Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii
MFANYABIASHARA Isack Mwasenga (40) Mkazi wa Kanga Chunya mkoani Mwanza, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi likiwemo la kukutwa na vipande 14 vya meno ya tembo na utakatishaji fedha.
Mwasenga amefikishwa mahakamani hapo leo Februari 28, 2019 na kusomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi Augustino Rwizile.
Akisoma hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon amedai, Desemba 21, mwaka jana huko katika nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Ubungo jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa na vipande 14 vya meno ya tembo vyenye thamani ya USD, 45,000 sawa na sh. 102,150,000 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Pia imedaiwa, mshitakiwa baada ya kukutwa na vipande hivyo, alitumia fedha hizo wakati akijua kwamba ni zao la uwindaji haramu. Hata hivyo, mshitakiwa haruhusiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida zinasikilizwa mahakama kuu au mpaka mahakama itakapopewa kibali na DPP
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 12, mwaka huu kesi itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.Mshitakiwa amerudishwa rumande
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...