Na Moshy Kiyungi
Sifa kubwa aliyonayo Aslay ni uwezo wa kutunga, kuimba na kurekodi nyingi kwa kipindi kifupi.
Ni msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka nchini Tanzania maarufu kama ‘Dogo Aslay’, ambaye tungo za nyimbo zale zimekuwa zikiwakuna wapenzi wa muziki wa huo, ndani na nje ya nchi.
Nyimbo za kijana huyu zimejikita zaidi katika mapenzi, ambazo kundi kubwa la wasikilizaji hupendelea sana kuzisikiliza.
Majina yake kamili anaitwa Isihaka Nassoro, alizaliwa Mei 06, 1995, akapata elimu ya msingi katika shule ya Yussuf Makamba kati ya mwaka 2003 na 2009, kabla ya kuingia sekondari ya Tandika mwaka 2010 alikosoma hadi kidato cha nne.
Pindi umuonapo Dogo Aslay, ukalinganisha na mashairi anayotunga na kuimba nyimbo, utabaini kwamba haziendani na umri wake, lakini kupitia kipaji chake, anafanya vitu vikubwa kama hivyo.
Alianza kufahamika kuanzia mwaka 2011 baada ya kuachia ngoma yake ya Nakusemea, aliyoitoa akiwa chini ya msimamizi wake Mkubwa Fella.
Baadae akatoa nyimbo kadhaa kabla ya kuundwa rasmi bendi ya vijana ya Yamoto.
Bendi hiyo ya Yamoto ilidumu tangu 2013 hadi 2017 ilipovunjika kwa sababu mbalimbali.
Kuanzia 2017, Aslay akawa msanii wa kujitegemea bila bendi wala usimamizi wa Mkubwa Fella.
Amebaki akiwa na meneja wake wa zamani Chambuso.
Aslay ametoa nyimbo nyingi mfululizo hali ambayo imewachanganya baadhi ya watu hata wasanii wenzake.
Alielezea kwanini aliamua kufanya hivyo, sababu kubwa ni kwamba hana nyimbo nyingi alizofanya akiwa msanii wa kujitegemea, zaidi ya zile alizokuwa na bendi ya Yamoto.
Ili asiimbe za Yamoto akiwa kwenye matamasha, kaamua kutoa nyimbo nyingi.
Baadhi ya nyimbo ni pamoja na Angekuona, Usiitie Doa akimshirikisha mama Khadija Kopa, Muhudumu, Baby, Likizo, Pusha Natamba na Huna.
Awali ilitazamika kama Mkubwa Fella ndiye hasa mmiliki wa muziki wa kizazi kipya, lakini kupitia Aslay, Chambuso anasema si lazima yeye ndiye awe meneja bora wa muziki huo.
Aslay alimemtaja kaka yake Idd kuwa ndiye aliyegundua kipaji chake na kumkutanisha na mdau wa muziki kutoka TMK, Said Fella ‘Mkubwa’, baada ya kumuona akipenda kuimbaimba kila alipokaa.
kufanya vizuri zaidi katika muziki wa dansi la kizazi kipya akiwa na kundi la Yamoto Band.
Yamoto Band.
Ndani ya kituo cha Mkubwa na Wanawe, Aslay alipokelewa na kunolewa kikamilifu na baadhi ya wakali aliowakuta, wakiwamo Yusuph Chambusso na Fella mwenyewe.
Mwaka 2011 akishiriki onesho la nchi za Majahazi maarufu kama (ZIFF), aliweza kulitendea haki ipasavyo onedho hilo kwa kuimba kibao ‘Zuwena’ ambacho ni cha marehemu Marijani Rajabu ‘Jabali la Muziki’.
Mwaka huohuo, 2011 akachomoka na ngoma yake ya kwanza, iliyotokea kutikisa vilivyo na kuteka nafsi za wengi, hususan watoto na wanawake, inayokwenda kwa jina la ‘Nakusemea’.
Mwaka uliofuata, 2012 Aslay alirekodi kibao ‘Umbea’ alichomshirikisha Chegge Chigunda kabla ya kuachia kete nyingine tena iliyojulikana ‘Bado Mdogo’.
Baada ya kushuka na kupanda huko, ndipo mwishoni mwa mwaka 2013, lilipoundwa kundi la Yamoto Band kwa kushirikisha pia vijana wengine watatu ambao ni Beka, Maromboso na Enock Bella.
“Changamoto kubwa tunayoipata ndani ya Yamoto Band kupendwa na kuchukiwa, kwasababu tulitokea kukubalika ghafla basi wapo waliotupenda na wengine kutuonea kijicho,” alisema Aslay katika mahojiano maalumu.
Malengo ya baadae ya Dogo Aslay ambaye hakutegemea kama atatoka kimuziki, ni kumiliki kituo chake mwenyewe cha kuibua na kukuza vipaji vya wasanii, kama ilivyo kwa bosi wake, Fella.
Aidha alieleza siri ya kuibuka kuwa mwimbaji, Aslay anayevutiwa na Banana Zorro katika muziki, alisema kwamba alipitia madrasa ya Aswabirina, Temeke, jijini Dar es Salaam.
Huko alikufundishwa jinsi ya kughani nyimbo za Kaswida, na kumfanya ajiamini mbele ya kadamnasi pasipo hofu yeyote.
Aslay alitamka kuwa kukosa ushirikiano kwa baadhi ya wasanii wa muziki na hali ya kuibuka kwa bifu, ni kati ya mambo yanayo mkera nyota huyo mpya asiyependa majivuno.
Safu hii inakutakia kila la heri ili uweze kufikia malengo uliyojipangia ili mradi ‘usilewe sifa’ zitakuponza.
Mwandishi wa makala hii anaptikana kwa namba: 0784331200, 0767331200, 0736331200 na 0713331200.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...