Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

KWANZA kabisa naomba nitumie fursa hii kukusabahi na natumai uko poa na mambo yanasonga.

Pia sote tunafahamu Taifa letu lipo katika majonzi kutokana na kifo cha mpendwa wetu Dk.Reginald Mengi aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Mei 2, 12019 akiwa Dubai. Mungu ilaze roho yake mahala pema peponi.Amina.

Baada ya hapo sasa tuendelee iko hivi ukweli uliopo wasanii nchini Tanzania na hasa wa muziki wa kizazi kipya a.k.a Bongo Fleva wamekuwa wakitumia fedha nyingi sana pindi wanapohitaji kurekodi video za nyimbo zao.

Ni mara kadhaa tumeshuhudia wakifunga safari kwenda nje ya Tanzania ili kupata maeneo ya kurekodi nyimbo zao. Wanamini nje ndiko kuzuri kwa kurekodi video zao kuliko nyumbani.Jamani sio kweli, ninao ushahidi.

Nikiri Watanzania walio wengi tunayo kasumba nikiwemo mimi kasoro wewe tu unayesoma hapa ya kuamini vya nje ni bora zaidi kuliko vya kwetu.Na ndicho kinachowasumbua wasanii wetu.Si wote ila wengi wao wako hivyo.Usikatae ndio ukweli.

Sasa umefika wakati kwa wasanii kubadili matazamo na fikra kwasababu katika ardhi ya Tanzania ambayo Mungu ameipagilia na ikapangika kuliko mahali popote tuna kila kitu.

Ndio maana Wazungu wanafunga safari kuja nchini kwetu kutalii.Tunavyo ambavyo wao hawana.Mungu ametupendelea Watanzania.Tunayo sababu ya kumshukuru kwa kusema Ahsante Mungu.

Chonde chonde wasanii wa Tanzania.Narudia tena chonde chonde, nyumbani kuna maeneo mazuri ya kurekodi video zenu.Niwahakikishie hamtajuta kutumia mazingira ya nyumbani kwa ajili ya video zenu.

Nashukuru Mungu baadhi ya wasanii wameona haja ya kubadili mtazamo wao na sasa wameamua kubaki na Tanzania yao katika kufanya kazi zao za muziki.

Wasanii Amini Mwinyimkuu na Linna Sanga wameonesha njia kwa wasanii wenzao.Unajua ambacho wamekifanya? Nikukumbushe wasanii hao wametoa nyimbo yao mpya inayofahamika kwa jina la Nimenasa.Nyimbo tamu balaa.

Katika kuhakikisha video ya wimbo huo inakuwa bora na ya kuvuta wakaona isiwe taabu, wakafunga safari hadi kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) kwa ajili ya kuomba eneo la kurekodi video yao.

Kwa moyo wa upendo walionao TFS kwa wasanii wa nchi yetu, wala wahakujiuliza mara mbili, walikubali ombi la wasanii hao. Na sio kukubali tu bali waliamua kufadhili na gharama ya video yenyewe kwa asilimia 80.Hongereni TFS.

Kwa dhamira njema ya TFS kwa wasanii, ni wajibu wa kila msanii iwe wa Bongo Fleva,Bongo Movie na hata wale wa filamu za 'Action' kuhakikisha mnakuwa karibu nao.Wameamua kutoa maeneo yao kwa ajili yenu pale mnapotaka kufanya kazi zenu.

Wapo tayari kusaidia hata kama isiwe fedha basi hata kutoa watalaam wao ili kushauri sehemu nzuri itakayofaa kwa msanii kurekodi kazi yake kulingana na mahitaji yake. Mnataka nini tena?

Kaimu Meneja Mawasiliano wa TFS Tulizo Kilaga amefafanua kwa kina sababu za kuamua kuwawezesha wasanii Amini na Linna kurekodi video yao ambapo amesema msingi mkubwa ulitokana na ombi la wasanii hao la kuomba eneo lenye mazingira asili zaidi ili kupata muonekana wanaouhitaji.

"Walikuja kwetu kuomba maeneo ya kwenda kurekodi video ya Nimenasa.Kwetu TFS tukaona hii ni fursa kwa umaarufu wa wasanii haoa na kampeni yetu ya kuhamasisha utalii wa ndani basi tunaamini ujio wao utatusaidia kuongeza idadi ya watalii wa ndani.

"Hivyo tuliwaelekeza video yao wakaifanyie Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Magamba ulikopo wilayani Lushoto mkoani Tanga. Kuna maeneo mengi mazuri yakiwemo maporomoko ya maji , wanyama , mimea , ndege, pango la Mjerumani na kila aina ya kivutio kilingana na mashairi ya wimbo wao,"amesema Kilaga.

Amefafanua kwa kuwa wasanii hao walionesha nia TFS imeona ni jukumu lake kuhakikisha kila ambacho wanakihitaji kinapatikana na uzuri wao wanasimamia hifadhi za misitu 17 nchini kote.

"Sababu za kufanya hivyo tunataka wasanii hawa baada ya kwenda Magamba wawe mabalozi kwa wasanii wengine kwa kuwaambia hakuna sababu ya kuumiza kichwa kwa ajili ya maeneo ya kufanya video zao kwani hapa nyumbani yapo.TFS tunasimamia hifadhi ya misitu 17 na kote huko kuna kila kitu ambacho msanii anahitaji.

"Kikubwa wasanii wanatakiwa kufika katika ofisi za TFS na kisha kueleza tu wanataka maeneo ya aina gani na sisi tutawapa maelekezo ya mahali pa kwenda na si kwa wanamuziki wa kizazi kipya hata wale ambao wanarekodi video za ngumi,"anasema.

Ameongeza kuna maeneo mengi ambayo wasanii wanaweza kutayatumia kurekodi na kazi zao zikapendwa na msanii haitaji kutumia nguvu kutafuta maeneo, bali wao wafike tu TFS.

Ameongeza wasanii wanapaswa kujivunia uwepo wa misitu iliyopo nchini Tanzania, kwani ina kila kitu ambacho kinaweza kuwepo kwenye kazi zao na kwamba TFS ipo tayari kutoa ushauri kwa wasanii.

Amesisitiza " Tupo katika kipindi cha kufanya promosheni hasa kwa kuzingatia tunaelekea kwenye msimu wa utalii.Hivyo ujio wa Linna na Amini ni sehemu ya kufanya hamasa ya kuvuta Watanzania wengine kwenda maeneo ya utalii".

Pamoja na mambo mengine, Tulizo anasema msanii anaweza kwenda katika Istagram ya TFS na kisha akatoa mawazo na ushauri wake na baada ya hapo wao wataufanyia kazi.

Kwa upande wake Amini anasema anatoa rai kwa wasanii nchini kuhakikisha wanaitumia hifadhi za misitu ya asili kwa ajili ya kufanya kazi zao za sanii kwani hakuna ambacho kinakosekana huku akieleza kuwa anao ushahidi kwani yeye amepata nafasi ya kurekodi video ya Nimenasa katika msitu wa Magamba.

Wakati Linna anasema hakuwahi kufikiria kama nchini kwetu kuna maeneo mazuri ya asili ambayo yaaweza kutumiwa na wasanii kurekodi kazi zao, hivyo naye amesema ni wakati muafaka kwa wasanii kutumia mazingira ya nyumbani kufanya kazi zao za muziki.

 Msanii Linna Sanga akiwa amekanyaga mgongo wa Kaimu Meneja Mawasiliano wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)Tulizo Kilaga ili kumsaidia kupita aende kurekodi kipande cha video kitakachokuwemo kwenye wimbo wa Nimenasa.Aliyeshika mkono ni msanii Amini Mwinyimkuuu.
 Amini Mwinyimkuu na Linna Sanga wakiwa katika Msitu wa Magamba baada ya kupewa kibali na TFS warekodi video yao ya wimbo unaofahamika kwa jina la Nimenasa.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...