NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuuchunguza ujenzi wa kibanda cha kuhifadhia jenereta ya kuvuta maji katika mradi wa maji wa Ruaha Mbuyuni, wilayani Kilolo mkoani Iringa kinachodaiwa kujengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 20.
Mbunge wa jimbo la kilolo vennance Mwamoto akimuelezea Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso juu ya mradi huo wa maji unavyoleta changamoto kwa wananchi wa jimbo la kilolo
Hichi ndio kibanda cha kuhifadhia jenereta ya kuvuta maji katika mradi wa maji wa Ruaha Mbuyuni, wilayani Kilolo mkoani Iringa kinachodaiwa kujengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 20.



NA FREDY MGUNDA,IRINGA

NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuuchunguza ujenzi wa kibanda cha kuhifadhia jenereta ya kuvuta maji katika mradi wa maji wa Ruaha Mbuyuni, wilayani Kilolo mkoani Iringa kinachodaiwa kujengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 20.

Aliyasema hayo juzi katika ziara yake ya siku moja wilayani humo kukagua miradi mbalimbali ya maji, ikiwemo ile inayosuasua kwasababu mbalimbali.

“Nimepata taarifa eti kibanda hiki kimejengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 20,” alisema na kuuliza ukweli wa taarifa hizo kwa mhandisi wa maji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Enock Basyagire aliyesema hakuwepo katika halmashauri hiyo wakati kikijengwa na kuomba akapitie nyaraka ili kujiridhisha. 

Aliwahimiza Takukuru kulifuatilia jambo hilo kwa haraka na kama kutakuwa na kile alichoita “matumizi mabaya ya fedha za umma” wahusika wakamatwe na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria. Wakati huo huo, waziri Aweso ameoneshwa kusikitishwa kwake kuona katika mradi huo, tenki kubwa la kuhifadhi maji limejengwa katika eneo lisilo na chanzo cha maji; ambalo kwa mujibu wa taarifa ya mhandisi wa halmashauri hiyo, gharama yake ni zaidi ya Sh Milioni 45. 

“Huu ni uhuni, mmejenga tenki la Sh Milioni 45 na halijawahi kuwa na maji; mimi sio mtaalamu wa maji lakini najua, huwezi kujenga tenki katika eneo lisilo na chanzo cha uhakika cha maji, ni bora hapa mngechimba kisima kirefu huenda mngepata maji kwa ajili ya wananchi hawa wakati mkisubiri mradi mkubwa,” alisema. 

Akitoa onyo kwa wahandisi wa maji kuacha kucheza na fedha za umma huku akiwataka wataalamu wa maji kutoka Bonde la Rufiji kufanya utafiti kujua eneo linaloweza kuwa na maji yatakayonusuru mradi huo ambao utekelezaji wake ulianza awamu ya nne ya Dk Jakaya Kikwete, Aweso alisema: 

“Serikali haipo tayari kuona wataalamu wanaotakiwa kuwasaidia wananchi kupata maji, wanatengeneza mazingira ya kula fedha za umma. Alimuita mhandisi huyo mbele ya wananchi waliokuwepo wakati akikagua tenki hilo na kumtaka kuwaomba radhi kwa ujenzi huo ulioshindwa kuzingatia mambo ya kitaalamu; ombi lililopokelewa vizuri na wananchi hao. 

Katika kukabiliana na changamoto za matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maji inayosimamiwa na halmashauri, alisema Wizara imeamua kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini hatua inayotarajiwa kusaidia kukomesha tabia hiyo. 

Alisema wakala hiyo itakapoanza itasaidia kupunguza au kumaliza ulaji wa fedha za miradi ya maji na wahandisi wasio na nia njema katika kushughulikia kwa weledi changamoto za maji katika maeneo yao, wataondolewa na nafasi zao watapewa wengine. 

Awali Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto alimwambia naibu waziri huyo kwamba kata ya Ruaha Mbuyuni ni moja ya maeneo yenye changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama katika jimbo hilo. Mwamoto alisema ukosefu wa maji safi na salama katika kata hiyo umewaweka wananchi wake katika mazingira hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipundupindu ambacho hutokea mara kwa mara. 

“Leo umekuja mwenyewe, umejionea na umesikia kutoka kwa baadhi ya wananchi, naomba uwaondoe hofu wananchi hawa,” alisema huku naibu waziri akiahidi kuishughulikia changamoto hiyo kwa kasi kubwa. Mwenyekiti wa Kijiji cha Ruaha Mbuyuni, Adam Danando alisema sehemu kubwa ya wananchi wa kijiji na kata hiyo wamekuwa wakitegemea maji ya bonde la mto Lukosi yenye chumvi na bakteria ambao ni hatari kwa afya zao. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...