Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (mwenye kinasa sauti) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Vuo wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, baada ya kuwasha umeme kijijini hapo akiwa katika ziara ya kazi Mei 18, 2019. Kushoto kwa Waziri ni Mbunge wa Jimbo la Mkinga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula.

Na Veronica Simba - Tanga

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, ameuagiza uongozi wa juu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukata asilimia 10 ya malipo ya Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Tanga, endapo itabainika hana sababu za msingi kuchelewesha mradi.

Alitoa maagizo hayo Mei 18 mwaka huu katika Kijiji cha Vuo, Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.

Akizungumza na wananchi wa Vuo, kabla ya kuwawashia rasmi umeme, Dkt. Kalemani alisema kasi ya mkandarasi hairidhishi maana ni ndogo sana hivyo akawataka watendaji wa TANESCO kufuatilia ili kujiridhisha endapo kuna sababu za msingi za ucheleweshaji huo wa mradi.

Mkurugenzi TANESCO fuatilia; ukikuta kuna uzembe, wakate asilimia 10 ya mshahara wao maana wanataka kutucheleweshea mradi.

Sambamba na agizo hilo, Waziri alielekeza mkandarasi huyo kuwa na Mpango-Kazi wenye mchanganuo wa kuwasha umeme katika vijiji vitatu kila wiki.

Kufuatia agizo hilo, alimtaka Meneja wa TANESCO wa Wilaya, kumwandikia barua ya kusitisha mkataba wake, Mkandarasi husika endapo atashindwa kuwasha umeme katika vijiji vitatu kila wiki.

Aidha, Waziri alimtaka Meneja huyo pamoja na Mkandarasi kuwasilisha maelezo ndani ya siku moja sababu za kusuasua kwa utekelezaji wa mradi.

“Meneja wewe ndiye wa kumsimamia Mkandarasi. Kama kasi yake ni duni, inamaanisha hata wewe utendaji wako siyo mzuri,” alisema Waziri.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani alibainisha kuwa moja ya sababu za Mkandarasi kuwa na kasi ndogo yawezekana kuwa ni uhaba wa vibarua alioanao. Alimtaka kuongeza idadi ya vibarua mara moja na kwamba vibarua hao watoke eneo husika na awalipe ujira wao kwa wakati.

“Ni marufuku kuajiri vibarua nje ya eneo unakotekelezwa mradi. Vibarua wote wawe wa eneo husika ili wanufaike kwa uwepo wa mradi katika eneo lao.”

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali ya Wilaya za Mkinga, Pangani na Muheza, ambako alikagua utekelezaji wa miradi ya umeme pamoja na kuwasha umeme katika vijiji kadhaa; Waziri Kalemani alitoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kulipia gharama za kuunganishiwa umeme ambazo ni shilingi 27,000 tu.

Aidha, aliwataka wale ambao tayari wameunganishiwa umeme, kuutumia kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi ili wanufaike kwa kuinua kipato na kuboresha maisha yao.

Waziri alitoa zawadi ya vifaa vya Umeme Tayari (UMETA), kwa wananchi katika maeneo yote aliyotembelea ili kuwahamasisha kuchangamkia fursa ya uwepo wa mradi wa umeme vijijini na hivyo kujitokeza kwa wingi kulipia na kuunganishiwa nishati hiyo.

Katika Shule ya Sekondari Bushiri wilayani Pangani, Waziri alikabidhi vifaa 40 vya UMETA kwa wanafunzi na walimu, ili vifungwe katika vyumba vya madarasa, maabara, ofisi, nyumba za waalimu, vyoo na barabara zote za shule ili pamoja na mambo mengine kuhakikisha usalama wa watoto, hususan wa kike.

Waziri anaendelea na ziara yake mkoani Tanga ambapo anatarajiwa kuhitimisha kwa kutembelea Wilaya ya Korogwe.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Vuo wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, kabla ya kuwasha umeme kijijini hapo akiwa katika ziara ya kazi Mei 18, 2019.
Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Dustan Kitandula, akizungumza wakati wa Hafla ya kuwasha umeme katika kijiji cha Vuo, wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga. Tukio hilo lilifanywa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto), Mei 18, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.
Mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme vijijini mkoani Tanga, Ahmed Hemed kutoka kampuni ya JV RADI Services Njarita & Aguila (kushoto), akizungumza na wamiliki wa nyumba inayoonekana pichani, Sabasaba Hassan na mama yake, muda mfupi baada ya Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kuiwashia umeme, akiwa katika ziara ya kazi, Mei 18, 2019.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akitoa maelekezo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), alipokuwa katika ziara kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga, Mei 18, 2019.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bushiri, wilayani Pangani, Mkoa wa Tanga, alipofika kuwawashia umeme shuleni hapo, akiwa katika ziara ya kazi, Mei 18, 2019.


Taswira ya baadhi ya nyumba za wakazi wa Wilaya za Mkinga, Pangani na Muheza mkoani Tanga, kama zilivyonaswa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Mei 18 mwaka huu. Waziri aliziwashia umeme nyumba hizo na kusisitiza kwamba ni marufuku kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kubagua aina ya nyumba wakati wa kuunganisha umeme.
Sehemu ya wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, pamoja na viongozi na wataalamu wengine mbalimbali wa Serikali, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Vuo, Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga, akiwa katika ziara ya kazi, Mei 18, 2019.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...