Na Peter Haule, WFM, Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango amewataka Mameneja wa TRA wa mikoa na Wilaya nchini kote kusimamia vema ukusanyaji wa kodi za majengo na kuhakikisha kuwa viwango vinavyotozwa ni vile vilivyoko kisheria.
Dkt. Kijaji ametoa rai hiyo mjini Dodoma baada ya kupata malalamiko kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi Mheshimiwa Yahaya Masare, kwamba Mamlaka ya Mapato mkoani Dodoma imempelekea ankara ya kodi ya jengo na kumtaka alipe shilingi laki moja badala ya shilingi elfu 10 zilizoainishwa kisheria kwa majengo ya kawaida.
Dkt. Kijaji ambaye alifika kwenye makazi ya Mbunge huyo, katika Mtaa wa Uzunguni Jijini Dodoma, alibaini kutokuwa na mawasiliano ya kutosha kati ya TRA  na wateja wake jambo lililosababisha malalamiko ya mteja huyo na kuagiza Mameneja wa TRA mikoa na wilaya kuhakikisha wanawafikia wateja badala ya kuwaachia kazi viongozi wa mitaa peke yao.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mhe. Yahaya Masare  alimweleza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji kwamba alishitushwa na hatua ya TRA mkoa wa Dodoma kumpelekea ankara hiyo yenye kiwango kikubwa cha madai wakati anafahamu vema sheria ya kodi ya majengo iliyopitishwa bungeni imeainisha viwango vya kodi kwa kila jengo lililoko katika maeneo ya mijini na vijijini
Kwa upande wake Meneja wa TRA mkoa wa Dodoma Bi. Kabula Mwemezi, amekiri kuwepo kwa kasoro ya ankara waliyompatia Mbunge huyo na kujitetea kwamba hali hiyo ilitokana na taarifa walizonazo zinazohusu wateja wote wanaomiliki majengo na kwamba suala hilo limepatiwa ufumbuzi
Bi Mwemezi aliwataka wateja wenye malalamiko kuhusu ankara walizo letewa kutoa taarifa kabla hawajalipa ili waweze kupatiwa suluhisho.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa tatu mbele) akiwasili katika nyumba ya Mbunge wa Manyoni Magharibi Mhe. Yahaya Masare, ili kutatua malalamiko ya kodi ya Majengo katika Mtaa wa Uzunguni Jijini Dodoma
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia) akitoa ufafanuzi wa kodi ya majengo kwa Mbunge wa Manyoni Magharibi Mhe. Yahaya Masare, alipofika kujionea hali halisi ya nyumba na bili aliyotakiwa kulipa ya Sh. 100,000, jijini Dodoma
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto), Mbunge wa Manyoni Magharibi Mhe. Yahaya Masare (katikati) na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Dodoma Bi. Kabula Mwemezi wakizungumza jambo.
Nyumba ya Mbunge wa Manyoni Magharibi Mhe. Yahaya Masare , iliyopo jijini Dodoma ambayo TRA walimtaka alipe Sh. 100,000 badala ya Sh. 10,000 jambo liliomfanya Mbunge huyo kufikisha malalamiko kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ambaye alilipatia ufumbuzi suala hilo. 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...