Kimsingi, VAT inayolipwa au Kurejeshwa hukokotolewa kama ifuatavyo:

VAT INAYOLIPWA/INAYOREJESHWA= VAT YAMAUZO – VAT YA UNUNUZI

Ambapo;
VAT ya UNUNUZI ni kodi inayolipwa na mfanyabiashara anaponunua bidhaa ambazo ataziuza kwa bei ambayo itampatia faida wakati VAT ya MAUZO ni kodi inayokusanywa na mfanyabiashara kutoka kwa wateja anapouza bidhaa zake kwa wateja wa mwisho.

Mazingira pekee yaliyopo ambayo Mlipakodi anastahili kudai marejesho ya VAT kutoka TRA ni pale ambapo VAT YA UNUNUZI inakuwa kubwa kuliko VAT YA MAUZO. Endapo VAT YA MAUZO ni kubwa kuliko VAT YA UNUNUZI, basi Mlipakodi/Mfanyabiashara anatakiwa kulipa tofauti hiyo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Mbinu zinazotumika kuongeza VAT ya Ununuzi

i. Mauzo “hewa” ya bidhaa nchi za nje

Mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi yanatozwa kodi kwa kiwango cha asilimia sifuri kwa madhumuni ya kumbukumbu za VAT. Hii inamaanisha kwamba, wakati bidhaa zinaposafirishwa kwenda nje ya nchi, kodi yote ya ununuzi inayolipwa wakati wa ununuzi wa malighafi na bidhaa nyingine zilizotumika inarejeshwa kwa msafirishaji/Mfanyabiashara mara tu usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi unapofanyika na fomu za madai ya marejeso ya kodi kuwasilishwa kwa mamlaka husika.  

Katika utaratibu huo bidhaa zinazodaiwa kuwa zimesafirishwa nje ya nchi zinakuwa hazikusafirishwa nje ya nchi kabisa, bali badala yake zinatumiwa humuhumu nchini. Mara nyingi wafanyabiashara hao wasio waaminifu wanawasilisha nyaraka za kughushi za kusafirisha bidhaa nje ya nchi katika idara ya Marejesho ya kodi ili waweze kudai kodi inayohusika. Pia, wafanyabiashara hao wanakula njama na maofisa wa Idara ya Forodha na Ushuru kutengeneza nyaraka za kusafirisha bidhaa nje ya nchi kwenye mfumo wa TRA, kuandika maelezo ya ukaguzi kwamba wameuona mzigo wa bidhaa na kuthibitisha kwamba bidhaa zimesafirishwa kwenda nje ya nchi kikamilifu wakati katika hali halisi hakuna mzigo wowote uliosafirishwa kwenda nje ya nchi.

ii. “Ununuzi “kutoka kwa Kampuni Hewa

Kampuni hewa ni kampuni ambazo zinasajiliwa kisheria na msajili wa kampuni  zikiwa na Namba halali ya Usajili ya VAT (VRN) lakini kampuni hizo kimsingi hazipo kabisa. Kampuni hizo hewa zinatoa tu Stakabadhi za kughushi kwa Wafanyabiashara. Katika utaratibu huo, Wafanyabiashara huonekana kama wamenunua bidhaa kutoka kwao (kampuni hewa) wakati katika hali halisi hakuna muamala uliofanyika (hakuna malipo ya bidhaa yaliyofanyika na hakuna usafirishaji wa bidhaa uliofanyika kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuzi).


iii. Ununuzi Hewa

Ununuzi huu hufanyika pale Mfanyabiashara/Mlipakodi anapoweka madai ya VAT kwenye fomu ya Ankara za Kodi kutoka katika kampuni ambazo zipo na zinafanya kazi lakini hakuna mauzo yoyote yanayofanyika. Jambo hili mara nyingi hutokea kwa kampuni ambazo zinahusika na sekta ya madini. Kampuni hizo hujumuisha katika madai ya VAT kampuni wenza ambazo mara nyingi Ankara hizo huwa zina thamani ya juu sana. Kuna mambo mawili ya kuzingatia hapa:

(a) Hakuna malipo yanayofanyika kwa ajili ya kununua bidhaa, hakuna bidhaa zinazochukuliwa kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuzi, bali ni Ankara ya kodi tu inayotolewa na  muuzaji  kwenda kwa  mnunuzi (Kampuni mwenza)

(b) Malipo yanafanyika, mzigo unachukuliwa kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuzi lakini bei ya bidhaa inayowekwa kwenye Ankara kwa ajili ya kutumika kudai marejesho ya VAT inakuwa ni ya juu mno.

Katika mazingira yoyote kutoka (i) hadi (iii) Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Ununuzi inakuwa kubwa sana kuliko VAT ya Mauzo na hivyo madai ya marejesho ya VAT kwa ajili ya VAT ya Ununuzi yanalipwa na wafanyabiashara wakati wa ununuzi au uzalishaji wa bidhaa zao.

Madhara ya Madai ya Marejesho ya VAT Yasiyo  halali katika Uchumi

i. Inapaswa ieleweke kwamba kiasi cha fedha za Ongezeko la Thamani (VAT) ambacho inabidi kirejeshwe kwa Mlipakodi/Mfanyabiashara ni kodi ambayo imekuwa ikikusanywa na kutambuliwa kama mapato kwa Serikali. Mapato hayo yanatumika kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi yetu. Kwa kurejesha fedha hizo kwa Mfanyabiashara/Mlipakodi tunapunguza uwezo wa Serikali wa kugharimia bajeti yake na hivyo, kuchelewesha shughuli za kijamii na kiuchumi katika nchi.

ii. Marejesho yasiyo halali yanadhoofisha sera ya fedha ya Serikali kwa kuweka fedha kwenye mzunguko wa uchumi ambao hauhusiani na matumizi ya kawaida ya fedha na hivyo kusababisha mfumuko wa bei.


iii. Jambo hilo pia linaweza kusababisha mazingira ya kutokuwa na ushindani wa haki katika uchumi wetu kwa sababu madai ya marejesho ya VAT yasiyo halali yanaonekana kama kupewa ruzuku na Serikali. Kwa hiyo, wakati ruzuku za serikali zinapotolewa kwa wafanyabiashara bila haki, hali hiyo inatoa mazingira ya ushindani yenye upendeleo kwa wale wanaopata ruzuku ya Serikali ukilinganisha na wale wasiopata ruzuku, kwa kuwa wanaopata wataweza kuuza bidhaa kwa bei za chini sana kutokana na gharama za uzalishaji kupunguzwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...