Na. Paschal Dotto-MAELEZO
Rais Dkt John Pombe Magufuli amewahakikishia wananchi wa Nanyamba, Tandahimba, na
Newala Mkoani Mtwara kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya uhakika ili
kuunganisha Kanda ya Kusini Kiuchumi na wananchi wa Mkoa huo kuendelea kufanya kazi kwa
juhudi ili kuweza kujiletea maendeleo yao.
Akizungumza katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo, Rais Magufuli amesema Serikali itaanza
ujenzi wa barabara ya Mtwara-Tandahimba-Nanyamba yenye urefu wa kilometa 50
itakayogharimu kiasi cha Tsh.bilioni 86 na kumwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Isack Kamwelwe kutangaza zabuni ya ujenzi wa kilometa zingine na kufikia
kilometa 100 na hivyo kuunganisha kwa urahisi nyanda za kiuchumi katika mikoa ya kusini.
“Barabara hii itakuwa ni kiunganishi cha uchumi mikoa ya kusini, hatuwezi kushindwa kujenga
kilometa 100, lengo letu kuu ni kuiunganisha Bandari yetu ya Mtwara na mizigo inayotoa
Malawi,” alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema kuwa katika kuwainua wakulima wa Mkoa wa Mtwara, ambapo
Serikali imetekeleza ununuzi wa korosho kutoka kwa wananchi wenye korosho zaidi ya kilo
1500, na Tsh Bilioni 50 tayari zimetengwa kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao, na kwa upande
wa wakulima wa korosho wenye kilo chini ya 1500 wamelipwa kiasi cha Tsh Bilioni 578.
Rais Magufuli amewahiza wafanyabiashara walanguzi wa zao la korosho ‘Kagomba’ kuacha
kuwadhulumu wakulima wadogo kwa kuwapa bei ambayo hailidhishi huku wakijua wametumia
gharama kubwa katika kuendeleza zao hilo, na kusema serikali ya Awamu ya tano haitarudi
nyuma kuwatetea wakulima hao.
“Utakuta mtu amelima korosho zake, amenunua madawa, ametumia gharama kuzivuna
unakuja kumpa bei ya 1500, kwa Serikali ya Awamu ya Tano hili halikubaliki”, alisema Rais
Magufuli.
Akiongelea miradi mingine inayotekelezwa serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni pamoja na
upanuzi wa bandari ya Mtwara, , upanuzi wa uwanja wa Ndege na ukarabari wa mradi wa maji
wa makonde ambao utagharimu kiasi cha Tsh.bilioni 160 zikiwa ni fedha za mikopo kutoka
Serikali ya India unaowezesha ujenzi wa miradi ya maji katika miji 28 nchini.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...