Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameupongeza Uongozi wa shule ya Dar es Salaam International Academy kwa kuwajengea uwezo na kuona umuhimu wa kuwafundisha na kuwapa nafasi wanafunzi kujifunza wenyewe.

Prof. Ndalichako ametoa pongezi hizo jijini Dar es Salaam aliposhiriki katika maonesho mbalimbali ya wanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo ambapo amesema wanafunzi hao wamefundishwa kutafuta taarifa mbalimbali kutokana na mada walizopewa.

“Nimefurahi kuona wanafunzi wa darasa la tano wanaonesha ubunifu katika kuangalia matatizo ya jamii kwani hata mada walizoangalia zinaendana na hali halisi ya sasa ambayo serikali imekuwa ikiwekea msisitizo kama masuala ya jinsia, magonjwa ya homa ya ini na Ebola, dawa za kulevya pamoja na Teknolojia,” amesema Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema katika kutafuta taarifa wanafunzi hao wameonyesha vipaji vya hali ya juu wakati wa kuandaa mada za maonyesho kwani wametumia mitandao pamoja na kuwahoji watu waliowaona muhimu kuwapatia taarifa zilizowawezesha kukamilisha mada zao kwa ajili ya maonyesho hayo.

Aidha, Waziri Ndalichako ametoa wito kwa walimu kuwawezesha na kuwapa nafasi wanafunzi katika kuwa na ubunifu, kujiamini na kuweza kutafuta taarifa mbalimbali katika kujifunza kwani wanafunzi wa kitanzania wana uwezo wa kufanya mambo makubwa sana lakini wanakwama kutokana na kushindwa kujiamini na uoga wakati shuleni ni sehemu ambayo vipaji hivyo vinaweza kuendelezwa.

“Suala la kujiamini ni changamoto kubwa kwa watanzania wengi, wana uwezo, akili na vipaji lakini wanakuwa hawajiamini hili ni tatizo, kwa hiyo tuendelee kuwa na maonyesho kama haya ambayo yatawajengea wanafunzi wetu uwezo, kujiamini, kuonyesha yale wanayoweza na kutoogopa kusema mbele za watu,” amesisitiza Waziri Ndalichako.

Aidha, Waziri Ndalichako amesema hata katika shule za serikali maonyesho kama hayo yanafanyika katika ngazi ya shule za sekondari ambayo yanaanza katika ngazi ya shule, wilaya na kilele inakuwa katika ngazi ya Kitaifa hata hivyo wameahidi kuangalia namna ya kuanza kushirikisha wanafunzi wa shule za msingi kwani kufanya hivyo inawezesha kuwaandaa wabunifu tangu wakiwa katika umri mdogo.

Akizungmzia mkakati wa serikali wa kutambua na kukuza ubunifu nchini Waziri Ndalichako amesema kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia inazo atamizi ambazo zinatumika kuendeleza ubunifu lakini pia imeona si rahisi kila mtu kuweza kufika katika Tume hiyo hivyo imeanza utaratibu wa kuanzisha katika ngazi za Halmashauri ambapo mwaka huu mwongozo umetoka wa kuangalia namna gani wabunifu wakitambulika wanaweza kuendelezwa.

“Pia katika vyuo vikuu vyetu kuna hatamizi kwa mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Nelson Mandela kuna atamizi ambazo zinafanya vizuri sana na wao wamejikita katika mazao na kuangalia vitu ambavyo vinaweza kuweka sumu katika mazao lengo ni kuhakikisha tunaongeza wigo ili vipaji wa watanzania viweze kuendelezwa,” amesema Ndalichako.

Naye Mkuu wa Shule hiyo, Fawzya Hirji amesema shule hiyo imejipanga kuhakikisha kunakuwa na ushirikiano kati ya walimu, wanafunzi na wazazi katika kuwawezesha wanafunzi hao kuwa na uwezo wa ubunifu, kujiamini na kutumia mitandao katika kutafuta taarifa mbalimbali zinazowapatia maarifa ya kujua mambo mbalimbali duniani.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipata maelezo kwa wanafunzi wa darasa la tano wa Shule ya Dar es Salaam International Academy.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipewa maelezo na wanafunzi wa Shule ya Dar es Salaam International Academy jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipata maelezo kwa wanafunzi wa darasa la tano wa Shule ya Dar es Salaam International Academy.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipewa maelezo na wanafunzi wa Shule ya Dar es Salaam International Academy jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...