*Mkewe aeleza mchango wake katika jamii, aomba radhi kwa yeyote aliyewahi  kukwaruzana na na Captain Komba

*Vijana waombwa kujitokeza kwa wingi katika usahili ili kuweza kupata ajira

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii

TAASISI ya The Captain Komba Arts Memorial Foundation ambayo imeanzishwa kwa ajili ya kuenzi na kuendeleza mchango wa marehemu Komba katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kijamii na sanaa inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Julai 6 mwaka huu huku katibu mkuu wa chama cha mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally akitarajiwa kuwa mgeni rasmi akiongozana na viongozi mbalimbali wa vyama, wabunge, wawakilishi kutoka serikali ya Zanzibar, wadau wa sanaa na wasanii.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam katibu mkuu wa taasisi hiyo ambaye pia ni mjane wa Captain Komba; bi. Salome Komba amesema kuwa taasisi hiyo imesajiliwa  kwa sheria ikiwa na malengo ya kuenzi na kuendeleza mchango mkubwa alioufanya marehemu Komba na jitihada hizo zilianza kufanyika mwaka 2018 ambapo taasisi hiyo ilifanikiwa kuanzisha ujenzi wa jengo la makumbusho la kumuenzi marehemu Komba ambapo Waziri wa habari, sanaa, utamaduni na michezo Dkt. Harrison Mwakyembe aliweka jiwe la msingi.

Bi. Salome amesema kuwa taasisi hiyo itazinduliwa rasmi siku ya Julai 6 katika viwanja vya kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam na hiyo itatanguliwa na usahili utakaofanyika katika idara ya sanaa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam tarehe 22 na 23 mwezi Juni kwa vijana wenye vipaji vya kuimba kama marehemu Komba na uwezo wa kubuni aina nyingine ya uimbaji, wapiga drums, gitaa, solo pamoja na kinanda na kueleza kuwa vijana watakaopita katika usahili watapewa ajira na kuwa chini ya usimamizi wa taasisi hiyo.

Pia ametumia nafasi hiyo kuomba radhi kwa niaba ya marehemu Komba kwa yeyote aliyekwazana naye huku akitoa shukrani kwa marais wa awamu zote tano ambao amefanya nao kazi, watanzania wote hasa wananchi wa jimbo la Nyasa na kusema kuwa wataendelea kukienzi chama cha mapinduzi (CCM) kwa kuwa ndicho kilichomlea, kumkuza na kumpa umaarufu marehemu Komba.

Akizungumzia vigezo vya ushiriki kwa vijana hao mratibu  na mmoja wa majaji wa shughuli hiyo Catherine Kahabi amesema kuwa mshiriki anatakiwa awe mtanzania mwenye akili timamu  na mwenye umri wa miaka 18 hadi 25 huku wakitakiwa kujiandaa kwa nyimbo mbili alizoimba marehemu Komba enzi za uhai wake ambazo ni Mgeni na CCM mbele kwa mbele na jopo la majaji waliobobea fani ya sanaa watawasahili.

Bi. Catherine amesema kuwa kila mshiriki atajaza fomu bure na fomu hizo zinapatikana nyumbani kwa marehemu Komba Mbezi Beach Tank Bovu na katika ukumbi wa idara ya sanaa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Captain John Komba aliyefariki dunia tarehe 28 Februari, 2015 mchango wake katika sanaa, jamii na siasa hauwezi kusahaulika na siku ya kuzindua rasmi taasisi hiyo bendi mpya, THT, TOT na wasanii watatumbuiza bure bila kiingilio.
 Katibu na mjane wa marehemu bi. Salome Komba akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uzinduzi wa taasisi wa kumuenzi marehemu Komba, ambapo ameeleza kuwa sauti ya mume wake iliyokuwa ikimkosha na kumfanya alale vizuri hivyo hana budi kuenziwa.
 Mkurugenzi wa TOT Gasper Tumaini akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa mchango wa marehemu Komba katika jamii ni mkubwa na ataenziwa daima, leo jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa majaji na mratibu wa shughuli hiyo  Catherine Kahabi akitoa akitoa vigezo kwa washiriki watakaounda bendi hiyo mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...