Serikali imeonya kuwa haitakuwa na msalie mtume
na mtu,chama cha siasa ama kikundi chochote kitakachojihusisha na rushwa
kabla,wakati na baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu 2019 pamoja na Uchaguzi mkuu wa 2020.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi wakati
akifungua mkutano wa kujadili namna ya kudhibiti rushwa katika uchaguzi wa
serikali za mitaa 2019 jijini Dar es Salaam, na kuongeza kuwa Serikali ya awamu
ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli inataka wananchi watambue kuwa
serikali yao imedhamiria kupambana na rushwa katika nyakati zake zote na sura zake
zote.
“Sote
tunafahamu mwaka 2019 tutakuwa na Uchaguzi katika ngazi za Serikali za
Mitaa hivyo basi,chaguzi hizi zinapaswa kuendeshwa na kusimamiwa kwa
uadilifu na umakini mkubwa kwa
kuzingatia sheria,kanuni na taratibu ili haki,usawa,uhuru na demokrasia
viweze
kustawi,kuendelezwa na kudumishwa hivyo Takukuru kamwe isiwe na Msalie
Mtume kwa
yeyote atakayejihusisha na masuala ya rushwa”
Profesa Palamagamba John Kabudi ameongeza kuwa
rushwa katika uchaguzi ni zaidi ya udanganyifu wa hesabu za kura,kwakuwa una
madhara kadha wa kadha ikiwemo viongozi kukosa uwajibikaji,kukosa viongozi
waadilifu,kukosa viongozi wazalendo,uwepo wa vitendo vya uvunjifu wa Amani kutokana
na migogoro ya mara kwa mara ya kisiasa,uchumi wa Taifa kudidimia kwa kukosa
mipango ya maendeleo na viongozi kufanya maamuzi ya kisera yenye maslahi kwa
wachache.
Aidha,amewapongeza TAKUKURU kwa kuandaa Warsha hiyo
katika wakati muafaka na kusisitiza,pamoja na sheria na kanuni zilizopo
bado kuna wajibu mkubwa wa kuhakikisha jamii inashirikishwa na kuelimishwa
kuhusu madhara ya rushwa katika Uchaguzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya
kuzuia na kupambana na rushwa nchini TAKUKURU Kamishna wa Polisi Diwani
Athumani amesema rushwa katika Uchaguzi ni hatari na inaweza kuleta madhara kwa
Taifa kwani viongozi wala rushwa au watoa rushwa hawataweza kuisimamia nchi kwa
misingi ya haki,usawa,uwazi,uwajibikaji na uzalendo na vilevile wananchi
wapokea au watoa rushwa hawawezi kuhoji masuala mbalimbali kwa viongozi wao.
Amewataka
wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha na kutoa taarifa bila woga kwa
wale wote watakaojihusiha na masuala ya utoaji ama upokeaji
rushwa ili sheria ziweze kufuata mkondo wake na baadae kuwa na Taifa
lenye
usawa katika nyanja zote.
Warsha hiyo ya wadau kujadili namna ya kudhibiti
rushwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa imehudhuriwa na wadau mbalimbali
wakiwemo viongozi wadini,vyama vya siasa,vyama vya kiraia na vyombo vya ulinzi
na usalama.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...