Na  Moshy Kiyungi
Licha ya kufariki miaka 38 iliyopita, muziki wa hayati Robert Nesta Marley ‘Bob Marley’ bado unapendwa na idadi kubwa wapenzi mashabiki wa muziki wa reggae duniani.

Bob Marley alionesha ujasiri mkubwa wa kugoma kwenda kupigana vita nchini Vietnam, baada ya akijiuliza ni kwanini aende kupigana vita au kushiriki katika suala la mauaji ya watu wasio na makosa, akaamua kurudi nchini kwake Jamaica.

Historia ya gwiji hilo unaonesha kuwa alizaliwa Februari 6, 1945 katika kijiji cha Nine Miles kwenye Parishi ya mtakatifu Ann, nchini Jamaica.

Baba yake Norval Sinclair Marley, alikuwa mzungu na mama yake Cedelia Booker alikuwa Mjamaica mweusi ambaye alikuwa mwimbaji wa kwaya Kanisani.

Kwake Bob Marley ilikuwa ni majonzi na huzuni baada ya kuachwa chini ya mzazi mmoja (mama yake), akiwa na umri wa miaka kumi, pale alipofiwa na baba yake Norval Sinclair, Sinclair kufariki dunia mwaka 1995 akiwa safarini, wakati huo alikiwa na umri wa miaka 60.

Marley alimalizia udogo wake akiwa huko shamba kwenye mazingira ya wakulima wa ndizi na minazi, akinywa madafu. Huko alikuwa akikamua ng’ombe maziwa na mbuzi, pia alikuwa akienda kuogelea kwenye vijito na Bahari.

Mama yake Cedella Booker hakutaka mwanaye aishie kutanga tanga na kuzurura, akihofu kuwa mwanaye Bob angeliharibika kama ilivyo kwa watoto wa familia zingine zenye tabaka la chini.

Alitamani sana mwanaye ajifunze kazi yoyote ya ufundi ambayo ingeweza ingeweza kumudu maisha yake hapo baadaye.
Booker akapata wazo ya kuhamishia makazi yao na kwenda mji wa Kingstone nchini Jamaica.

 Wakiwa Kingstone, Bob akaanza kujifunza ufundi wa kuchomelea vyuma (Welding). Katika ufundi huo alikuwa akishirikiana na kijana mwenzake Desmond Dekker.

Bob na Desmond wakawa vibarua waliokuwa wakilipwa ujira kwa siku, huku wakiendelea na shughuli za uchomeleaji. Vijana hao wakaanza kujifundisha kutunga na kuimba nyimbo.

Shughuli hiyo waliifanya mara nyingi wakiwa kazini hapo walionekana kutingwa na kazi, lakini waliendelea kuimba huku wakichapa kazi.

Siku moja kipande cha chuma chenye moto kiliingia jichoni kwa Desmond. Hapo mambo ndipo yalianza kubadilika, Desmond aliamua kurudi nyumbani kwao kwa kuwa alikuwa na ujira wa kutwa. Wakati akiuguza jicho lake akaamua kuanza kile kilichokuwa kwenye damu yake (muziki).

Desmond Dekker hakuchuka kipindi kirefu, akatoa kibao chake kilichoitwa ‘Honour Thy Father and Thy Mother’, akimaanisha ‘waheshimu Baba na Mama’. Wimbo huu ulipendwa sana na katika mafanikio hayo ilikuwa ni kijana huyo kusaidiwa na studio za Beverleys.

Mambo yalipo mnyookea katika muziki, Desmond hakufanya uchoyo, alimshawishi Bob Marley kujaribu kuupa kipaumbele muziki.
Bob alikubaliana na ushauri wa rafiki yake huyo, wote wakaenda kwenye studio za Beverley’s. Huko Bob akakutana na mwanamuziki maarufu Jimmy Cliff.

Cliff mbali ya umaarufu aliokuwanao, pia alikuwa na moyo wa huruma wa kupenda kusaidia watu. Alimsaidia Bobo Marley kwa vifaa na ushauri mpaka hapo Bob alipofanikiwa kuipua wa ‘ngoma’ yake ya kwanza ya ‘Judge Not’.
Baadae Bob aliishi maisha ya Gheto huko Trench Town kwenye nyumba ya baba wa Bonny Livingstone, ikiwa ni muda mfupi tu tangu alipounda urafiki na Bonny.

Siku moja alionekana mwanamuziki Peter Tosh akipitapita mitaani akiwa na Gitaa lake. Alikuwa akipiga na kuimba, akicheka, akitania, akitukana na kuchokoza na ubishi kama jadi yake.

Ndipo walipojenga urafiki wa watu hao watatu Bonny Livingstone, Bob Marley na Peter Tosh. Wakaunganisha nguvu na kuanzisha kundi zima la The Wailers ambayo mwanzoni waliita The Wailing Wailers.

Vijana hao Bob, Bonny na Tosh wakatokea kuwa tishio waliyapanda majukwaa ya Kingstone wakiimba nyimbo zenye mtazamo wa Kibiblia pamoja na nyimbo za mapenzi kama vile wimbo wa ‘Do It Twice’. Aidha waliimba nyimbo za kuchangamsha na kuliwaza vijana wa Gheto.

Kujulikana kwa vijana hawa kuliongezeka zaidi hasa pale walipo chukuliwa na ‘Studio one’ ya jamaa aliyeitwa Coxsone Dodd. Huyo alikuwa maarufu sana hasa katika utengenezaji wa Santuri,lakini mambo hayakuwa mazuri kwa ‘wapiganaji’ hao kuhusiana na kipato.

Mnamo mwaka 1966, Wailers waliipua kibao kama vile Put It On, Rude Boy, I’m still waiting na Rule them Rudie. Vibao hivyo vilimwingizia kipato kikubwa Coxsone Dodd. Ilipofika wakati wa sikukuu ya Krismasi, vijana hao walidai haki yao ili wakafurahi na wenzi wao Trench Town.

Dodd akawapatia Paund 60 Bob hakuweza kuvumilia akazichukua pesa hizo akamtupia usoni Dodd. Bob akaamua kuanza safari ya kumfuata mama yake huko Marekani huko akaendelea kutunga nyimbo kama vile wimbo uitwao ‘Bend Down Low’.

Akiwa huko Marekani Bob akapata kibarua katika kiwanda cha kutengeneza magari aina ya Cryster kilichopo mjini Delaware,lakini huko Amerika hakukaa sana aliamua kuondoka nchini humo baada ya kupata barua .

Barua aliyoipata Bob ilimtaka akapigane vita huko Vietnam, wazo hilo Bob hakuafikiana nalo huku akijiuliza ni kwa nini aende kupigana vita au kushiriki katika suala la mauaji ya watu wasio na makosa, akaamua kurudi nchini kwake Jamaica.

Ulimwengu wa kibepari bado uliendelea kumtupa huku na kule, aligundua kuwa kila mahali wanataka kumtumia au kukitumia kipaji chake cha muziki ili wajitajirishe wao au kumtumia kama kibarua mchomeaji kisha kumlipa ujira mdogo ama kutumia ujana wake katika vita huko Vietnam kwa manufaa ya mabeberu.

Bob Marley alibaini kwamba watu wale walijifanya ni marafiki kumbe walitaka kumtumia kama ilivyokuwa kwa Coxsone Dodd ambaye alijifanya rafiki kipenzi.
Fikra hizo zilionyesha hali halisi jinsi Bob alivyo itameibua jamii ya Kibepari. Ndipo alipoamua kuifikishia ujumbe huu Dunia nzima kupitia kibao chake cha ‘Who The Cape Fit’katika Santuri ya Rastaman Vibration.

Bob Marley alimuoa kimwana Rita Anderson Februari 10, 1966 na kwenda kuishi kwa muda na mama yake huko Wilmington, Delaware nchini Marekani. Huko wakaibuka na imani kali ya Kirastafari na kuja na mtindo wa kufuga nywele uitwao "Dreadlocks".

Rita aliyezaliwa Julai 25, 1946, huko Santiago de Cuba, jina lake halisi ni Alpharita Constantia Anderson. Katika maisha ya ndoa yao walifanikiwa kupata watoto watatu.

Hata hivyo Bob Marley aliwahi kukiri kuwa alikuwa na watoto wengine watatu kutoka katika mahusiano yake mengine.
Bob Marley na kundi lake la The wailers, baadaye walitoa vibao vingi vilivyoitikisa Dunia. Kati ya vibao hivyo ni pamoja na “Africa unit”, “Zimbabwe”, “Could you loved?”, “Iron lion zion”, “Is this love”, “Buffalo soldier” na vingine vingi..

Vyombo vya habari vikiwemo Redio, Matangazo, Magazeti ya Kibepari hayakutaka kabisa kukubali mafanikio ya The Wailers kwamba yalitokana na bidii za pamoja za wahusika wote.

Vyote hivyo viliamini kwamba kila kitu kilifanyika na Bob Marley na hao wengine walifanywa kama vijana wake tu kitendo ambacho kiliwaudhi Bunny na Tosh, hizo zilikuwa hisia ,mbinu za mabepari ili kuhakikisha  wanawatenganisha.

Peter Tosh aliiacha bendi ya The Wailers mnamo mwaka 1974 baada yeye na Livingstone kukataa kufanya ziara hiyo.
Baada ya Peter kuondoka Bob alianza kutafuta wanamuziki wengine, akawapata Al Andason Rasta, Junior Marvin ‘Rasta bitoz’ na Tyrone Downie kijana ambaye kwa muda mrefu alikuwa anawahusudu sana The Wailers.

 wakajiunga pia wale I Threes, wanawake weusi watatu waliokuwa na sauti nzuri Rita Marley, Juddy Mowatt na Marcia Griffiths walimsaidia Marley katika uimbaji. Hapo ndipo hapo Bob Marley akabadilisha jina la bendi na kuwa ‘Bob Marley & The Wailers’ akiwa yeye mwenyewe mpiga gitaa, mtunzi wa nyimbo na mwimbaji mkuu.

Ujio wa wanadada hao ulikuwa ‘mtaji’ mkubwa kwa kundi la The Wailers kwa kuwa Rita alionyesha umahiri wake kwa kuipua albam iliyoitwa ‘Who Feels It Knows It’. Mwanadada Marcia alithibitisha dhahiri kwamba yeye ni mwimbaji bora huenda kuwazidi wenzie Juddy na Rita, aliposhirikiana vyema na Bob Marley katika santuri yake iitwayo ‘Young Giftted and Black’.

Ni ukweli usiopingika kwamba Bob Marley alitoa mchango mkubwa wa kuuza na kuusambaza muziki wa Regae Duniani kote hata kuwepo kwa gumzo kubwa kuhusiana na kundi zima la The Wailers. Kwa hakika kundi hilo lilijituma sana katika kuboresha muziki wa Regae na ndilo lilikuwa jipya lililounda nguvu ya The Wailers. Walitoa albam iliyowatia moyo ma-Rasta iliyoitwa ‘Natty Dread’ ambayo iliwaongezea hamasa vijana weusi wa Ulaya na Duniani kote.

Ilifika wakati Bob Marley na kundi lake la The Wailers, walivamiwa na kushambuliwa kwa risasi, ambapo watu wengi walihisi kuwa walishambuliwa kwa sababu ya mawazo yao hasa yaliyotokana na albam yao ya Natty Dread. Ilikuwa mwaka 1976, The Wailers walifikiria kufanya onesho la amani ambalo mada yake kubwa ingekuwa kuwaunganisha watu wa Jamaica, kuwasihi waache uhasama na ghasia, wafungue macho.

Jioni moja siku tatu kabla ya onyesho hilo, watu wenye bunduki waliwashambulia The Wailers ambao walikuwa wanafanya mazoezi ya muziki, ghafla wakasikia milio ya bunduki mlango ukafunguliwa huku mitutu ikitangulia na kutoa milipuko kadhaa, Bob Marley na Rita Marley walijeruhiwa.

Sababu ya mashambulizi hayo haikujulikana lakini hilo haikuwa kikwazo kwa Bob na The Wailers kusitisha onesho hilo. Mara baada ya onesho, Bob akaondoka zake kuelekea Miami, Marekani. Aidha Bob Marley alikuwa mwanaharakati wa kupigania Uhuru na haki kupitia muziki aliokuwa akiupiga katika staili ya midundo ya Regae.

Mfalme huyo wa muziki wa reggae alipinga ubaguzi kwa kiasi kikubwa kwa kusema kuwa: “wananiita chotara, lakini mimi siegamii upande wowote bali nipo upande wa Mungu aliye niumba kutoka kwa weusi na weupe…" Robert Nesta Marley alikuwa na kipaji pia alipendwa na wengi, si mashabiki tu hata baadhi ya wanamziki wenzie ambao ni mashuhuri katika ulimwengu wa muziki, walimkubali na kumheshimu kama vile Jimmy Cliff.

Marley aliwapenda wanawake, hasa wanawake wa matabaka la chini, la wakulima na wafanya kazi wa kipato cha chini, wanawake wa tabaka hizo aliwafahamu zaidi hasa wanawake weusi. Ndio maana katika wimbo wake wa ‘No Woman No Cry’ utusikia msimamo wa kisiasa wa Marley.

Bob Marley alifanya mambo mengi wakati wa uhai wake ikiwa ni pamoja na kujihusiha pia na michezo kama vile mpira miguu. Walipokuwa ziarani huko ulaya, Bob alikuwa na bendeji mguuni lakini hakuonesha wasiwasi tokana na jeraha alilolipata siku alipocheza mpira wa miguu.

Marley alipokuwa jukwaani akipiga muziki, alikuwa akirukaruka huku na kule kama mtu asiye na jeraha mwilini. Alikuwa akifanya mazoezi ya viungo kama kawaida, alikimbia kutoka studio na kuingia uwanjani kusakata kabumbu na mara kadhaa alionekana akikimbia mchaka mchaka.

Baadaye uvumi wa kutisha ukazuka kwamba mguu wa Bob Marley ulikuwa ukioza na ingebidi ukatwe. Baadae wataalamu wakitamka kuwa asingehitajika kuukata na wakasisitiza kwamba Marley angeendelea kuwa yule yule mwenye mwili mkakamavu, mcheshi, mchangamfu, mchezaji, mwanamuziki aliyeyumba na kutamba. Alikuwa akirukaruka jukwaa zima kama kawaida yake siku zote.

 Kumbe kulikuwa na ukweli wa kutisha kwamba tayari alikwisha patwa na Kansa ya Melanoma ambayo iliendelea kumtafuna ikiyaharibu maini pamoja na mapafu yake. Bob Marely ilifikia kuanguka wakati akikimbia mchaka mchaka, baada ya kupiga muziki maeneo ya Midson Sqare Gardens New York, nchini Marekani. Bob Marley akalazwa katika hospitali iliyoitwa Sloan Carttering ya jijini New York. Uchunguzi wa kina ulifanywa na matokeo ya uchunguzi huo, yalithibitisha ukweli wa kusikitisha juu ya afya yake.

Baada ya kutoonekana hadharani, uvumi ukaenea kuwa amekwenda Sheshamane nchini Ethiopia. Huko Sheshame ni sehemu maalumu kwa ajili ya wenye imani za Kirasta, japo hakuwa huko. Yeye alikuwa amekwenda Bad Wiese, nchini Ujerumani Magharibi ambako alilazwa kwa ajili ya matibabu katika hospitali mashuhuri kwa magonjwa ya Kansa ya Sun shine House Cancer Clinic.

Bob alipofika hospitalini hapo tayari alikuwa na uvimbe katika ubongo na alikuwa hawezi kutembea, alikuwa hoi bin taabani. Siku zilivyokuwa zikienda hali yake ikazidi kuzorota. Ukafikia wakati ambao yeye na daktari wake wabaini kuwa alikuwa mtu wa kuaga dunia wakati wowote.

Alipotambua kuwa mauti yake yamekaribia, Bob akaamua kufunga safari ya kurejea Jamaica ili akafie huko. Kinyume na alivyopanga kufika Jamaica akiwa hai, badala yake Bob Marley alifika huko akiwa ni marehemu.

Bob Marley alifariki dunia katika hospitali ya Florida, nchini Marekani Mei 11, 1981 kutokana na ugonjwa wa Kansa alioupata akiwa na miaka 36.
Mapema Bob alikataa kuandika urithi akiamini kuwa marastafari huwa hawafi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...