*Awataka wasikubali kutoa rushwa kwa chombo chochote 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa kati na wadogo wa Kariakoo ambapo amewataka wasikubali kutoa rushwa kwa chombo chochote.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inapiga vita vitendo vya rushwa, hivyo wakiona kuna mazingira ya rushwa watoe taarifa kwani rushwa ni adui wa haki.

Waziri Mkuu amekutana na wafanyabiashara hao leo (Alhamisi, Februari 28, 2019) katika ukumbi wa Anatouglo jijini Dar es Salaam. Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imepata mafanikio makubwa baada ya kupiga vita rushwa.

“Rushwa si sehemu ya mkakati wa Serikali, hivyo vita dhidi ya rushwa lazima iendelezwe na watu wote. Mafanikio tuliyoyapata ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa huduma za afya ni matokeo ya kupiga vita rushwa.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka watumishi wawe na tabia ya kuwatembelea wafanyabiashara kwenye maeneo yao na kusikiliza kero zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi.

“Kila mtendaji katika eneo lake atekeleze majukumu yake kikamilifu Urasimu, dharau, lugha za ajabu zimeshamiri kwenye maeneo ya kutolea huduma jambo ambalo si sahihi. Badilikeni.”

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imepanga mpango wa kulibadilisha utaratibu wa kufanya biashara katika eneo la Kariakoo ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa saa 24 kama yalivyo masoko makubwa duniani.

Waziri Mkuu amesema lengo la madiliko hayo ni kukuza uchumi wa Taifa na wa wafanyabiashara kwa ujumla. “Nchi yetu ina usalama na ulinzi wa kutosha hivyo hatuwezi kushindwa kufanya biasahara wakati wote.

Katika mkutano huo alioutisha kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao, Waziri Mkuu amesema kesho atakutana na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam ili kupanga namna ya kutekeleza mpango huo.

Waziri Mkuu amesema jiji la  Dar es Salaam ndio jiji la kibiashara nchini, hivyo Serikali inataka kuhakikisha mwenendo wa biashara unaboreshwa pamoja na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kufanyabiashara zao wakati wote.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu  amemuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda kufanya mazungumzo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsiia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuhusu ziunganisha Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Waziri Mkuu amesema TFDA na TBS zinafanya kazi ambazo zinafafa hivyo Mawaziri hao wakutane na wafanye mapitio ya kazi za mamlaka hizo na waandae muswada kuunganisha mamlaka hizo na kuuwasilisha bungeni. 

Amesema mamlaka hizo zikiunganishwa zitaweza kuondoa malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakilalamikia kuwepo kwa tozo nyingi na urasimu unasababisha Taifa kupoteza makundi makubwa ya wafanyabiashara na wateja.

Waziri Mkuu amesema mamlaka hizo zimekuwa zikitumia muda mrefu kwa ajili ya kupima bidhaa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara. “Sijui mnatumia kemikali gani ambazo zinachelewesha majibu. Na sasa TBS napima hadi stuli na mashati na mnapoona havina ubora hamuwarudishii wenyewe.”

Amesema kuna mwananchi mmoja aliagiza madirisha na bidhaa nyingine kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba yake akaamiwa havina ubora. Kila taasisi ifanyekazi yake kwa mujibu wa sheria na waache uonevu na kuomba rushwa.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na  wafanyabiashara wa kati na wadogo wa Kariakoo kwenye ukumbi wa Anatouglo jijini Dar es salaa,, Februari 28, 2019.  Kushoto ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda akizungumza kaika kikao cha wafanyabiashara wa kati na wadogo alichokiitisha, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye ukumbi wa  Anatouglo jijini Dar es salaam, Februari 28, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya wafanyabiashara wa kati na wadogo wa Kariakoo wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Anatouglo jijini Dar es salaam, Februari 28, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...