NA SULEIMAN MSUYA
MRADI
wa Kuleta Mageuzi Katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) maarufu 'mkaa
endelevu' umefanikiwa kuingizia halmashauri, vijiji na wananchi zaidi ya
shilingi bilioni 3 kuanzia 2014 hadi sasa.
Hayo
yamesemwa na Meneja Mradi wa TTCS, Leonard Charles wakati akiwasilisha
mada kwa maofisa mbalimbali kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Serikali Kuu walikutana mkoani Morogoro.
Meneja
huyo amesema mradi wa TTCS unatekelezwa katika vijiji 30 vya wilaya za
Mvomero, Kilosa na Morogoro chini ya usimamizi wa Shirika la Kuhifadhi
Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Kusimamia Misitu
Tanzania (Mjukita), Shirika la Kuendeleza Nishati Asili Tanzania
(TaTEDO) na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC).
Amesema
katika mradi huo vijiji 22 vimeanza kunufaika katika pande mbili ambazo
ni kiuchumi na utunzaji wa mazingira huku nane vikiwa katika mchakato.
Ameongeza
hadi kufikia mwezi Mei 2019 vijiji vimeweza kikusanya mapato halali
zaidi ya shilingi bilioni 1.4, wachomaji mkàa shilingi bilioni 1.2 na
halmashauri shilingi milioni 500.
Ametaja
baadhi ya vijiji ambavyo vimenufaika na mradi ni Ulaya Mbuyuni, Matuli,
Kitunduweta, Mlilingwa, Ulaya Kibaoni, Diguzi na vingine.
Leonard
amesema mradi wa mkaa endelevu ulianza Machi 2012 katika vijiji 10
lakini baada ya kuonekana mafanikio wamelazimika kuongeza vijiji hadi
kufika 30.
"Mradi wa TTCS
maarufu mkaa endelevu umefanya mapinduzi makubwa kiuchumi, kijamii na
maendeleo katika vijiji vilivyopo kwenye mradi kama kuboresha sekta ya
afya, elimu, maji, kilimo na mitaji," amefafanua.
Ameongeza
mafanikio ya mradi yamezingatia kutoa elimu kwa jamii husika, watendaji
na wafanya maamuzi hivyo kurahisisha utekelezaji.
Amesema
pia utekelezaji unazingatia uwepo wa mpango wa matumizi bora ya ardhi
za vijiji, kutenga maeneo madogo ya mradi na kuvuna kwa kutumia
vitalu.Pia mradi umefanikisha ujenzi wa ofisi za vijiji hali ambayo
inarahisisha usimamizi wa mradi.
Kwa
upande wake Ofisa Uhusiano wa TFCG, Bettie Luwuge amesema warsha hiyo
ya siku tatu imelenga kujenga uelewa kwa pande zote ili kurahisisha
utunzaji wa misitu nchini.
Luwuge amesema rasilimali misitu ikitunzwa kwa ushirikiano wa wadau wote inaweza kubadilisha jamii kiuchumi na maendeleo.
"Tumeamua
kukutanisha maofisa kutoka sekta ya kilimo, misitu, maliasili na sheria
wa wilaya 19 lengo ni kuweza kubadilishana mawazo namna ya kutunza
misitu yetu ili iwe endelevu," amesema.
Amezitaja
wilaya husika kwa warsha hiyo ni Kigoma, Kilwa, Tabora, Namtumbo,
Handeni, Kilindi, Mvomero, Morogoro, Kilosa, Lindi, Liwale, Tunduma,
Kilolo, Ruangwa, Nachingwea, Mpwapwa, Songea, Nyasa, Mbinga.
Awali
akifungua warsha hiyo Ofisa Misitu wa Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa
alisema warsha hiyo itasaidia kuongezea uelewa maofisa hao kuhusu
utunzaji misitu ya vijiji.
Chuwa alisema rasilimali mali misitu ikitunzwa kwa dhana ya uendelezaji itasaidia jamii kuinuka kiuchumi.
Meneja Mradi wa TTCS, Charles Leonard akitoa mada kuhusu Mkaa endelevu kwa maofisa mbalimbali kutoka wilaya 19 nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...