Said Mwishehe, Globu ya jamii
MBUNGE wa Kibamba katika Jiji la Dar es Salaam John Mnyika (CHADEMA) ametakiwa kufanya ziara ndani ya jimbo lake ili kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofanywa na Serikali ikiwemo ya miradi ya maji.
Mnyika ameelezwa hayo leo Bungeni Mjini Dodoma baada ya Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso kuelezea hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali kutatua changamoto ya uhaba wa maji.
Wakati Aweso anazungumzia miradi ya maji alizungumzia jimbo la Kibamba na miradi ya maji ambayo imefanyika lakini baada ya maelezo hayo Mnyika alisimama bungeni na kumtaka aombe radhi kwa madai Naibu Waziri anasema uongo bungeni.
Mnyika alisema "Nimemsikia Naibu Waziri wa Maji anavyoelezea miradi ya maji na ametaja jimbo la Kibamba lakini ukweli hayo anayoyasema hayana ukweli wowote na ni vema akaomba radhi kwa kusema uongo bungeni."
Baada ya kauli hiyo ya Mnyika, Naibu Waziri wa Maji alitakiwa kutoa ufafanuzi na hapo ndipo alipoamua kumpa makavu mbunge huyo kwa kuelezea hatua ambazo zimefanywa na Serikali katika kutatua changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Kibamba jijini Dar es Salaam.
"Naomba nitumie nafasi hii kumshauri ndugu yangu Mnyika, tatizo lake hafanyi ziara katika jimbo lake na hivyo hata miradi ya maendeleo inavyotekelezwa na Serikali haoni.Ukitoka Bungeni nenda kafanye ziara ya kutembelea jimbo.
"Kote ambako nimetaja uwepo wa miradi ya maji iliyokamilika utaikuta.Wizara ya Maji kwa niaba ya Serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana,"amesema Aweso.
Naibu Waziri huyo pia ametumia nafasi hiyo kueleza wazi Serikali imedhamiria kutatua changamoto ya uhaba wa maji nchini na ndio maana imeanzisha Wakala wa Maji Vijijini ambayo itakwenda kumaliza tatizo lililoko sasa na kwamba Wizara ya Maji iko makini.
"Kupitia Wakala wa Maji Vijijini tunakwenda kumaliza tatizo la uhaba wa maji, na hata wale wakandarasi uchwara katika maji nao wanakwenda kuondoka kwa namna ambavyo Wizara ya Maji tumejipanga,"amesema Aweso.
MBUNGE wa Kibamba katika Jiji la Dar es Salaam John Mnyika (CHADEMA) akifafanua jambo Bungeni leo.Picha hisani ya Edwin Njwahuzi -Mwananchi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...