Na Moshy Kiyungi,

Mashairi ya nguli Patrick Balisidya aliyokuwa akitunga na kuimba katika nyimbo zake, kamwe hayatachuja kufuatia ujumbe uliomo.

Alikuwa kiongozi wa bendi ya Afro70, ambapo alijizoea umaarufu mkubwa humu nchini hata nje ya mipaka yetu.

Hata hivyo historia ya muziki haiwezi kumuweka pembeni mwanamuziki huyu Balisidya, aliyezaliwa katika kijiji cha Mvumi mkoani Dodoma Aprili 18, 1946.

Alikuwa ni wa kabila la Wagogo, ambalo limetoa wanamuziki wengi maarufu akiwemo marehemu Dk. Hukwe Zowose.Mama yake alikuwa mpiga Kinanda Kanisani, kwa mantiki hiyo vikichanganywa na asili ya kabila lake, pasipo shaka muziki ulikuwa ndani ya damu yake.

Patrick Balisidya wakati akiwa mwanafunzi katika sekondari ya Dodoma, alipewa nafasi ya kuwa kiongozi wa bendi ya shuleni, baada ya kugundulika kuwa na kipaji cha muziki.

Baada ya kumaliza elimu yake, alikwenda kujiunga na Chuo cha Ufundi jijini Dar es Salaam, kisha alkapata ajira ya muda.Mwaka 1967 Balisidya alichukuliwa kwenda kupiga muziki katika bendi ya Dar es Salaam Jazz B. Nyakati hizo bendi za muziki hata klabu za mpira wa miguu nyingi zilikuwa A na B.

Baada ya kipindi kupita, mwaka 1970 Patrick alianzisha bendi yake mwenyewe aliyoipa majina ya Afro70.Bendi hiyo ilianza kupiga muziki maridadi na kuonekana kama tishio kwa bendi zingine kubwa zilizokuwapo wakati huo.

Bendi hiyo alikuwa ikitumia mtindo wa Afrosa, uliobuniwa na nguli huyo.
Balisidya alikuwa mbunifu katika muziki, kwa muda mrefu alikwepa sana kuingia katika wimbi la kufuata mapigo ya Kikongo.Mwaka 1979, alipata fulsa ya kwenda nchini Sweden, huko alishirikiana na kikundi cha Archimedes, wakatoa album nzuri sana iliyoitwa ‘Bado Kidogo’.

Kuna wakati Patrick alijiunga na bendi ya Orchestra Safari Sound, (Masantula), aliweza kupiga Piano katika wimbo maarufu wa ‘Unambie siri’.
Balisidya alikuwa na talanta nyingi za ziada katika muziki. Licha ya kutunga na kuimba, pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kubofya kinanda.
Baadhi ya nyimbo walizotunga na kupiga wakiwa na bendi ya Afro70, ni pamoja na Harusi, Dirishani, Weekend, Tausi, Pesa, Nakupenda kama Lulu, Ni mashaka na Mahangaiko.

Patrick Balisidya na bendi yake ya Afro70, iliwahi kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika maonesho ya mtu mweusi yaliyofanyika katika jiji la Lagos, nchini Nigeria yaliyojulikana kama (FESTAC Festival 1977).
Kabla ya kuondoka wakati huo serikali ilikuwa imemtaarifu kuwa ndiye atakuwa mwakilishi.

Kwa bahati mbaya pamoja na kuteuliwa huko, vyombo vyake vyote vya muziki vilikuwa vimeharibika katika ajali ya gari.Kwa bahati njema Serikali ilikuwa tayari imenunua vyombo vipya kwa ajili ya bendi yake ya Wizara ya Utamaduni wakati huo.Balisidya na bendi yake wakaenda Lagos kwenye maonesho hayo wakiwa na vyombo muziki vipya.

Mara nyingi alikuwa akitamka kuwa aliaahidiwa kuwa vyombo hivyo vitakuwa vyake baada ya maonesho hayo ya Nigeria.Lakini waliporejea nchini, kiongozi mwingine wa serikali aliamumuru vyombo hivyo kurudisha serikalini.Taarifa hiyo haikuwa njema kwa Balisidya, aliyekuwa na imani kubwa kwamba atakabidhiwa yeye.

Alitumia muda mwingi kujaribu kudai haki aliyokuwa akidhani yake, lakini uongozi wa serikali wakati huo ukawa unamkwepa.Hata hivyo vyombo vilitumika kuanzisha bendi ya Asilia Jazz iliyokuwa ikimilikiwa na Wizara ya Utamaduni na Vijana.Kitendo hicho cha kunyang’anywa vyombo hivyo, Balisidya na wanamuziki wenzake wakawa hawana la kufanya, na ndipo ikiwa mwazo wa kifo cha bendi hiyo ya Afro70.Patrick Balisidya kwa mapenzi yake mungu, alifariki Agosti 07, 2004 na kuzikwa Agosti 12, 2004 katika makaburi ya Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam.

Daima atakukumbukwa Patrick Balisidya, Mungu ailaze roho yako pahala pema peponi, Amina.


Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba:

0713331200, 0736331200, 0767331200 na 0784331200.

PICHA ZA PATRICK BALISIDYA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...