Mkurugenzi Mkuu wa Forum CC Rebecca Muna akizungumza leo kuhusu umuhimu wa wadau wa mazingira kuwa na jukwaa la pamoja la kujadiliana na kufikia makubakiano ya namna bora ya kukabiliana na changamoto zilizopo katika eneo la mazingira nchini.
Mchokoza mada Samuel Bubegwa akichangia wakati wa majadiliano ya wadau wa mazingira katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Dar es Salaam ambapo emetumia nafasi hiyo kushauri uwepo wa jukwaa la majadiliano ambalo litajikita kuweka mikakati ya kuondoa taka zikiwemo taka ngumu.
Ofisa Programu wa ForumCC Euphrasia Shayo akifuatilia majadiliano yaliyohusu mazingira ambayo yameandaliwa na ForumCC kwa kushirikiana na Halmashauri ya Ilala kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya(EU).
Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala Omar Kumbilatomo akizungumza kwa niaba ya Meya wa manispaa hiyo akizungumza wakati akifungua kikao cha majadiliano  kiichowakutanisha wadau wa mazingira na ForumCC.
 Moja ya wadau wa mazingira Kahana Lukumbuzya akichangia mada wakati wa kikao cha majadiliano kuhusu uboreshaji wa mazingira ya Halmashauri ya Ilala jijini Dar es Salaam.
 Wadau wa mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam wakifuatilia majadiliano yaliyohusu kuwekwa mikakati ya kuweka mazingira safi ya manispaa hiyo.

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
SHIRIKA la FORUMCC kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam wamewakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili changamoto za kimazingira na kutafuta ufumbuzi wake kwa hamashauri hiyo.

Mjadala huo unafanyika chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya(EU) kupitia Mradi wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi. EU wamekuwa wakishirikiana kuandaa mijadala na makongamano yanayohusu kujadili mabadiliko ya tabianchini na hali ya mazingira nchini kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa akifungua majadiliano hayo Meya wa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam Omari Kumbilamoto amesema ni jambo muhimu wadau kukutana na kuweka mikakati itakayosaidia kuweka mazingira safi.
“Tunashukuru kwa uwepo wa majadiliano haya yanayohusisha sekta binafsi na Serikali kwa kuangalia namna gani wanaweza kukabiliana na taka ngumu.Mjadala umekuja wakati muafaka hasa kwa kuzingatia tayari Serikali imetoa tamko la kuzuia plastiki ambalo binafsi na Halmashauri ya Ilala tunaunga mkono katazo hilo,”amesema.

Amesema Manispaa ya Ilala imekuwa na jitihada mbalimbali katika utunzaji mazingira kwa kuweka mbinu na mifumo sahihi za usafi mazingira huku akisisitiza kutambua mchango wa sekta binafsi katika jitihada hizo.

Pia ameshauri kampuni ambazo zipo Manispaa ya Ilala na zinatoa huduma za kubeba taka ngumu pamoja na kufanya vizuri maeneo ya kati ya Jiji ni vema pia wakaweka nguvu kubwa katika kuzoa taka maeneo ya pembezoni.
“Ni lazima kuwepo na mipango madhubuti ya kuzoa taka katika Manispaa ya Ilala.Pia niwakumbushe wenye kampuni za kuzoa taka kuendelea kushirikiana na wananchi na vema nikaeleza gharama ya Sh.3000 ya taka nayo inaonekana kuwa changamoto kwa wananchi walio wengi, hivyo mtaangalia namna ya kufanya.

“Tunatarajia majadiliano ya leo yatakuwa na ufumbuzi mzuri katika kumaliza changamoto za taka na kuweka mazingira safi lakini nikiri bado tunayo changamoto ya dampo na kwa bahati nzuri wenzetu wa Jiji wameahidi kutafuta ufumbuzi kwa kuwa na dampo la kisasa,”amesema Kumbilamoto.

Pia amesema pamoja na Manispaa ya Ilala kukusanya mapato mengi yatokanayo na vyanzo mbalimbali vya fedha lakini ifahamike kuwa imekiwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya masuala mbalimbali yakiwamo ya sekta ya afya na kufafanua Ilala tayari imetenga Sh.milioni 52 kukabiliana na Dengue na wakati huo huo kuna viashiria vya magonjwa ya mlipuko ,”amesema Kumbilamoto.

Wakati wa majadiliano hayo imefafanuliwa katika katika eneo la taka ngumu bado kunachangamoto kubwa na hivyo wadaua wameamua kuweka mikakati ambayo itasaidia kuondoa taka hizo.Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa ForumCC Rebecca Muna amesema lengo la kuwakutanisha wadau hao ni kuhakikisha kunakuwa na makubaliano ya pamoja katika kukabiliana na changamoto ya uwepo wa taka ngumu.

Amesema wanatambua dhamira njema ya Serikali ya kuondoa taka hizo ikiwemo mifuko ya Plastiki, hivyo Forum CC kwa kushirikiana na wadau wengine wa mazingira wanawajibu kuwa sehemu ya kufanikisha malengo ya Serikali.

 Pia ametumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa kuhakikisha kila mmoja wetu kwa maana ya Serikali, wadau na mtu mmoja moja anakuwa sehemu ya kufanikisha mazingira yanakuwa salama.

“Forum CC ni shirika ambalo si la kiserikali ambalo limekuwa likiandaa majadiliano yanayohusu mabadiliko ya tabianchi.Kwa kuwa tunatambua tunaingia kwenye katazo la mifuko ya plastiki tukaona iko haja ya kukutanisha wadau kuweka mikakati ambayo itsaidia kuondosha plastiki ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa kimazingira,”amesema Muna.

Amefafanua uchafuzi wa mazingira una madhara makubwa yakiwemo ya kutumia fedha nyingi kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hivyo ni vema wadau wakaendelea kuweka mikakati ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi,”amesema.

Hata hivyo amesema kuwa kikubwa ambacho kinahitaji ni kuweka uwajibikaji ambao utakuwa na tija kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yao iwe kwa upande wa serikali au wadau wa mazingira.

Mmoja wa wachokozi wa mada Samuel Bubegwa wakati akichangia majadiliano hayo amefafanua kwa Manispaa ya Ilala wamekuwa na mfumo mzuri katika kuweka mfumo wa uzoaji taka na kuweka mazingira safi na kuomba ni vema Ilala ikaangalia namna ya kukutana na viongozi wa ngazi za juu serikalini ili kuwaelimisha namna wanavyofanya katika eneo la mazingira.

Pamoja na mambo mengine sehemu kubwa ya taka ngumu zilikuwa zinatokana na plastiki na saas kuondolewa kutasaidia kimazingira huku akishauri uwepo wa jukwaa kati ya wakandarasi, wadau  na Serikali katika uondoshaji wa taka.

Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa kwa manispaa ya Ilala taka ambazo zinazalishwa kila siku ni tani 2000 na hivyo ni jukumu la wadau mbalimbali kushirikiana katika kuondoa taka hizo na Ilala imekuwa ikijitahidi katika kuweka mazingira safi.

Kwa upande wake Ofisa Mazingira Mkuu wa Baraza la Mazingira la Taifa(NEMC) Mhandisi Benjamin Mchwampaka amesema suala la uwepo wa uchafuzi wa mazingira linatokana na tabia na hivyo ni vema wananchi wakabadili tabia.

Amesema kuna kila sababu ya taka kuwekwa kulinana na aina ya taka zenyewe, ikiwemo taka zinazooza, taka ngumu pamoja na taka zenye kemikali za sumu na kila familia ikiweza kutenganisha taka uwezekano wa kudhibiti taka ngumu utafanikiiwa.
Mwisho  


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...