Ni zaidi ya miaka miwili tangu atutoke Shakila Bint Said, aliyekuwa nguli katika miondoko ya muziki wa taarabu humu nchini na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.

Wakati wa uhai wake, aliweza kuonesha umahiri wake wa uimbaji wa taarabu katika bendi zote alizowahi kuzitumikia.

Shakila alifariki ghafla ambapo Binti yake wa mwisho aitwaye Shani, alisikika kupitia vyombo mbalimbali vya habari akisema kuwa mama yake Bi. Shakila alianguka gahfla alipokuwa akifagia muda mfupi mara baada ya kufanya ibada ya magharibi nyumbani kwake Charambe jijini Dar es Salaam Agosti 19, 2016.

Alikuwa na Weledi wa kujuwa jinsi ya upangiliaji wa sauti kupitia maneno ya lugha adhimu ya Kiswahili katika nyimbo zake zote alizoimba.

Shakila hakuimba nyimbo za mapenzi pekee, alikuweza kuimba nyimbo zinazoigusa jamii, za siasa na Ukombozi. Wasifu wa Bi. Shakila unaeleza kuwa alizaliwa mnamo Juni 14, 1947, Wilayani Pangani, mkoa wa Tanga.

Miaka ya nyuma zao la Mkonge lilikuwa na soko kubwa ulimwenguni, Tanganyika wakati huo ikiuwa ni nchi mojawapo iliyokuwa ikizalisha kwa wingi zao hilo.Wamiliki wa mashamba ya Mkonge walikuwa wakiwachukua watu ‘Manamba’ kuwapeleka kufanya kazi ya vibarua katika mashamba hayo.

Manamba hao walipofika huko waliamua kuoa wake akiwemo Mzee Said Hamis baba yake aliyekwenda Tanga akitokea wilayani Kiomboi mkoani Tanga. Mzee huyo alifuatana na vijana wenzake kutafuta vibarua katika mashamba ya Mkonge.

Mzee huyo alioa mwanamke aliyekuwa wa kabila la Zigua toka mkoani Tanga wakaweza kumpata mtoto wakampa majina ya Tatu bint Said.Alikulia katika malezi mema ya baba na mama yake, na alipofikisha umri wa kwenda shule, aliandikishwa kuanza masomo katika shule ya Msingi Pangani mkoani humo.

Tatu bint Said aliolewa na mume wake wa kwanza Khatibu Akida akiwa na umri wa miaka 11, wakafanikiwa kupata mtoto mmoja.Mume huyo alikuwa mbofya Kinanda maarufu ambaye ndiye aliyemshawishi kuingia katika tasnia hiyo ya muziki wa taarabu.

Tatu alikubali ushauri wa mumewe akaanza kufanya mazoezi makali ya kutunga na kuimba nyimbo za taarabu.Baada ya kuonekana kuwa ana uwezo mkubwa, mumewe Khatibu alimshawsihi kujiunga katika kundi la Kijamvi taarabu lililokuwepo mjini Pangani mkoani Tanga.

Hakudumu kwa kipindi kirefu na kikundi hicho akalazimika kuhamia mjini Tanga kumfuata mumewe Khatibu Akida.Alipofika huko alijiunga katika kundi la Al Watan, lakini kwa sababu ambazo hazikuelezwa, Tatu akiwa katika kundi hilo hakupewa nafasi ya kuimba mbele ya kadamnasi.

Kitendo hicho kilisababisha yeye na mumewe baada ya muda mfupi wakahamia katika kundi la lililokuwa likimilikiwa na mzee Kiroboto la Young Novelty mwaka 1961.Msomaji wa makala hii itakumbukwa miaka ya 1960 hadi 1980 Sinema za Kihindi zilichukuwa nafasi kubwa katika kumbi nyingi hapa nchini.

Katika sinema hizo watu walimshuhudia mwimbaji wa nyimbo za Kihindi aliyekuwa akiitwa Shakila.Hivyo wapenzi na mashabiki wa miondoko ya taarabu wa wakati huo walilinganisha na sauti ya Tatu Saidi kuwa haitofautiani sana na ya Shakila, wakampachika jina hilo

Shakila bint Said alikuja kuwa miongoni mwa waanzilishi wa kundi la taarabu la Black Star, ambako alionesha cheche zake baada ya kuachia tungo yake ya “Duniani nakupenda wewe”.

Aidha alifanikiwa kuimba wimbo mwingine unaoitwa “Jogoo acha makuu”, ukiwa ni utunzi wa Awadhi Seif, walishirikiana kuimba na mwimbaji Hamadi Mrisho.Yaelezwa kuwa wimbo huo uliwavutia mamia ya mashabiki waliokuwa wakijazana kwenye kumbi ambazo Black Star ilikuwa ikitoa burudani.

Hiyo ilielezwa kuwa ilitokana na uwezo mkubwa wa Bi. Shakila kuweza kucheza na sauti katika nyimbo za taarabu.Ndani ya kundi hilo ambalo lililokuwa likimilikiwa na Soud Saidi, Shakila aliweza kufanya makubwa katika uimbaji wake uliokuwa ukiwavutia watu wengi.

Ndani ya mwaka mmoja alifanikiwa kuimba nyimbo kali kama vile Kitumburi, “Macho yanacheka” na “Kifo cha mahaba”.Black Star walimpa majukumu mazito Bi Shakila, karibia nyimbo zote za kundi hilo, sauti yake ilisikika na kuweza kuipandisha chati bendi hiyo.

Alidumu ndani ya Black Star kwa miaka kumi, tangu mwaka 1961 mpaka 1971, baadaye alihama na kwenda kutafuta maisha bora sehemu nyingine.

“…nikiwa Binti wa umri wa miaka 18, niliondoka Black Star baada ya kuitumika kwa kipindi kifupi, nikaenda kujiunga katika kundi la Lucky Stars lililokuwa mjini Tanga…” alisema Bi. Shakila.

Shakila alifanya ‘kufuru’ akiwa katika kundi hilo kwa kuimba nyimbo nyingi zenye maudhui maridhawa kwa jamii.Nyimbo hizo ni pamoja na Mapenzi ni kama donda, Mapenzi yamepungua, Bunduki bila risasi, ’Viva Frelimo, Viva Samora, Kitanda kuwekwa pembeni na nyingine nyingi.

"Nilianza muziki mwaka 1960 kabla ya nchi yetu haijapata Uhuru na nimekuwa huko kwa miaka mingi. Wakati nikianza muziki, nilimkuta marehemu Saada Binti Saad na Fatuma Binti Baraka ‘Bi Kidude’ yeye akiwa tayari amejiunga na ngoma za Unyago.

Alikuwa bibi yangu na mtu wa karibu sana na mimi wakati huo nilikuwa na miaka sita...” Shakila aliwahi kutamka.Akiyaelezea maisha yake ya ndoa, alisema kuwa aliolewa na mume wa kwanza akiwa na umri wa miaka 11.

Katika ndoa yao waliweza kupata mtoto mmoja lakini ndoa hiyo ilidumu kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja wakahitilafiana hadi kuachana.
Shakila aliyekuwa na haiba yenye mvuto, aliolewa tena na mume mwingine aliyepata naye watoto watano.

Kwa bahati mbaya mnamo mwaka 1975 mume huyo alifariki baada ya miaka 18 ya ndoa yao. Akakaa Eda kwa mujibu wa taratibu ya dini ya Kiislamu.

“…baadaye niliolewa na mume mwingine huyo nilizaa naye watoto watano baadaye tukaachana. Nikaolewa tena kwa mara ya nne nikaza watoto wawili. Nilipokuwa na mimba ya mtoto wangu wa mwisho Shani mwaka 1993, mume wangu akaniacha…” alisema Shakila.

Rais wa awamu ya kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikuwa ni mmoja wa viongozi waliokuwa wakivutiwa na uimbaji wa Tatu bint Said ‘Shakila’, hata marehemu mzee Rashid Mfaume Kawawa.

Baadhi ya mikutano ya hadhara Bi. Shakila alikuwa akialikwa kutumbuiza kabla ya Mwalimu Nyerere ama Kawawa kuhutubia.

Kwa Weledi wake mkubwa ulipelekea mwaka 1987 kukubali ushawishi wa aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo Dk. Salim Ahmed Salim, pamoja na makada wa Chama Cha Mapinduzi Moses Nnauye na Abdurahman Kinana, kumuondoa Tanga kwenda kuwa mkufunzi wa kikundi cha taarabu cha Jeshi la Kujenga Taifa Makao Makuu jijini Dar es Salaam.

Bi Shakila akiwa na kundi la hilo la JKT kati ya miaka 1980 na 1990, aliendeleza wigo wa umaarufu ndani ya nchi hata Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.

Akiwa na kundi hilo alifyatua wimbo wa ‘Kitanda kukaa Pembeni’ ambao alikiri kuwa ulikuwa ukimkuna sana hususan baada ya kukosa majibu akaonekana kuwazidi uwezo wa utunzi wasanii wenzake.

Shakila aliwahi kutamka kuwa aliimba kibao hicho mwenyewe kikiwa na nia ya kuuliza swali hilo ili apatiwe jibu toka kwa wasanii wenzake, hasusan wale wa muziki wa taarab.Alisema kuwa tangu aimbe kibao hicho ni miaka 25 imekwishapita, lakini hakuna msanii yeyote wa taarab au mwimbaji wa muziki mwingine aliyethubutu kumjibu swali lake hilo.

“Niliimba kibao hicho nikiwa na nia ya kujibiwa swali langu, lakini cha kushangaza hadi leo hii, bado swali langu hilo halijajibiwa na mimi sijakata tamaa bado nasubiri jibu litakaloniridhisha…” alisema Bi. Shakila aliyeacha wajukuu 20.

Wakati wa uhai wake Tatu Said Khamis maarufu kwa jina la Bi. Shakila, alikuwa mmoja wa waasisi wa muziki wa taarabu nchini na Mwenyekiti wa Chama cha Waimbaji wa taarabu Tanzania.

Akielezea taarabu ya wakati huu alisema “….mwanzoni taarab haikuimbwa bali ilighaniwa, na ndiyo maana waimbaji wake walikuwa wanakaa `kitako` na kutulizana huku wakifikisha ujumbe.

Miaka inavyokwenda na ndivyo taarab inavyozidi kupoteza mwelekeo na kuichafua jamii badala ya kuijenga kama ilivyoasisiwa kufikisha ujumbe na kukuza lugha ya Kiswahili…”

“Tumebaki na Taarab inayokwenda kama Kuku aliyokatwa shingo, taarab isiyotazamwa na watoto na wazazi wao…” alilalama Shakila.Pamoja na sifa zote hizo alitamka kuwa hakufaidika na jasho lake na hata kama alifaidi siyo faida inayolingana na jasho lake alilotumia.

Shakila aliwahi kutamka kuwa yeye ni miongoni mwa Wasanii ambao hawakunufaika kwa jasho lao kama ilivyo kwa wasanii wengi wa zamani kutokana na mfumo mbovu.

Sauti yake nyororo alikuwa hatofautiani sana na ya Bi. Aisha Abdul maarufu ‘Malika’ anayeishi hivi sasa nchini Marekani hata Bi. Mwanahela anayeishi mkoani Tanga.

Bi. Shakila alistaafu muziki akiwa katika bendi ya Jeshi la Kujenga Taifa mwaka 2009.Licha ya kustaafu kwake, alikuwa aikiitwa kwenda kuimba na kundi lake hilo la JKT ambapo alikuwa akilipwa ujira wa sh. 3,000 wakati akifanya onesho moja.

Tatu Said ‘Shakila’ alikuwa akilalamika kuwa baada ya kustaafu, hakuwa na pesa za kujikimu kimaisha kwa kuwa kiwango alichokuwa akipokea kama kiinua mgogo cha sh. 80,000 kwa mwezi toka NSSF, kilikuwa hakimtoshi kabisa. Alilazimika kuishi kwa kupika na kuuza visheti na vitumbua.

Bi. Shakila alikuwa mbioni kumalizia albamu yake ya ‘Mama na Mwana’ ambayo ingelikuwa na nyimbo nane na kati ya hizo, tano zilikuwa zimekamilika ukiwamo wa ‘Mama na Mwana’

Aidha katika mikakati ya kuimba tena wimbo wa “Kifo cha Mahaba” alikuwa amedhamiria kumshirikisha mwanamuziki wa kizazi kipya Naseeb Abdull ‘Diamond Platnumz’.Katika maisha yake Bi. Shakila alibahatika kupata watoto 15, 12 kati yao bado wapo hai.

Binti yake anayejulikana kwa jina la Mape, ndiye pekee aliyetajwa kwa aliyerithi mikoba ya taarabu ya mama yake.Shani ambaye ni binti yake wa mwisho, alionesha ujasiri mkubwa katika kipindi kigumu cha msimba wa mama yake kwa kuweza kueleza chanzo cha kifo cha mama yake mbele ya vyombo vya habari.

Alisema kuwa mama yake hakuwa anaumwa ila baada ya kumaliza kuswali sala ya Magharibi, alianguka ghafla na alipofikishwa hospitali alielezwa kuwa tayari amekwisha fariki.Bi. Shakila Saidi alizikwa Agosti 20, 2016 katika makaburi ya Uwanja wa Ninja huko Mbagala Charambe jijini Dar es Salaam. 

Bi. Shakila, hatutakusahau kamwe, mungu uipumzishe roho yako pahala peponi, Amina.


Imeandaliwa na Moshy Kiyungi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...