo, mkoani
Morogoro, Haji Salum ambaye alikutwa kiwandani hapo akichukua trekta
aliyoinunua kwa mkopo, ameeleza kuwa anafuraha kubwa ya kumiliki chombo
hicho ambacho atakitumia kulimia mashamba yake pamoja na wakulima
wenzake.
"Ninayofuraha
kubwa kupata chombo hiki ambacho sikutarajia kukimiliki katika maisha
yangu. Ninamshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kauli mbiu yake ya ujenzi wa
viwanda ambayo imetuwezesha hata sisi maskini kumiliki trekta," amesema
Salum.
Mkulima
huyo anayemiliki heka 120 za mashamba ya mahindi na alizeti mkoani humo
amesema, kwa kulima mashamba yake peke yake anauwezo wa kurejesha fedha
ambazo zimebaki kukamilisha malipo ya trekta hiyo anayoimiliki.
Mkulima
huyo amewashauri Watanzania kujitokeza kwa wingi kununua trekta hizo
kwani masharti yake ni nafuu na zipo kwa ajili ya kila Mtanzania hata
wale wenye kipato cha chini.
Aidha,
mmiliki mwingine wa trekta hizo kutoka Wilaya ya Malinyi, Mkoa wa
Morogoro Jacob Mbifile ameishukuru Serikali kwa kupata trekta kwa
gharama nafuu ambayo anaitumia kulima mashamba yake pamoja na kuwalimia
wakulima wenzake kwa kuchangia kiasi kidogo kwa ajili ya marejesho ya
mkopo na uendeshaji wa chombo hicho.
"Kwa
sasa tunalima kwa wakati, kutokana na uwepo wa trekta nyingi, tofauti
na ilivyokuwa zamani, ambapo wakulima wengi walikuwa wakipata huduma ya
kulimiwa kwa kuchelewa kutokana na uchache wa trekta uliokuwepo hivyo
kusababisha kuvuna mazao machache kutokana na kuchelewa kupanda,"
ameeleza Mbifile.
Kwa
upande wake, Mkulima wa zao la Mpunga Wilayani humo, Ladislaus Kidunda
amesema kabla ya uwepo wa trekta hizo, kulikuwa na uhaba mkubwa wa
trekta hivyo kusababisha foleni kubwa ya kusubiri trekta ili kulimiwa.
"Kipindi
cha nyuma tulikuwa tukipata huduma ya kulimiwa kwa trekta kwa tabu sana
kutokana na wamiliki wa trekta hizo kuwapa kipaumbele wale wenye
mashamba makubwa kuanzia heka 10 na kuendelea. Tofauti na ilivyo sasa
ambapo wamiliki wamekuwa wengi hata sisi wenye heka mbili au tatu
tunaweza kupata huduma hiyo kwa wakati," amesema Kidunda.
Nae
Msimamizi Mkuu wa Kiwanda hicho, Godwin Mubi amesema mpaka tarehe 15
Januari mwaka huu, jumla ya trekta 261 zimenunuliwa kwa njia ya mkopo
katika mikoa ya Manyara, Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Singida na Morogoro na
mikoa mingine ikiwa kwenye mchakato wa kununua trekta hizo.
"Tunakopesha
trekta hizi kwa kila Mtanzania anayehitaji, ambapo hutakiwa kutoa
asilimia 25 ya gharama ya trekta na gharama inayobaki atairudisha kwa
kipindi cha miaka miwili. Njia nyingine ni ile ambayo mkulima anaonesha
dhamira ya kupata trekta, hivyo hulipia milioni 3 hadi 4 na kiasi
kinachobaki hurejesha katika kipindi cha miaka miwili," amesema Mubi.
Aidha
Mubi ameeleza, spea za trekta za Ursus zipo na zinapatikana kwa wingi
nchini hivyo Watanzania watembelee kiwandani hapo kujua namna ya
kumiliki trekta hizo kwani masharti na gharama yake ni nafuu.
Kiwanda
cha Kuunganisha Trekta za Ursus ni kiwanda kinachosimamiwa na Shirika
la Taifa la Maendeleo (NDC) ambapo huunganisha Trekta zinazokuja kwa
vipande kutoka nchini Poland. Kiwanda hicho kilianza rasmi kufanya kazi
Aprili, 2017 ambapo ni moja ya matunda ya kauli mbiu ya Mhe. Rais Dkt.
John Pombe Magufuli ya ujenzi wa viwanda.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...