Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam.
Miaka mitatu imetimia tokea mwanamuziki nguli Papa Wemba, kufariki dunia.
Ilikuwa mithiri ya simulizi za ‘Alinacha’ asubuhi ya Jumapili Aprili 24 2016, kuzagaa kwa taarifa za kifo cha cha mtunzi na
mwimbaji mkongwe Papa Wemba kwamba amefariki dunia.
Taarifa hizo zilieleza kwamba nguli huyo alianguka jukwaani akiwa anatumbuiza jijini Abdjan, nchini Ivory Coast katika
tamasha la muziki la FEMUA.
Baadhi ya Wanabendi wake waliokuwa jukwaani, waliendelea kupiga dansi kabla ya mmoja wao kukimbia kumuokoa baada
ya kuona kasalia chini kwa sekunde kadhaa akiwa anatetemeka kisha akazirai.
Msemaji wake Henry Christmas Mbuta Vokia, alikaririwa akisema ’’marehemu Papa Wemba alikuwa ameingia muda mchache
tu jukwaani kisha akacheza wimbo wa kwanza, mashabiki wakamuomba awaimbie tena wimbo mwengine akakubali.
Lakini dakika chache tu baada ya kuanza kupiga wimbo wake wa tatu Papa Wemba alianguka na kuzirai ghafla jukwaani.
Watu wa Shirika la Msalaba Mwekundu walijaribu kumsaidia lakini hakuonesha dalili nzuri kwa hivyo wakampeleka hospitali,
lakini baada ya dakika karibu thelathini hivi tukaambiwa kuwa Papa Wemba ametuacha''
Watu walishuhudia kipande cha video kinachomuonesha jamaa mmoja akichukua microphone, halafu akairudisha kwenye steji.
Baada ya Pamba Wemba kuanguka, inadaiwa jamaa yuleyule badala ya kumsaidia alikimbilia kwenye ile microphone ili
isijulikane kwamba alibadilisha.
Baadhi ya watu wakazagaza taarifa kwamba microphone hiyo ilikuwa imewekewa sumu.
Taarifa za kifo chake ziliendelea kuwafikia watu mbalimbali akiwemo mwimbaji mkongwe wa Kongo DRC Koffi Olomide,
ambaye aliandika maneno machache kwenye ukurasa wake wa Instagram akisema ‘kwaheri Kaka, asante‘ na kuambatanisha
picha yao ya pamoja ya siku nyingi kwenye hayo maneno.
Koffi Olomide amekuwa akitajwa kuwa mpiga gitaa wa zamani na mtunzi wa nyimbo kadhaa zilizoimbwa na Papa Wemba.
Baada ya miezi kadhaa kupita tangu mumewe afariki, Marie Rose Lozolo, au kwa jina jingine mama Amazone, mke wa
marehemu Papa Wemba, alikutana na waandishi wa habari na kufunguka mengi kuhusiana na mpendwa wake huyo.
Alianza kwa kusema kuwa katika maisha yake ya miaka 45 ya ndoa na mumewe walipitia mambo mengi.
“Bado naona ugumu kuishi bila mume wangu kipenzi ambaye alikuwa ni mwanamuziki kamili, mpole sana. Awapo nyumbani
ni nadra sana kumsikia akiongea hovyo, lakini awapo jukwaani ni mtu mwingine tofauti kabisa, kwani huko ndiko ilikuwa
dunia yake…” alisema Marie Rose Lozolo.
Aliendelea kusimulia kuwa, sehemu nyingine ambayo alikuwa akionesha uchangamfu wa hali ya juu ni pale anapokuwa na jamaa zake.
Mama Amazone alifahamiana na Papa Wemba akiwa na umri wa miaka 15 tu, wakati marehemu mumewe alikuwa na miaka 20.
Katika kipindi chote alichoishi na mumewe hakuwahi kujua kama mumewe alikuwa na hadhi kubwa hadi pale alipofariki.
“Wakati akiwa hai alikuwa akipenda kunitania mara kwa mara, akisema siku atakayokufa ndiyo nitajua hadhi yake, pia
aliniambia angependa kifo chake kimkute akiwa kazini (Jukwaani ), kwa kweli utabiri wake ulitimia…” anasimulia Marie Rose Lozolo.
Alitamka kuwa hakuwahi kuambiwa na Papa kama ana mke mwingine au watoto zaidi ya binti mmoja ambaye alimlea yeye aitwaye Kukuna.
Mama Amazone alisema ataendelea kupigania haki miliki ya marehemu mumewe, kwani ameacha kazi nyingi na kubwa.
“Mume wangu alikuwa na nyimbo nyingi sana, kuna nyingine alishawahi kunitungia akinitamkia maneno haya; “Nasali nini
Mpo, Nakoma Mopaya, Na Motema nayo yebisa Nga, Yebaka bolingo Emata Nzete, Boni lelo tokomi Separer, Ngai Naleli Ngo,
Show me the Way, Maboko ezangi Amazone, Wemba alingaka, Ngai Naleli, Maboko ezangi Amazone, Jules Alingaka na
nyuingine nyingi.
Tafsiri yake: Hebu niambie inakuwaje, najikuta kama mgeni moyoni mwako, fahamu kwamba penzi lina nguvu ya kuupanda
mti hadi juu, vipi leo twafikia hadi kuachana! Nalia mie nalia kweli nammiss Amazone nimpendaye, mie Wemba nalia mie
Jules, naimiss mikono niipendayo ya Amazone.
Marie Rose Lozolo alisema kabla ya kifo cha mumewe, walikuwa jijini Paris nchini Ufaransa ambako alipatwa na homa
akalazwa hospitali kwa muda wa siku 10.

Iligundulika kuwa alikuwa na Malaria, baada ya kupata matibabu aliruhusiwa, lakini madaktari walimshauri apumzike kwa
muda wa wiki nne.
Baada ya wiki nne kumalizika wakiwa Paris, waliamua kuongeza wiki mbili zaidi za mapumziko. Baadaye kuingia studio
kurekebisha kazi ya albamu yake mpya ambayo tayari imeshatoka, kisha kurejea jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo DRC).
Kwa ujasiri mkubwa mama huyo aliendelea kusimulia kuwa, waliwasili Kinshasa akiwa na afya njema kabisa na alikuwa
akihudhuria mazoezini na vijana wake kama kawaida.
“Siku moja kabla ya safari ya Abidjan, tulikuwa na wageni nyumbani kwetu, baada ya wageni kuondoka majira ya saa nne
usiku, nilimuona mume wangu anapanga nguo zake kwenye begi, nikamuuliza kulikoni?
Akaniambia anajitayarisha kwenda mazoezini usiku huo, kwani asingeweza kurudi nyumbani kwakuwa asubuhi alitarajia
kusafiri na vijana wake kwenda nchini Ivory Coast ambako angefanya onesho…” alisimulia mjane huyo.
Mama Amazone alisema hakufurahishwa na utaratibu huo, kwa vile alihofia hatua ya mumewe kulala mazoezini kungeweza
kumsababishia matatizo ya kiafya, hivyo alimshauri kuachana na mpango huo, lakini Wemba alikataa.
Alisema kuwa mazingira waliyokuwa wanafanyia mazoezi hayakuwa rafiki, yalikuwa na mbu wengi, ndiyo sababu hakuafiki
uamuzi wake, akamshauri alale nyumbani, lakini aligoma.
“Nakumbuka siku mume wangu anasafiri ilikuwa Jumanne, ilipofika Ijumaa nikaenda kwenye ibada ya maombi, nikakaa huko mpaka Jumapili alfajiri ndio nikarudi nyumbani.
Ilipofika saa mbili asubuhi walikuja watu kuniamsha, huku wengine wakilia, nikajiuliza kuna nini? Wakaniambia mume wangu
amefariki,” alisimulia kwa uchungu mama Amazone.
Papa Wemba aliyekuwa nguli aliyezikonga nyoyo za wapenzi wa muziki wa Soukus nchini DRC na kote duniani kwa kipaji
chake cha kipekee na sauti isiyokuwa na mfano.
Wasifu wake unaeleza kuwa alizaliwa Juni 14 mwaka 1949, katika eneo la Lubefu - Wilaya ya Sankuru nchini Congo.
Majina yake halisi alikuwa akiitwa Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba, aliyeanza kazi ya muziki akiwa na umri mdogo mno.
Wemba alikuwa akimfuata mama yake katika matanga na hivyo akaibukia kuwa mtunzi wa nyimbo za kuomboleza.
Shungu Wembadio alijiunga na kundi la ''Stukas'' kabla ya kuliacha, akajiunga katika kundi kubwa la Zaiko Lana Langa
mwaka huohuo wa 1969.
Akiwa na bendi hiyo, sauti yake ya kipekee na uweledi wake uliisaidia kundi hilo katika utunzi wa nyimbo za "Pauline",
"Chouchouna" na "Liwa is somo".
Wemba wakati huo aliungana na wanamuziki wenzanke akina Nyoka Longo Jossart, Manuaku Pepe Felly, Evoloko Lay Lay,
Bimi Ombale, Teddy Sukami, Zamuangana Enock, Mavuela Simeon, Clan Petrole na wengine kadhaa.
Wakati Papa Wemba anaanza kupiga, jukwaa la muziki nchini humo lilikuwa limetawaliwa na vigogo wa muziki Franco
Luambo Luanzo Makiadi wa T.P.OK. Jazz, Tabu Ley Rochereau wa Afrisa Internationale, na makundi mengine mapya kama
vile Les Grands Maquisards, Le Trio Madjesi, Bella-Bella na Thu Zaina na Empire Bakuba.
Hata hivyo sauti ya kipekee ya Papa Wemba akijulikana wakati huo kwa majina yake kamili yakawa Jules Presley Shungu
Wembadio, aliyezikonga mioyo ya wapenzi wa Soukus.
Kilele cha ufanisi wa kundi la Zaiko Langa Langa ulikuja miaka ya mapema ya mwaka 1973.
Shungu ndipo alipobadili jina lake na kuanza kuitwa jina la utani ''Papa Wemba''.
Baada ya miaka mitano alilihama kundi hilo na kujiunga na kundi la Isifi Lokole. Hapo alitunga wimbo maarufu wa "Amazon",
aliokiri kuwa alimtungia mkewe.
Hata hivyo Papa Wemba aliamua kuliacha kundi hilo akaenda kujiunga na kundi lingine la Yoka Lokole, kabla yake kuunda
kundi lake la Viva La Musica" mapema mwaka wa 1977.
Vibao vyake ni kama Mwasi, Show me the way, Yolele, Mama, Proclamation "Chouchouna" alizotunga yeye Papa Wemba,
"Eluzam" na " Mbeya Mbeya", utunzi wake Evoloko Lay Lay, "BP ya Munu" uliotungwa na Efonge Gina, "Mwana Wabi" na
"Mizou" zilizotungwa na Bimi Ombale.
Wimbo wa "Zania" ulikuwa utunzi wake Mavuela Somo, Emotion, Wake Up, Maria Valencia, Le Voyageur,Rail On,
Kaokokokorobo, Legend tunzi zake nguli Papa Wemba.
Wembadio Papa Wemba aliwahi kukamatwa kwa madai ya ulanguzi wa binadamu.
Aidha Februari 18, 2003, maafisa wa idara ya upelelezi nchini Ufaransa walimkamata Papa Wemba kwa tuhuma za
kuwaingiza raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire wakati huo) barani Ulaya kinyume cha sheria.
Mahakama ya ubelgiji ilimpata na hatia mwezi Juni mwaka wa 2003, ikamhukumu kifungo cha mwaka mmoja na miezi mitatu jela.
Aidha mahakama hiyo ya Brussels ilimpiga faini ya Euro 22, 000. Hata hivyo alitumikia kifungo cha miezi mitatu na nusu
gerezani baada ya mdhamini kulipia dhamana ya Euro 30,000.
Papa Wemba alipoachiwa huru aliwaambia mashabiki wake kuwa aliyokumbana nayo akiwa gerezani yamemfunza mengi tu.
Katika utunzi wa wimbo wake "Numéro d'écrou" (2003), Papa Wemba alisimulia kukutana na mwenyezi Mungu akiwa gerezani.
Huyo na ndiye Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba ‘Papa Wemba’ aliyeiaga dunia akiwa na umri wa miaka 67.
Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0784331200, 0713331200, 0736331200 na 0767331200.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...