RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein amewanasihi wafanyabiashara kuwa waadilifu katika kuwafanyia wanunuzi tahafifu za bei za bidhaa na huduma nyenginezo hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo katika risala maalum aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari katika kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika mwaka huu wa 1440 Hijria sawa na mwaka 2019 Miladia.
Katika risala yake hiyo, Alhaj Dk. Shein aliwataka wafanyabiashara kukumbuka kwamba kwa kufanya hivyo hawatokula hasara bali watazidi kupata fadhila mbali mbali za Mola wao Mlezi zinazoambatana na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Aidha, aliwataka wakulima waendelee na ustaarabu pamoja na utamaduni wao ule ule wa ustahamilivu na uadilifu kwa kujiepusha na tabia ya uvunaji na uuzaji wa mazao machanga.
Rais Dk. Shein aliongeza kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar si kumkomoa mtu kwa sababu Serikali huwa haiwakomoi wananchi wake bali dhamira yake ni kuwalinda na kuona kwamba hawafikwi na matatizo ambayo yanaweza kuepukika na kujikinga nayo.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alitoa nasaha zake kwa wale ambao si Waislamu na wale ambao watakuwa na dharura zinazowazuwia wasifunge kuwa wasifanye vitendo vitakavyoathiri wanaofunga.
Alhaj Dk. Shein alisisitiza haja ya kuhimizana zaidi kuisoma Qur-an kwa wingi ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na kujitahidi kufahamu mantiki ya maelekezo yake.
Aliwataka waumini kuhimizana kuhudhuria darsa katika misikiti ndani ya mwezi wa Ramadhani na kuepuka kutumia muda kwa kufanya mambo yasiyo na manufaa katika mwezi huo ambayo yanapingana na mafunzo ya Uislamu na silka zao.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwatakia kila la heri Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi wakiongozwa na Spika Zubeir Ali Maulid katika Mkutano wao wa 14 wa Baraza la Tisa la Wawakilishi utakaojadili Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha wa 2019-2020.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...