UPANDE wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi kuwa, wameshindwa kuwaita mashahidi kuja kutoa ushahidi wao leo, sababu mpaka sasa mashahidi watano waliotoa ushahidi bado hawajalipwa stahiki zao.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa ameeleza hayo leo Juni 3,mwaka 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba wakati kesi hiyo illipoitwa leo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka.
Amedai kuwa kesi hiyo leo ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa lakini wameshindwa kuwaita mashahidi wengine kwa sababu shahidi wa 9,10,11,12 na 13 ambao tayari walishatoa ushahidi wao bado hawajalipwa stahiki zao, hivyo ameiomba mahakama itoe amri kwa uongozi wa Mahakama ili mashahidi hao waweze kulipwa stahiki zao
Baada ya kutolewa taarifa hiyo, Hakimu Simba amesema watalitatua tatizo hilo sababu kesi hiyo ni ya muda mrefu na walikubaliana waletwe mashahidi wa kutosha ili kesi imalizike haraka. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 17 mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa na itaendelea kusikilizwa Juni 18, 20 na 24.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera. Gugai na mwenzake watatu wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo, makosa 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, ambalo linamkabili Gugai.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...