Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.

KANISA la Evangelistic Assemblies Of God Tanzania (EAGT), limemfungulia kesi katika baraza la ardhi mtoto wa marehemu, Mchungaji John Mfuko aliyekuwa Mwenyekiti wa wadhamini wa kanisa hilo, Frida Mfuko kwa madai kuwa amevamia eneo lililopo katika kiwanja namba 154 Kitalu II kilichopo Temeke.

Kesi hiyo yenye namba 127/2019, imefunguliwa na kanisa hilo katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Temeke mbele ya Mwenyekiti wa Baraza hilo, Amina, ambapo mdai namba moja ni EAGT.

Mbali na dhehebu hilo, wadai wengine waliofungua kesi hiyo ni Mchungaji Sara Samson, Wilbroad Adebe na Enosi Ndembeta ambao ni wazee wa kanisa liliko katika eneo linalogombaniwa, ambapo wote wanadai kuwa Frida amevamia eneo hilo.

Kesi hiyo, inatarajiwa kuanza kusikilizwa Julai 19,2019 ambapo Sara na wenzake waliwasilisha zuio wakiomba isikilizwe chini ya hati ya dharura huku Frida akiomba apewe muda wa kuwasilisha utetezi wake.

Aidha, kabla ya kesi hiyo kupelekwa mahakamani, viongozi wa jimbo wa EAGT walifika katika eneo hilo linalogombaniwa na kumtangaza Mchungaji Samson kuwa mchungaji katika kanisa aliloliacha Marehemu Mchungaji John, jambo ambalo limekataliwa na waumini wa kanisa hilo.

Akizungumza hivi karibuni, Frida amesema baba yake ni mmoja wa waanzilishi wa kanisa hilo tangu 1993, baada ya kutokea kwa mgogoro katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) ambapo baba yake, Marehemu Mchungaji Mfuko alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa EAGT hadi pale kifo kilipomkuta Agosti Mosi, 2018.

Amesema Mei 5,2013 wajumbe watatu wa bodi ya wadhamini walikaa kikao na kuidhinisha kuwa kiwanja hicho si mali ya EAGT bali ni mali ya Marehemu Mchungaji John Mfuko na hivyo,wadhamini waliaamua kumilikisha kiwanja hicho. 

"Baraza la wadhamini lilifanikiwa kuandaa nyaraka za kubadilisha hati ya kiwanja hicho na kumilikisha rasimi marehemu na hivyo hati ya kiwanja ikabadilishwa kutoka jina la The Registered Board of Trustees Of EAGT, na kuwekwa jina la Rev John Henry Mfuko mmiliki halali wa kiwanja hichi na shule iliyopo katika kiwanja hicho ambayo pia imesajiliwa kwa jina la marehemu", alisema Frida 

Ameongeza, kabla ya kufariki baba yake alikuwa akihoji viongozi wakuu wa kanisa la EAGT kuhusu tuhuma za kuingiza magari nchini kwa kutumia jina la EAGT ikiwa magari hayo hayapo ndani ya umiliki wa EAGT na ukiwa kuna ukwepaji wa kodi ya Serikali

Aidha, watoto wa marehemu wamelaani kitendo hicho cha kutaka kuwafukuza na kuwanyanganya mali ya baba yao ikiwa viongozi wa EAGT wanajua fika kuwa kiwanja kile pamoja na majengo yaliyopo na shule ni mali ya marehemu Mchungaji Mfuko.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...